DARASA LA ALHAMISI NA DR. CHRIS MAUKI: JIFUNZE NAMNA YA KUJISAIDIA MWENYEWE (Self Help Skills)

JIFUNZE NAMNA YA KUJISAIDIA MWENYEWE

(Self Help Skills)

 

Utafiti uliofanywa katika maeneo mengi katika nchi zilizo endelea na zinazoendelea unaonyesha kuwa watu wengi bado wanahitaji kiwango kikubwa cha uwezo wa kujisaidia wenyewe.  Hata katika nchi kama marekani ambayo teknolojia ni kubwa lakini watu pia wanakiu kubwa ya jinsi ya kujua kujisaidia wenyewe katika baadhi ya mambo yanayowasibu kimwili, kihisia na maisha kwa ujumla.

Wachunguzi wakubwa wa maswala ya kisaikolijia Richard na Tony Robbins wanaafiki kwamba yawezekana kabisa tukarekebisha na kuweka sawa vile visivyokaa sawa katika miili yetu au akili zetu pasipo kutegemea msaada wa daktari au mshauri.

Watu wengi ulimwenguni wanapata msada wa ujuzi huu kupitia kuenea kwa mtandao wa intanet na vitabu vya ujuzi huu vilivyo vingi sana (self help books).

Takwimu zinaonyesha wamarekani walitumia zaidi ya dola 563 milioni kwa manunuzi ya vitabu vya ujuzi wa kujisaidia mwenyewe, na pia zaidi ya tovuti 12000 za masuala ya afya ya akili “mental health” hutumika nchini marekani.  Yote hii ni watu kutafuta uwezo wa kujisaidia zaidi ya kutegemea kusaidiwa  hasa katika mambo ya afya ya akili, hisia ,nk. Zaidi ya 40% ya tovuti za masuala ya afya kutumiwa na watu hasa katika kutafuta kufahamu juu ya tatizo la kupoaaza moyo na upweke (depression).

Huu ni wakati wa kila mmoja kujua jinsi ya kurekebisha maumivu yake na kuponya majeraha yake mwenyewe. Hii  inawezekana.

Habari au taarifa nyingi za namna ya kujisaidia binafsi zimekuwa zikikosewa na kutafsiriwa tofauti mara nyingi.  Hii ndio maana wengi wamekuwa hawatilii maanani na pia wengi kutopata matokeo halisi yanayotarajiwa.  Safu ya gazeti hili leo inakwenda kukufungua na kukusaidia.

Yafuatayo ni baadhi ya maeneo katika maisha yetu ya kila siku ambayo huleta matatizo kwa kushindwa kuwa na ujuzi wa kujisaidia wenyewe.

 

1.Unapokuwa Katika Hasira Kali.

Kama vile yalivyomatundu katika kuta kubwa kwa ajili ya kupumulia hewa na kupunguza presha  katika ukuta huo ili usije pata nyufa  (ventilations) ndivyo hivyo mtu mwenyehasira  kali hutakiwa kujua jinsi ya kuyaruhusu mazingira aliyopo yaweze kumsaidia kuipumulia nje ile hasira pasipo kuleta madhara kwake yeye na wale wanaomzunguka  (venting anger)

Tumeona sana katika filamu au vitabu vya  asili ya nchi za magharibi wengi wakiwa katika hali hii hukumbatia au kung’ata au kupiga ngumi mito ya kulalia (pillow) au wengine hutupa ngumi katika mfuko wa mazoezi ya kupigana (punching bag) katika hali hii hasira kali hupata pakupenyezea na kupoa.  Watalaam wameshauri kutumia nguvu zote kutupa ngumi au kupiga mito hii au puching bag na kama ni mtu amekuudhi basi fikiria kuwa unauona uso wake katika mto huo na uiachie hasira yako kimwili (kwa kupiga)  na kimaneno kwa kuongea yale yote yaliyo moyoni mwako. Watafiti wanasema aina hii yaweza pia kuwa msaada kwa kupunguza msongo wa mawazao mbali na hasira.

Tafiti za hivi karibuni zimeonyesha mtazamo wa tofauti kidogo katika hili.  Dr Brad Bushman  mwanasaikolojia  wa Iowa state university anasema watu wengi hufikiri kwa kufanya hivi wanafanikiwa kupona hasira ila wale wachache ambao inashindikana wanakuwa na hasira kali maradufu na kuchanganyikiwa.

Baadhi ya tafiti zimeonyesha kuwa kukosewa kwa namna ya kuipunguza au kuitoa hasira kumewasababishia wengi matatizo ya misuli ya kichwani na hivyo kuhatarisha akili zao.

Nini Kifanyike Basi

 1. Jaribu kufanya chochote kile ambacho chaweza kikachukua nafasi ya hasira moyoni, kila mtu anakitu anachokipenda, kifanye hicho sasa, kwa mfano; kuangalia filamu, picha, kusoma au kusikiliza hadithi au kusikiliza nyimbo unazozipenda, jihadhari kukaa karibu na yule aliyekukwaza mpaka mmesuluhisha yaliyowasibu.
 2. Pata muda wa kucheka na marafiki wengine, kama ni baba pata muda wakutoka na watoto wako, hawa wananafasi kubwa ya kukuingia moyoni kwa haraka na kusafisha hasira uliyonayo.
 • Usikimbilie sana kwenye mazoezi ya viuongo kwasababu utafiti wa Dr. Bushman unaonyesha kuwa mazoezi ya viungo yananafasi kubwa ya kuiamsha hasira, wengi waliotafitiwa walienda kupigana mara tu baada ya kumaliza mazoezi ya viungo.
 1. Michezo ya kijadi kama vile tai, chi, na yoga yaweza kuwa msaada wa kurekebisha hisia na hali ya akili, ni vema ukafanya michezo hii kama unaujuzi nayo na kama inaruhusiwa na imani yako, kwa sababu mingi iko zaidi katika imani za dini za nchi za bara Asia.
 2. Muendelezo wa kufanya kazi au shughuli itakayochukua muda mrefu wa kufikiri na kuifanya bize akili yako inaweza kupooza hasira pia

 

2. Unapokuwa Umefadhaika, Umepooza, Unahuzuni na Kuvunjika Moyo

Tafuta sana kufikiria yale yaliyo mema na ya kukutia moyo.  Peleka moyo wako katika yale yanayokupa furaha zaidi kuliko katika yale yanayovunja furaha yako. Funga milango yako ya akili, usiruhusu chochote kisicho cha furaha kuingia ndani. Tumia ubongo wako kufikiri kuwa yote yanawezekana                (optimistic thinking).

Teka uwezo wa akili na fikra zako na uzielekeze kule tu unakopenda wewe,

usiruhusu kamwe watu au mazingira yakuletee picha inayokuumiza moyo

Tafiti zinaonyesha kuwa mara nyingi tunapokuwa katika huzuni na kuvunjika moyo kila kitu huonekana kinyume nasi.  Nguvu ya ubongo nayo inashindwa kuyadidimiza yale yaliyo mabaya ili tusiyawaze.  Na kila tunapojaribu kujitahidi wenyewe kuikataa hali hii mawazo na mitazamo ya kufeli na kushindwa hujaza fikra zetu.  Mara unapojaribu kufikiri yale mema moto huwa mkali zaidi na kuona kuwa wewe ni wakushindwa zaidi.

 

Ufanye nini Basi?

 1. Pata muda zungumza na marafiki, watu wa dini (wachungaji, mapadri, shekhe, washauri au yeyote anayeweza kukupa mitazamo ya tofauti na kukuwezesha kuwaza mambo mengine.
 2. Nenda katika maeneo ambayo watu wanafurahi, kama vile sherehe, ufukweni, hotelini, super market au katika maduka makubwa, taratibu utaona roho na nafsi yako vinanyanyuka upya.
 • Na kama unajua kuwa kunakitu kitakuudhi na kuharibu furaha yako panga vitu vingi vilivyo vyema na vyakukujenga utumie muda kuviwaza hivyo.

 3. Unapojihisi Kupoteza Mwelekeo wa Maisha

Kumbuka na uyafikirie tena na tena malengo yako, hii itakuwezesha kuyafanya yawe kweli. Pata mawazo na picha ya wewe ukifanikiwa na sio ukishindwa, iache picha hiyo ikae katika akili yako, itakusaidia kuyafanya matendo yako yapiganie uhalisi wa kile kilichopo akilini mwako.

Kwanza tu kuwa unafanikiwa hakutoshi, hapa ninazungumza pia na wale wenye imani zao kali za dini ambao hukesha wakiamini wanafanikiwa na wamekwisha fanikiwa na wakati hakuna wanachokifanya, lazima ufanye mabadiliko yakimtazamo lasivyo kifo kitakukuta hapo hapo ukiwaza unafanikiwa wakati watu wanakuona wewe kama mfano mzuri wa walioshindwa maisha.  Lazima picha ulionayo ya kufanikiwa itiwenguvu na matendo(actions) ya kila siku katika kuifanya ndoto yako kuwa halisi “to make your dream come true”

Shelley Taylor, Daktari wa saikolojia wa chuo kikuu cha UCLA Marekani ameonyesha kuwa katika kufikiria tu kuwa unafanikiwa  na kuliwekea picha lengo lako katika akili bila matendo ina athari mbili; Kwanza inalitenganisha lile lengo mbali na kile kinachohitajika kufanywa ili lengo lifikiwe, na pili inakufanya ufurahie utamu wa kuwa mtu aliyefanikiwa wakati bado kabisa hujafika popote,  hali hizi zinafifisha nguvu ya lengo lako (power of the goal) na kukufanya kushindwa kujitahidi kufanya kazi na kukubali kupoteza (to take risks) katika kukipata kile ambacho kiko katika ndoto zako za kila siku.

 

Nini kifanyike?

 1. Pamoja na kuwaza kila siku na kuwa na ndoto za mafanikio, pata wakati jiulize ninini unaweza kufanya ili kufikia mafanikio hayo, na ukipata njia au mbinu hizi anzia kuzifanyia mazoezi akilini kabla ya kuziweka katika uhalisia.
 2. Kwa malengo ya muda mfupi waweza kupitia hatua zote ulizo zipanga ndani ya siku moja kabla ya kuanza kuzitendea kazi. Lakini kwa malengo makubwa na yamuda mrefu unaweza kupitia mipango yako tena na tena kadri unavyozidi  kuendelea na mchakato mzima na uone kama kunahitajika marekebisho.

4. Unapokuwa na hali ya Kutojithamini na Kutojipenda (Low Self Esteem)

Jitambue ya kuwa wewe ni wathamani na ni mtu bora zaidi.  Hii itakuwezesha kujithamini na kujipenda. Jifunze kuandika maneno ya ushindi yanayoonyesha ujasiri na ukakamavu (affirmation) kwa mfano viko vikaratasi vidogo vya kunatisha (stickers) katika kuta au katika magari vinamaneno “every thing is possible” vikimaanisha kila kitu kinawezekana.  Nyingine zimeandikwa “I can do it’ (ninaweza), nakumbuka nimeona katika gari la rafiki yangu kikaratasi  cheye maneno ya dini “nayaweza yote katika yeye anitiaye nguvu” maneno haya na mengine mengi yawe ya dini au yakutungwa au waweza kuandika mwenyewe na kubandika katika ukuta wako, kioo cha kujitazama, katika mlango wa friji yako, ndani ya gari lako, pembeni ya kitanda au bafuni.  Kwa teknolojia ya sasa unaweza kuyarekodi maneno haya na yakasema katika redio yako mara kwa mara au kuyaandika  katika compyuta yako yakawekwa kama “screen saver”  ili mradi tu kila unapogeuka unayaona yanasema na wewe.  Maneno haya yana nguvu ya kupenyeza ujumbe ndani ya fikra na moyo wako na kuruhusu mwili wako kudaka na kuyatendea kazi.

William Swann, daktari wa chuoo kikuu cha Texas anasema mtazamo huu unaweza kuwa mgumu kidogo na sio wote wanaweza kufanikiwa katika hili kwasababu kubadili jinsi tunavyojihisi wenyewe ni kazi ngumu sana.

Hali ya kujithamini na kujipenda inategemea mambo mawili; Kwanza hisia zetu za jinsi gani tunavyojipenda, na pili hisia zetu za uwezo gani tulionao katika kazi zetu na shuhuli nyingine zinazohitaji ujuzi na vipawa vyetu. Katika hili matumizi ya maandishi yanayoonyesha ushindi na kuweza (affirmations) yaweza kufanikiwa kwa baadhi ya watu lakini pale yanaposhidwa kufanya kazi huweza kumuacha mtu akiwa ameumia moyo zaidi.

Mara nyingi wale wenyemitazamo mibovu kuhusu wao wenyewe hawajiamini na hawaamini kama waweza kusema au kufanya  kitu bora hata siku moja kwa jinsi hii hata kama wakiandika vimaneno vingi vilivyo vya kutia moyo bado hawatakuwa na imani maana wanachokijua wao ni kwamba kamwe hakuna  chema kitakachoweza kutoka kwao. “Nothing good shall ever come from them”

 

Nini kifanyike basi?

 1. i) Njia pekee ya kubadilisha matunda ya vile tunavyojihisi au tunavyojithamini ni kubadili vile vinavyotuingia na kutengeneza ile hali ya jinsi tunavyojiona. Kwamfano; kama unajikuta unashindwa kujithamini au kujipenda sababu ya wale unaohusiana nao   au unaokuwa nao zaidi, basi badilisha,chagua watu wengine wakuhusiana nao, labda hao watasema yaliyobora kuhusu wewe na kukutia moyo zaidi.  Kama uko katika ajira ambayo kila mtu anakuona wewe hujui na wewe niwakushindwa tu, amua kuwataka wabadili mtazamo wao kwako au ikibidi  ondoka pata kazi sehemu ambayo watu wanamtazamo mzuri kwako.  Jaribu kufanya kazi yako vema zaidi ya ulivyoifanya kule kwa awali.
 2. ii) Simama ujitetee mwenyewe usingoje kutetewa “stand for yourself”

hakikisha unazungukwa na watu wanaokuona kuwa wewe ni wathamani, unayeweza, na ni mtu mwema. Hakikisha wanalikiri hilo kwa vinywa vyao. Uwe mvumilivu na wakati wote jitahidi kutimiza majukumu yako ili usiwavunje moyo wale wanokuona wewe kuwa mtu mwema na wanayekuamini. Fahamu kuwa jinsi tunavyojiona sisi wenyewe, na mtazamo tulionao kuhusu sisi wenyewe (self esteem) ni mjumuisho wa jinsi tunavyohusiana na watu wanaotuzunguka kwa muda tuishio hapa  duniani na kwamwe hauwezi kubadilika kwa usiku mmoja.

 

 1. Unatatizo la Mawasiliano Katika Mahusiano Uliyonayo:

Usikivu makini (active listening) unaweza kukusaidia kuwasiliana vema na rafiki yako au mpenzi wako. Katika usikivu makini tunamaanisha sio tu kusikia, bali kuelewa kwa uhakika kile mwenzako anachojaribu kukisema.  Hapa ndipo tofauti kati ya neno “hearing” na neno “listening” inapojidhihirisha na hata maneno kusikia na kusikiliza yanapoonyesha tofauti.  Katika mahusiano baina ya watu, marafiki, wapenzi, ni lazima kuwepo na kusikilizana “listening” na sio “kusikiana”

 Mahusiano mengi na hata ndoa nyingi zimekuwa na migogoro na hata mivunjiko maana kumekuwa na kusikiana zaidi ya kusikilizana kamwe msisahau kuwa tunayasikia magari, tunasikia ndege wa angani na ndege za abiria, tunasikia upepo na miti na makelele mengine lakini tunawa sikiliza watu  na yale wanayoyasema.

Tunasikiliza kile tunachoelezwa kwa kukitathmini kama vile kilivyosemwa na tunakirudia kwa maneno yetu wenyewe tukijaribu kifikiri kile mwenzetu anachojaribu kutuambia.  Katika hili tunatambua yakwamba kusikiliza ni mchakato (process) wakati sio hivyo katika kusikia. Baadhi ya wachunguzi wamegundua kwamba usikivu makini au masikilizano, yanawasaidia zaidi wale walioko katika mahusiano mazuri, lakini maranyingi mchakato mzima wa kusikilizana hukwama hasa pale wapenzi wanapokuwa katika ugomvi au mahojiano makali, hapa kusikilizana huwa ni ndoto.

Zingatia haya!

Walioko katika mahusiano (wanandoa) wajaribu  kupeleka jitihada zao zote katika mambo matatu muhimu

 1. wanawake wajitahidi kuwasilisha hoja na madai yao katika hali ya upole na upendo. Tafiti zinaonyesha kuwa wanaume wengi wamekuwa tayari kusikiliza toka kwa wanawake pale ambapo wanaongeleshwa kwa utulivu na unyenyekevu.
 2. Wanaume wanahitaji kuwasikiliza wenza wao kiufasaha na kuzingatia juu ya hisia na mawazo yao.
 • Pande zote mbili yaani wanaume na wanawake jitahidini kwa kila hali kuutuliza utu wa kiume na kuutiisha. Kiasili wanaume wanatabia ya kuhemka nakuwaka hisia zao za hasira haraka hasa wanapogadhibishwa, na kwa hali hii hujitahidi kujitoa kwenye tatizo haraka ili waziponye nafsi zao hatakama ufumbuzi wa tatizo haujapatikana na hii hufanya matatizo mengi katika mahusiano kuachwa bila suluhisho “unsolved Conflicts” na hali hii pia huwaacha wanawake katika hasira na maumivu makali.

Jitahidini kuhakikisha hamfikii katika hali hii kwa kurushiana utani kidogo au mwanamke kumkumbatia mwanaume angalau kupunguza gadhabu yake na mara mtajikuta mnaishia pazuri.

Na. Dr. Chris Mauki

Social, Relationship & Counseling Psychologist

Email: chrismauki57@gmail.com

www.chrismuki.co.tzDr. Chris Mauki. An expert in Relationships, Social and Counseling Psychology. Lecturer in Psychology: UDSM. Inspirational & Motivational speaker. Family man


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *