KUHUSU MIMI

      Dr. Chris Mauki ni mkufunzi “Lecturer” katika idara ya saikolojia ya chuo kikuu cha Dar es Salaam. Dr. Chris ni mtaalam na mwalimu wa saikolojia ya jamii pamoja ushauri wa kisaikolojia. Mbali na kufundisha ushauri wa saikolojia Dr. Chris Mauki pia amewasaidia wengi kupitia ushauri wa kisaikolojia (professional counseling) katika maeneo mbalimbali ya maisha kama vile ndoa, mahusiano, matatizo ya kitabia, uzazi na malezi, matayarisho ya kustaafu, ushauri wa mambo ya kazi, namna za kuishuhulikia misongo ya mawazo, na mengine mengi. Kwa utaalamu wake wa saikolojia ya jamii na ushauri wa kisaikolojia Chris Mauki amefanya kazi kwa karibu sana na taasisi nyingi za kiserikali na zisizo za kiserikali. Kwa sasa Dr. Chris Mauki pia ni mtaalam mshauri wa kampuni ya ICAS South Africa inayoshuhulika na masuala ya kisaikolojia ya wafanyakazi wa taasisi za fedha hapa nchini.
Dr. Chris Mauki mekuwa akitumia muda wake mwingi katika mikutano ya uhamasishaji wa masuala ya maisha (motivational talks), badhi ya mikutano na makongamano haya yamekuwa yakiandaliwa nayeye mwenyewe, na mengine mengi amekuwa akitumika kama mzungumzaji mwalikwa. Maeneo ambayo amekuwa akiyazungumzia na kuyafundisha kwenye mikutano na makongamano haya ni kama vile; Njia bora na malezi, mahusiano, usuluhishi na utatuzi wa migogoro katika mahusiano, mbinu za kuukomboa na kuutumia muda kiufanisi, jinsi ya kujiwekea mipango na malengo katika maisha, maisha baada ya maisha ya chuoni, uongozi, saikolojia ya watoto, na mbinu za maendeleo binafsi. Baadhi ya mafundisho haya yanapatikana katika mfumo wa santuri (CD na DVD). Kitabu chake cha kwanza kinachozungumzia mambo haya kwa undani zaidi kiko katika matayarisho.
 Katika jitihada za kutanua wigo wa vipawa na talanta zake Dr. Chris Mauki amejihusisha sana na vyombo vya habari. Kwa zaidi ya miaka mine amekuwa akiendesha program  inayoitwa “Saikolojia ya Maisha” katika kituo cha Praise Power Radio 99.2 FM, mara kwa mara amekuwa mwalikwa katika mazungumzo maalum katika vituo vya Clouds FM, WAPO FM, East Africa Radio na vingine pia. Dr. Chris Mauki amekuwa mtangazaji wa kipindi cha Televisheni kiitwacho Five Connect (5connect) kinachorushwa na EATV ambacho kimekuwa kikishuhulikia mambo mengi yahusuyo vijana na maisha ya kilasiku. Mbali na redio na televisheni Chris Mauki pia amekuwa akiandika makala zihusuzo saikolojia ya maisha katika magazeti ya Global Publishers. Maisha ya wasomaji wengi wa makala hizi, ndani na nje ya Tanzania yamebadilika na kuboreka zaidi.
 Pamoja na majukumu mengine nje na kazi za kitaaluma, Chris Mauki anahusika pia na kupanga na kuratibu shuhuli na matukio mbalimbali (MC), yakiwemo ya kiserikali, makampuni na ya kijamii. Chris Mauki amekuwa msaada pia katika kazi za kutafsiri lugha za kiingereza na Kiswahili (oral and written).
 Kielimu, Dr. Chris ana shahada (BA) ya sanaa na elimu, shahada ya uzamili (Masters) ya saikolojia ya jamii na sasa yuko masomoni katika shahada ya uzamivu (Ph.D) ya masuala ya matatizo ya ndoa na madhara ya kisaikolojia kwa watoto.
 Kimajukumu, Dr. Chris Mauki anafuraha kuwa mume wa Miriam Lukindo Mauki na wawili hawa wamebarikiwa  watoto wawili wa kike Rommy na Ronel