DARASA LA ALHAMISI NA DR. CHRIS MAUKI: IFAHAMU MISONGO YA MAWAZO INAYOTATIZA FAMILIA NYINGI (FAMILY STRESS)

 

 

IFAHAMU MISONGO YA MAWAZO INAYOTATIZA FAMILIA NYINGI (FAMILY STRESS)

Katika familia kuna stress ambazo zinasababishwa na wanafamilia wenyewe na nyingine zinasababishwa na walio nje ya familia(internal and external stressors).  Visababishi vyote hivi huwaathiri wanafamilia kwanamna moja au nyingine.

Visababishi vilivyo ndani ya familia hujulikana kama “family stressors” wakati vile vinavyotoka nje ya familia huitwa “extrafamily stressors”. Matokeo ya visababishi hivi yaweza kuwa magonjwa mbalimbali kwawanafamilia.

Ukosefu wa muda waonekana kuwa tatizo kwawanafamilia wengi, wengi huwahisana kutokanyumbani mapema asubuhi na kuchelewa sana  kurudi usiku, hakuna siku shuhuli zime pungua au kuisha. Hamna aliyetayari kumpa mwingine muda wake, si mke wala si mume,kila mmoja yuko bize, kila mmoja anajitahidi kukamilisha vingi alivyonavyo katika muda kidogo alionao.

Hali hii imeondoa amani katika familia nyingisana, nyingine hazikuweza kustahimili na kwahiyi kuvunjika.

 

Jinsi gani twaweza kukabiliana na hili.

Jaribu kuomba marafiki wa familia nyingine kuwasaidia katika yale wanayoweza kuwasaidia, kwamfano; jirani au marafiki wanaweza kuwasaidia kufanya manunuzi, kuwachukua watoto toka shule, kwenye mazoezi ya mpira au kuwapeleka sehemu fulani. Ikishindikana basi mwaweza kuajiri mtuambaye ataweza kuwasaidia katika shuhuli zile msizoweza kuzifanya na zisizo muhimu sana ninyi kuzifanya ili kuwaachia nafasi ya kufanya vile vilivyo muhimu. Huyu anayeajiriwa anaweza kuwasaidia shuhuli kama kufua, kuosha vyombo, kutunza bustani nk. Kipaumbele chako cha kwanza, uwe mke au mume nilazima kiwe kiwe familia yako.

Ili kuhakikisha una muda mzuri na familia yako basi waweza kupanga kupata likizo za mwezi au za mwisho wa wiki, likizo zitakazo kuweka mbali na marafiki, wafanyakazi wenzako, majukumu ya kazini, ili uweze kuweka macho, akili, na masikio yako kwa familia yako.

Wenzetu wa nchi za magharibi hupanga kwenda katika likizo za kwenda katika uvuvi, uwindaji, au kucheza katika theluji. Najua mazingira yetu ni tofauti kidogo lakini wenye mashamba au mifugo nje ya mji waweza kwenda huko. Likizo za mahotelini na katika makambi (camps) ambako watoto hupiga kambi na wazazi kushiriki michezo kamavile gofu sio muafaka sana kwa familia zinazotaka kuwa na muda mzuri kwa mambo muhimu.

Ndoa ni kazi ngumu, kutunza na kuendeleza mahusiano bora katika ndoa au katika familia ndiyo kazi yenyewe. Katika utafiti uliofanywa na David Farell umeonyesha kuwa katika wanandoa waliofanikiwa katika mahusiano yao, wengi wamekuwa wakishiriki tabia  tano kuu muhimu zifuatazo.

 1. Ukweli na uhalisi kwa mwenza wako (mke/mme)
 2. Heshima na utii kwa mwenza wako
 3. Mwenza alihesabiwa kama rafiki mkubwa, sio tu kama  mke au mme
 4.  Utayari wa kusamehe na kusamehewa
 5. Hamu ya kumfurahisha na kumsaidia mwenza.

 

Nimatumaini yangu kuwa wote tunahitaji kutumia jitihada zetu ili tuyafanye haya katika familia zetu.

Katika visababishi vingi vilivyotajwa humu vyaweza kuboreshwa kwa kuboresha mawasiliano baina ya wanafamilia. Tenga na tafuta muda maalimu wa kuongea na kuwasiliana bayana na wanafamilia wote, sio tu kuwa bize na kutumia muda wote kwa mamboyako mwenyewe,huu ni ubinafsi mkubwa “selfishness”. Jueni kutenganisha muda wa waajiri wenu na muda wa familia zenu, nyumbani ni nyumbani mahali kwa ajili ya familia na ofisini ni ofisini mahali kwa ajili ya mabo ya kazini “two different places”.

Familia nyingine zina siku maalum katika wiki ambayo kila mmoja helezea jinsi au pale alipoudhiwa na nini kifanyike. Weka muda wa kujua nini wanao wanafanya shuleni, nani anawasumbua na kuwaumiza( miili yao au hisia zao) kwanini na wanafikiri nini. Pata muda wa kupokea mawazo yao aktika kuijenga familia yao, wewe sio bosi wa familia, watoto nao wananafasi tene bora zaidi, fahamu ninani au nini kilicho ndani ya familia ambacho huwafurahisha, huwahuzunisha, nk.

 

Baadhi ya vitu vinavyosababisha msongo wa mawazo katika familia (family stressors)

 • Kuzidiwa na majukumu
 • Mmoja kutoyaelewa majukumu yake
 • Mgongano katika kuyatimiza majukumu ya kifamilia(role conflict)
 • Mapungufu katika kuyatekeleza majukumu ya mmoja
 • Ukosefu wa kupeana zawadi au vichochezi au vihamasishi pale mmoja  anapofanya vema, (suprises and motivators)
 • Mahusiano mabovu
 • Ukosefu wa fedha
 • Kutotoshelezeshwa katika tendo la ndoa

Tabia binafsi ambazo zaweza kuchangia katika kuleta msongo wa mawazo

 • Mmoja kujisikia au kujithamini zaidi ya mwezake
 • Kiwango cha juu cha hasira
 • Mmoja kuchukulia kazi yake kuwa ya muhimu zaidi ya ile ya mwenzake
 • Mapungufu katika mbinu za mahusiano, Mfano; mmoja hana tabia yakusema asante, au kutoa zawadi au hata kusema neno “nakupenda”
 • Udhaifu katika afya ya mmoja

 

Dalili za kukuonyesha kuwa misongo ya mawazo ipo ndani ya familia

 • Mahusiano nje ya ndoa
 • Muda mwingi kazini hata kama hakuna kinachofanywa huko
 • Malumbano kuzidi
 • Mmoja kutokuwa tayari kumhudumia  mwenzake katika tendo la ndoa    “sexual withdrawal”
 • Kuanza au kuzidi kwa matumizi ya vilevi
 • Hali ya mmoja kupooza na kukosa raha wakati mwingi
 • Uadui baina ya wanandoa

 

Matokeo ya kuzidi kwa dalili hizi

 • Talaka au kutengana
 • Mmoja kunyanyasika au wote kunyanyasana
 • Unyanyasaji wa watoto( child abuse) nk.

 

Visababishi toka nje ya familia(extrafamily stressors)

 • Kazi
 • Mahangaiko ya maisha
 • Familia kubwa(extended family)
 • Kukosa kazi
 • Mshahara mdogo kazini
 • Matatizo ya shule(hasa kwa wale wanaosoma wakiwa ndani ya ndoa)
 • Kukosa elimu(kwa wale ambao hawakubahatika kusoma)

 

Matokeo ya misongo hii kiafya baina ya wanandoa

 • Kuongazeka kwa matatizo ya shinikizo la damu
 • Kuongezeka kwa matatizo ya misuli(muscle tention)
 • Kuongezeka kwa mapigo ya moyo
 • Kuongezeka kwa kasi ya mfumo mzima wa upumuaji(breathing system)

 

Hali hii inapozidi kwa wanandoa tunategemea yafuatayo

 • Magonjwa ya moyo
 • Shinikizo la damu
 • Vidonda vya tumbo( ulcers)
 • Maumivu makali na ya mara kwa mara ya kichwa
 • Maumivu ya mara kwa mara ya mgongo
 • Hypertension
 • Saratani (cancer)
 • Hofu kubwa katika baadhi ya vitu( allergic reaction)

 

Msongo wa mawazo juu ya masuala ya uzazi wa mpango

Pangeni ninyi wawili kukutana na kuzungumza na mshauri, hili sio jambo la mmoja wenu bali wote. Fanyeni chaguzi fasaha ni njia ipi ya uzazi wa mpango mtaiweza na mtaipenda. Tafuteni taarifa Muhimu za kuhusu uzazi wa mpango toka kwa wataalamu, marafiki, ndugu, vitabu, na vijarida husika, msitegemee taaria za uzushi zisizoweza kuaminika.

 

Yamkini njia nyingine zitakinzana na imani au misimamo yako binafsi, basi pata ushauri toka kwa kiongozi wako wa dini. Katika kuyatimiza haya yote shirikianeni kwa upendo katika kuelekezana na kukumbushana  juu ya ushauri mlioupata.

 

Msongo wa mawazo unaosababishwa na mzazi mmoja kuwa mbali na familia

Panga kuitembelea familia yako kila upatapo nafasi zaidi ya kwenda maeneo mengine. Wasiliana nao kwa simu  mara kwa mara, hii inaruhusu  muda wa maongezi na kujuliana hali. Njia nyingine isiyo ya gharama sana ni kutumiana barua, hapa ninatia msisitizo katika barua na sio kadi. Kadi kama za siku za kuzaliwa na nyingine hazina uzito mkubwa wa mawasiliano kama ule uliopo katika barua. Lazima familia yako ijue kuwa unatumia jitihada zako zote katika kuwasiliana nao hii itawajengea haja moyoni ya kutaka kukujibu.

 

Misongo ya mawazo inayoletwa na masuala ya fedha

Stress zinazosababishwa na masuala ya fedha ni mbaya sana, zaweza kuvunja mahusiano baina ya wanafamilia, zaweza kuleta matatizo kiafya hasa pale matibabu yanapocheleweshwa mpaka mgonjwa azidiwe sana kwasababu ya ukosefu wa fedha. Hali hii huwafanya wanafamilia kuwa na hisia mbaya, kutojithamini, na  kutojipenda, hali ya kujitawala kwao hushuka maana hamna mwenye uhakika na maisha.

 

Jinsi ya kukabiliana na misongo hii.

Jifunzeni kuwa na bajeti ya mapato na matumizi ya familia, bajeti hii itawasaidia kupunguza madeni, ambayo kama yasipolipwa huleta stress zaidi na maranyingine kushitakiwa kisheria. Bajeti pia itawasaidia ninyi kutawala fedha zenu zaidi ya fedha  zenu kuwatawala ninyi.

 

Namna nzuri ya kuandaa bajeti ni kupiga picha nyuma, nijinsi gani mlitumia fedha mwakajana, au mwezi uliopita. Angalia vyanzo vyenu vya mapato, vile vikubwa na vile vidogovidogo. Wakati wote jitahidi sana matumizi yasije yakawa ya kasi kubwa kuliko kasi ya kuingiza. Fahamu ni vitu vipi hutumia fedha zenu zaidi, matumizi haya yawe ya lazima na yakishatimizwa yote ndio mwaweza kufikiria matumizi mengine ya anasa.

 

Na. Dr. Chris Mauki

Social, Relationship & Counseling Psychologist

Email: chrismauki57@gmail.com

www.chrismuki.co.tz

 

 Dr. Chris Mauki. An expert in Relationships, Social and Counseling Psychology. Lecturer in Psychology: UDSM. Inspirational & Motivational speaker. Family man


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *