DARASA LA ALHAMISI NA DR. CHRIS MAUKI: BAADHI YA DALILI ZA KUKUONYESHA KUWA MAPENZI YA MWANAUME YAMEKWISHA KWAKO

BAADHI YA DALILI ZA KUKUONYESHA KUWA MAPENZI YA MWANAUME YAMEKWISHA KWAKO

DALILI YA 1

Mwanaume anaanza kuonyesha hasira na kuhamaki kwenye kila unachokifanya hata kama ni kitu kidogo. Hii ni kwasababu penzi limempungua au kumuisha na hivyo anakosa uvumilivu kwako. Anaweza kukupayukia hata ukiwa katikati ya watu na wala hatojali unavyo jisikia kwa yeye kufanya hivyo. Utashangaa na kujiuliza mbona huko mwanzoni aliweza kunivumilia? Jibu ni kwamba penzi limepoa au kuisha

DALILI YA 2.

Kwa kawaida mwanaume anavyompenda mwanamke huwa na kiu ya kumfurahisha,  hufanya vitu kuhakikisha mpenzi wake anatabasamu na anajisikia murua. Kilasiku kiu ya mwanaume ni kuona mwanamke huyo anatamani kuendelea kuwa ndani ya penzi hilo. Mapenzi yakiisha vitu hivi vyote vinayoyoma na kupeperukia mbali

DALILI YA 3.

Mapenzi ya mwanaume yanapokwisha kwa mpenzi wake anakosa kabisa kuwa na muda naye. Mwanzoni mlikuwa mnakuwa na muda wa pamoja sasa hapati tena muda huo na kila ukiuliza unapewa visingizio kibao, mara kazi, mara ubize, mara safari, mara kuumwa au kuchoka n.k. Yani inakuwa ni bora autumie muda wake akiwa na marafiki zake kuliko kuwa na wewe. Vile vicheko vya pamoja mkiwa peke yenu vyote vinakwisha. Ukiona hivyo ujue hiyo taa nyekundu ndugu yangu

DALILI YA 4.

Dalili hii yaweza kufanana kidogo na nyingine niliyokwisha isema. Mwanaume anapoacha kumpenda mwanamke hupunguza sana au kuacha kabisa kumjali na kumhudumia mpenzi wake. Inakuwa ngumu kwake kukufanya ujisikie mwanamke au ujisikie uliye maalumu kwake. Atawatendea wengine mema na kuwajali lakini sio wewe. Zile bashasha na malavidavi aliyowahi kuwanayo hutoyaona tena

DALILI YA 5.


Mapenzi ya mwanaume yanapopungua au kuisha kwako utaona jinsi inavyokuwa ngumu kwake kuwasiliana na wewe. Unapomwonyesha umuhimu au uhitaji wako wa mawasiliano yeye anaona ni mzigo mkubwa. Anakuwa mzito sana kuzungumza, mgumu kuzionyesha hisia zake kwako, mara nyingine inakuwia ngumu kugundua lini amefurahi na lini amekasirika. Zamani alikusikiliza, sikuhizi hakusikilizi tena. Zamani ulijua alipo na anachofanya sikuhizi ukiuliza unazua ugomvi. Ukiona hivi ni dalili kuwa penzi lake kwako limeshapata shida

DALILI YA 6.


Mwanaume anapompenda mwanamke humruhusu mwanamke huyo kuyajua maisha yake yote. Maisha ya mwanaume huyu yanakuwa kama kitabu kilichowazi. Hafichi kitu wala kuishi maisha ya kona kona. Tofauti yake ni kwamba mapenzi yakimwisha utaona siri zina kuwa nyingi, haujui nini kinaendelea kwenye maisha yake na wala haoni umuhimu wa kukushirikisha kinachoendelea kinachomhusu yeye

DALILI YA 7.


Penzi la mwanaume linapoisha juu yako mara nyingi huwa anaona shida kukushirikisha kwenye maisha yake au yeye kushiriki maisha yako. Furaha yake inakuwa yake na yako inabaki kuwa yako wakati mwanzoni furaha ya kwako ilikuwa furaha yake. Ukifanikiwa kitu nayeye anajisikia furaha lakini sio sasa. Inapofikia hapa utaona mnakaa nyumba moja kama wapangaji wawili na sio mtu na mwenza wake. The love is depleted

Na: Dr. Chris Mauki

Mtaalam wa saikolojia na mahusiano

University of Dar es salaam

0713 407182

Chrismauki57@gmail.com

www.chrismauki.com

 Dr. Chris Mauki. An expert in Relationships, Social and Counseling Psychology. Lecturer in Psychology: UDSM. Inspirational & Motivational speaker. Family man


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *