DARASA LA ALHAMISI NA DR. CHRIS MAUKI: JINSI YA KUJIJENGEA UWEZO WA KUFANYA MAAMUZI YALIYO BORA

JINSI YA KUJIJENGEA UWEZO WA KUFANYA MAAMUZI YALIYO BORA

Katika Maisha yetu ya kila siku mara nyingi tunajikuta katika mazingira yanayotulazimu kufanya maamuzi magumu au kuchagua kitu katikati ya vitu vingi ambavyo vinatuchanganya akili.  Wengi wetu kwa ugumu huu wamejikuta wakifanya maamuzi mabovu na kuchagua chaguzi mbovu ambazo ama ziliwapa hasara  au ziliharibu kabisa muelekeo au mustakabali wa maisha yao.  Ndio maana wenzetu wa magharibi (Ulaya) wanamsemo usemao “Life is how you make decisions” Maisha ni vile unavyofanya maamuzi.

Tunavyofanya maamuzi fulani, hususani katika kuchagua vitu  kati ya vingi  hatumaanishi vyote au vile vingine ni vibaya bali hatuwezi kuvichagua vyote kwa wakati mmoja na hivyo tunalazimika  kufanya maamuzi ya kuanza na kimoja na  kumalizia na vingine.

Mfano: Msichana aliyeomba kazi na wakati huo huo ameomba nafasi ya chuo na pia yuko katika mahusiano na mchumba wake anayehitaji waowane.  Hali hii inamfanya msichana huyu kuwa katika wakati mgumu wa kufanya maamuzi nini afanye kwanza na nini kifuate badae.

Daima huwezi kufanya vitu vyote vilivyo mbele yako, huwezi kuchukua kila fursa inayokujia  lazima uwe na uwezo wa kufanya maamuzi yaliyo bora.  Maamuzi haya  yatachangia sana katika kufika mwisho wenye ushindi au katika  kufikia mwisho wenye majuto na machozi.

 

Katika makala hii nitajaribu kukupa mbinu tofautitofauti ambazo zitakuwezesha kufanya maamuzi yako kwa haraka, kwa ubora na bado ukawa katika uwezo wa kuyasimamia maamuzi hayo.

 1. Angalia na zitafute fursa mbalimbali
  • Jambo la kwanza ni uwezo wa kuzidaka fursa pale zinapojitokeza
  • Jambo la pili ni uwezo wa kuzitengeneza fursa wewe mwenyewe

Katika jambo la kwanza, la uwezo wa kuzidaka fursa, namaanisha kuwa, baada ya kueleza au kutangaza kwa marafiki  na kupitia njia mbalimbali kuwa unataka au kutafuta kitu au kazi  fulani, haupaswi kukaa tu kimya na kulala, fursa zaweza kwanza kuja kupitia marafiki zako, wafanyakazi wenzako, au kupitia matangazo uliyoyafanya maeneo mbalimbali, sasa  hapa haustahili kulala bali kuzidaka na kuzifanyia kazi fursa hizo.

Katika jambo la pili, namaanisha uwezo wa kuzitengeneza fursa wewe mwenyewe.  Kama kweli unahitaji kitu lazima ufungue macho kutafuta nini tatizo la jamii inayokuzunguka, wakati wote tatizo au hitaji la jamii laweza kugeuzwa kuwa fursa.  Mfano, kama sehemu ni kame na maji ni tatizo jitahidi kuchimba kisima, kwa kutatua tatizo lililosumbua jamii umepata fursa ya kufanya biashara.  Usikae tu na kusubiri fursa zijihudhurishe miguuni pako zenyewe. “run for them”.

 

Njia zote hizi mbili hazinabudi kutiliwa mkazo na kila mtu.

 1. Jizindue wewe mwenyewe

Mara nyingi tunasikia neno uzinduzi.  Hapa naamanisha tendo la kuchukua na kuuendea mkondo uliouchagua ukutoe kimaisha.  Anza kupiga mbio  kwenye njia unayoona itakutoa.  (fanya uzinduzi wako mwenyewe bila kusubiri ufanyiwe).  Ili kuweza kujizindua pasipo kuchelewa, lazima kufuata ushauri ufuatao.

 • Jiulize Swali “Ni nini?”.

Kila wakati jiulize ni nini ninachotaka kukifanya na katika hiki ninachotaka kukifanya, ni nini  ninachotaka kukipata?

Unaporuhusu akili yako kufahamu ni nini unachotaka kukipata, unauruhusu mwili na nafsi yako kujitia nguvu tayari kwa kukiendea hicho kitu.

Faida nyingine ya kujiuliza ni nini ninachokitaka ni kukupa picha ya ukubwa au umuhimu wa kile unachokitaka ili uweze kuandaa kila kinachowezekana kama vile rasilimali vitu au rasilimali watu, au rasilimali fedha ili kuhakikisha unakipata kile unachokihitaji.

 • Uwe tayari kupata hasara! (be a risk taker)  Kama wewe ni mwoga wa kushindwa au mwoga wa kupata hasara kamwe hutoweza kujizindua kwa haraka.  Kwa ajili hii lazima ujue jinsi ya kushuhulikia hizo hofu zako. Usiogope kupata hasara katika chochote ufanyacho maana kupitia hasara tunajifunza mbinu bora zaidi za kuitafuta faida kubwa.
 1. Yatumie vema na kwa ufanisi maamuzi yako.

Ili uweze kuyatumia vema na kwa ufanisi maamuzi yako, tu utumie mfano huu. Jifikirie umebeba glasi tupu mkononi mwako, waweza kuijaza glasi hiyo kwa majuto na lawama za uliyowahi kuyafanya au  waweza kuijaza kwa yale uliyojifunza huko nyuma kwaajili ya kesho yako. Kama utabaki kujuta na kulaumu yaliyopita au uliko sasa hutofaidika chochote kiujuzi kwa ajili ya kesho yako.  Lakini kama utafanya kila unalokutana nalo kuwa ni somo utapata ujuzi tele kwa kesho yako.

Pinga tabia ya kulaumu na kujutia maamuzi yako kwa kuzingatia ukweli kwamba

 • Mambo mengi hutokea au hutegemea na mitazamo uliyonayo.

Maamuzi mengi tufanyayo hutegemea na mitazamo tuliyonayo maishani.  Kama mtazamo wako ni wakujutia kila kitu au kulaumu wengine, basi utalaumu na kujutia  kila utakachowahi kukifanya, mfano; utajutia na kulaumu  kozi unayosoma, kazi unayofanya, biashara unayofanya, mke au mume mliyeoana nae, watoto uliowazaa nk.

 • Maamuzi ufanyayo yanategemeana sana na mfumo wako wa maisha. maamuzi yako maishani hutegemea sana na kile unachokiamini. Kile ulichotayari kukisimamia na kukitetea, hutegemea sana uasili wa maadili yako, kupitia hivi vitu tunapata maamuzi mabaya au maamuzi mazuri. Mfano; maamuzi ya mtu mwenye maaadili ya kidini ni tofauti na maamuzi ya yule asiye na dini.
 1. Jifunze kufanya uamuzi

Jitahidi kuweka misimamo na malengo sahihi katika maisha yako.

Jaribu kuwa na msimamo fulani badala tu ya kuelea elea tu hewani ukisubiri wengine wakusaidie kuamua.

Jitahidi kuyatetea na kujasimamia maamuzi uiliyofanya.

Yathibitishe maamuzi yako kabla hujaamua kuyaacha na kufuata maamuzi mengine.

Anthony Robbins – Mwandishi na mhamasishaji maarufu ametoa maana halisi ya neno maamuzi (Decision).  Anasema neno hili limechimbuka toka maneno mawili ya kilatini “de”- ikimaanisha “from” (kutoka) na “caedere”-ikimaanisha “to cut” (kukata) kwa ujumla wake inamaanisha wakati tunapofanya uamuzi wowote tunazikatilia mbali fursa nyingine zozote na kuchukua ile tu tuliyoiamua.  Mfano mzuri unapoamua kumuoa binti fulani, hatakama uliwapenda wengi unalazimika kuwasahau wengine wote.

Pasipo kufanya jambo hili utakuwa hufanyi uamuzi bali ni matamanio tu.  Fahamu dhahiri kuwa uamuzi wakweli unamaanisha kujitoa, kujifunga katika lile uliloliamua.  Na sio suala la kubahatisha tu.

Unafanyaje pale unapojikuta umefanya maamuzi yanayosababisha tatizo

Sio wakati wote maamuzi tunayoyafanya yanatufikisha pazuri au kutuletea matokeo mazuri.  Maranyingine unajikuta mara tu ulipoamua kujizindua  mwenyewe, maamuzi hayo yanakutupa kwenye hasara au majuto. Unafanyaje hili linapotokea?

Ushauri!

 • Amini ujasiri wako
 • Nikosa kubwa sana kujikosoa na kujisuta na kuusuta ujarisi uliokuwanao mara tu baada ya kujiona umefanya kosa. Fahamu kwa wakati wowote unapofanya jambo la kijasiri kuna mambo mawili, labda upate matokeo mazuri au upate matokeo mabaya.  Lakini, kupata matokeo mabaya kwa sasa hakubadili ukweli kwamba kile kilichofanyika kilifanywa kwa ujasiri.

Ruhusu kushindwa kwako kuwe kitu cha kukukumbusha kwamba yote hayo unayoyapitia ni matokeo ya ujasiri wako.  Kama usingekuwa jasiri usingejaribu.

 • Jiambie mwenyewe kwamba bado utaendelea kuishi.

Usalama wa kweli hautokani na kule kupata vile tunavyovihitaji, bali katika uwezo wa kustahimili zile nyakati tunazojikuta tukizipitia.

Kama unaimani basi amini kwamba bado Mungu yuko na wewe.

Wawezajikuta unapata kazi kubwa na yenye uhakika sana na ukajikuta unaitegemea hiyo na kesho yake kampuni inafungwa au kufa.

 • Chukua masomo yaliyo muhimu katika changamoto za maisha

Katika kila hali tunayopitia hakuna cha kuacha kisichokuwa shule nzuri itakayo kusaidia kesho.  Jifunze kuyatazama mapito magumu kama darasa la kujifunza kustahimili kesho, yamkini isiwe shule itakayokusaidia wewe,  lakini kwa kuyajua hayo uliyiojifunza utawakwamua wengi watakao kwama katika tope linalo fanana na lakwako  kesho.

Katika mapito haya Jifunze ni nini chakukirudia tena kesho na ni nini kisicho faa kurudiwa tena. Sehemu ya Maisha yenye mafanikio ni pamoja na uwezo wa kujifunza na kukua kutoka uzoefu hadi  uzoefu.

Na. Dr. Chris Mauki

Social, Relationship & Counseling Psychologist

Email: chrismauki57@gmail.com

www.chrismuki.co.tzDr. Chris Mauki. An expert in Relationships, Social and Counseling Psychology. Lecturer in Psychology: UDSM. Inspirational & Motivational speaker. Family man


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *