DARASA LA ALHAMISI NA DR. CHRIS MAUKI: ZIFAHAMU MBINU BORA KATIKA MALEZI

ZIFAHAMU MBINU BORA KATIKA MALEZI

Utangulizi

Malezi yawezekana kutolewa kwa watoto wetu au ndugu zetu au hata watoto wa wenzetu. Hakuna mzazi au mlezi mwenyekusudi au atakayefurahia kuona mtoto wake anaharibika kimalezi, kila mmoja anahamu ya kuona yale anayoyatamani kwa mtoto au watoto wake yanatimia, ikiwemo malezi mazuri, heshima, elimu bora, kazi bora na hata kupata familia bora. Kila mzazi au mlezi anakiu na ndoto ya kuona anamuandaa mtoto wake kuwa baba bora au mama bora katika familia yake ya kesho.  Jambo lolote linalotokea na kuonekana kutaka kuharibu ndoto au maono haya ya mzazi huumiza sana moyo wa mzazi na hata kumkatisha tamaa.  Hii imepelekea mahusiano ya baadhi ya watoto na wazazi wao kufa au kulegalega, watoto wengine wametengwa au kufukuzwa majumbani mwao nk.

 

Kati ya vitu vinavyoharibu mahusiano ya wazazi na watoto wao, na kuwakatisha tamaa kabisa wazazi ni baadhi ya tabia kama vile, utovu wa nidhamu, kujiingiza katika mapenzi, kupata mimba au kumpa msichana mimba, ulevi, uvutaji wa sigara, bangi au madawa ya kulevya, magomvi, utoro wa shule, uvivu na mengine mengi.  Jinsi miaka inavozidi kwenda na jamii inavyozidi kubadilika ndivyo kazi ya malezi inavyoonekana kuwa ngumu zaidi, kila mzazi analalamika kuwa watoto wakuwa mzigo mkubwa unaoshindikana kubeba mara nyingine.

 

Kwa uzoefu kama mshauri wa kisaikolojia nina kesi tele za watoto walioshindikana na wale wenye tabia zinazosumbua wazazi au walezi wao, hii inaonyesha kuwa tatizo hili ni dhahiri.  Tofauti kubwa na miaka ya nyuma wakati wazazi wetu wanakua na kusoma maisha yalikuwa tofauti. Sasa hivi dunia inabadilika kwa kasi kila siku, vyanzo vya taarifa vinaongezeka, vikitoa taarifa nzuri na mbaya, wakati huhuo wazazi hawataki kubadilika, wakiwa na mawazo ya zamani na kulinganisha enzi zao na enzi hizi, wengi wakionekana kushangaa tafauti wazionazo baina ya vizazi hivi viwili.

 

Wazazi wengi bado wanaona aibu kuwa wazi  kutoa baadhi ya taarifa na msimamo yao kwa watoto wao wakidhani kuwa muda bado, na ni aibu kufanya hivyo mapema, kumbe jinsi wanavyochelewa ndivyo jinsi ulimwengu unawapa taarifa  potofu juu ya vitu kama mahusiano, mapenzi, ngono, ukimwi na magonjwa ya zinaa nk.  Mambo haya mengi na tofauti hizi nyingi zinachangiwa na jinsi watoto hawa wanayolelewa na mbinu za malezi ambazo wazazi wamekuwa wakizitumia.  Maranyingi nimekuwa nikisema kuwa suala sio mzazi au wazazi kulazimisha watoto kuwa na nidhamu, suala ni njia au mbinu gani za kujenga nidhamu zinatumika.  Wengi wamewaharibu watoto wao wenyewe pasipo kujua na wakati huo wao wakidhani wanawajenga na kuwaadabisha.

 

Mtiririko huu wa aina za malezi utakusadia kujitambua na ikiwezekana kubadilika, kama wewe ni mlezi sasa itakusaidia kubadilisha mtazamo wako kuhusu malezi na kama sio mlezi basi itakuandaa vema kwa mlezi bora baadae.  Nia ya mbinu hizi za malezi ni kurekebisha au kujenga tabia za watoto na kuwaelekeza katika muelekeo fulani.  Tatizo ni kwamba yako makosa mengi katika malezi yanayofanywa na wazazi na badala yake kuleta uharibifu kwa tabia za watoto wao.

 

Aina za malezi

 1. Wazazi wanaolea kiamri (Authoritarians)

Hawa ni wazazi wanao lazimisha kwa watoto wao utii, nidhamu na kufuata sheria bila kujali sheria hizo au masharti hayo yako sawa au la.  Wazazi wajinsi hii hutoa masharti makali katika kila kitu, mjadala au maswali juu ya kilichosemwa huruhusiwa kidogo sana au maranyingine hukatazwa kabisa. Mtoto au yule anayeadabishwa hukosolewa sana katika kila kitu.  Maelekezo ya jinsi ya kuwa na nidhamu hutolewa, kwa mfano, jinsi ya kukaa mezani wakati wa kula, jinsi ya kujiheshimu mgeni au wageni wakiwepo, namna ya kusalimu wakubwa nk. Baadhi ya sheria hizi husisitizwa kwa adhabu, watoto wanafahamu kabisa, kama asipofanya usafi, basi ajiandae kutokula chakula au kuchapwa fimbo.

 1. Wazazi wenyekuruhusu ukaribu (Permissive)

Hawa ni azazi wenye urahisi katika kuingilika, au kukaribiwa na watoto, wazazi hawa huwa na sheria chache sana, mara chache pia huadhibu watoto, hasa pale inapowalazimu. Anayeadhibiwa hupewa heshima yake na kusikilizwa pia.

 1. Wazazi wenye malezi ya kiutawala (Authoritative)

Hawa ni wazazi wenye amri na maarifa katika kusimamia amri zao, mzazi wa aina hii huamini katika kusimama kama mtawala kwa wale anaowaongoza, kwa mfano watoto wake. Hutoa maelezo mazuri na ya kutosha juu ya amri na masharti yaliyoweka na mjadala au maswali huruhusiwa.  Mtoto anaruhusa na uhuru wa kuelezea mawazo yake au mtazamo wake katika jambo fulani na hivyo kuweza kushawishi kubadili baadhi ya utekelezaji wa amri au masharti fulani kwa kutumia nguvu ya hoja.

Watoto hupewa nafasi ya kujiona washiriki katika utekelezaji wa masharti au amri zilizowekwa, katika hili watoto huweza kuziangalia amri za nyumbani kama “amri zetu” na sio “amri za baba au amri za mama”.  Wanaona pia manufaa au umuhimu wa kuzifuata amri hizo.  Adhabu za kuumiza mwili kama vile kuchapwa au kufinywa hutumika kidogo sana, adhabu hizi na adhabu nyingine pia hutumika kwa upendo na sio chuki.  Anayeadhibiwa hapa huona dhahiri kuwa anastahili kupokea adhabu na sio kuwa hapendwi au aheshimiki.

Makosa ambayo Wazazi au walezi hufanya katika kutoa adhabu (Disciplining Mistakes)

 1. Kudekeza (Lax Parenting). Hii inatokea pale mazi au wazazi wanaposhindwa kusimamia adhabu waliyoiweka, maranyinine wanasema kwa mdomo tu pasipo matendo, na taratibu mtoto anawasoma wazazi wake kuwa ni mbwa wasio meno (toothless dogs). Mtoto hapa huweza kujitetea, kulalama na kupindisha pindisha sheria au amri zilizowekwa ili tu kukwepa adhabu, na maranyingi hufanikiwa. Mzazi/mlezi unatakiwa kuwa imara na mwenye msimamo kusimamia ulichokisema katika kuadhibu.  Mama na baba wote wawe na msimamo mmoja, sio mmoja anakuwa tayari kuadhibu na mwingine anatetea mtoto kutoadhibiwa.  Au mama anasema tu kuhusu kuadhibu na kuja kushitaki kwa baba, kama vile yeye sio mzazi bali msaidizi wa kazi. Kama umedhamiria kutoa adhabu, basi adhabu hiyo itolewe, labda tu kuwe na msamaha ambao pia unaeleweka na utamsaidia anayesamehewa siyo ajione kuwa kasamehewa kwa sababu hakustahili adhabu.

 

 1. Kosa la pili ni lile linalofanywa na baadhi ya wazazi kwa kusifia au kuchochea tabia isiyofaa bila wao kujua. Kwa mfano; mtoto anapofanya kituko, badala ya kumkaripia utakuta anatazamwa na watu wataitana kuja kumuona anachofanya. Hii humfanya kujisikia jasiri kwa kushika hisia za wengi, uwezekano upo mkubwa kuwa tabia hiyo itandelea. Mfano mwingine katika hilo ni pale mtoto anapoelezea kupigwa na mwenzake na mzazi/mlezi anamwambia “na wewe mpige”, “kunja ngumi” “mtukane na wewe” huku ni kumharibu kabisa mtoto. Mzazi/mlezi adhibu kila tabia mbovu na chochea au hamasisha kila tabia iliyonjema indelee.

 

 1. Ukali wa maneno matupu (Verbosity). Hili ni kosa la mzazi hasa pale wanapopayuka au kuropoka au kuongea sana wakati anapotaka kutoa adhabu. Mfano, mtu anasema “mimi nimeshasema, hapa hapatoshi leo, lazima nimwonyeshe adabu”.  Huu siyo wakati wa kutunga mashairi ya adhabu ila ni wakati wa kuadhibu.  Tumia maneno machache, pasipo mihemko mingi wakati unaadhibu, elezea kwa kifupi juu ya adhabu unayotaka kuitoa, na msimamo wako na kumhimiza kutenda au kufanya kile kinachombidi.

 

 1. Kuzidiwa na hisia za hasira (Over reactivity). Mzazi au mlezi, wakati wa kuadhibu aidha kwa kitendo au kwa maneno usizidiwe na hasira au na hisia kali, jitahidi kutuliza hasira zako, maneno yako na sauti yako kwa mtoto au yule anayeadhibiwa yawe ya kawaida na yenye ujumbe wa kueleweka na sio vitisho vitupu.  Kumaanisha kwa mzazi hakupimwi na jinsi  unayvo mpayukia au kumropokea anayeadabishwa, pia hakupimwi na jinsi unavyomshika na kumtingishatingisha au kumsukuma na kumuahidi vitisho bali kwa  maneno ya chini, utulivu na sauti inayothibitisha msimamo wako.

 

Adhabu

Adhabu ni tendo au neno lolote linalotumika au kutolewa kufuatia tabia isiyofaa kwa kusudi la kuipunguza au kukomesha tabia hiyo.  Adhabu zimegawanyika katika makundi mawili,

 1. Kundi la kwanza ni adhabu zinazoambatana na kupewa (anayeadhibiwa analizimika kufanya kitu fulani, kazi fulani, au anapokea maumivu kwa kuchapwa, kufinywa nk.)
 2. Kundi la pili ni zile adhabu zinazoambatana na kunyimwa (refraining) mfano: – anayeadhibiwa ananyimwa kufanya kitu au vitu fulani anavyovipenda au vilivyozoeleka katika maisha yake ya kila siku kama vile kunyimwa kwenda kutembea, kunyimwa kuangalia Luninga, kuchelewa kulala, kunyimwa mlo nk.

 

Wazazi wengi wamekuwa wakitumia zaidi aina ya kwanza ya adhabu tena msisitizo umekuwa katika adhabu zinazoumiza mwili (physical punishment) kama vile fimbo, vibao, kufinywa nk.  Ukweli ni kwamba, aina au kundi hili la adhabu limeonekana kutokuwa na ufanisi mkubwa katika kubadili tabia za watoto, na wengine wamezizoea na kuwa sugu.  Kundi la pili la adhabu limeonekana kufanyakakazi kwa ufanisi sana. Mfano, mtoto aliyenyimwa kuangalia kipindi cha luninga jana atafanya kazi yake haraka zaidi ili asikose kipindi hicho leo.

 

Kwa namna yoyote ile adhabu yoyote inatakiwa kuangaliwa kama chombo au njia ya kinidhamu au ya kimaadili inayotumika kubadili tabia fulani kuwa bora zaidi.  Adhabu nyingine zimetumiwa na wazazi au walezi kwa muda mrefu pasipokuzitathmini kama zinafanyakazi ya kubadili tabia ya anayeadhiwa kuwa nzuri au la! Na nyingine badala yake zimekuwa zikiwaharibu watoto zaidi na kuwafanya kukomaa katika tabia mbaya walizozizoea.

 

Mwongozo katika kuadhibu

 • Usilazimishe wala kutumia zaidi adhabu zinazoumiza mwili (physical punishment) badala yake jaribu kutumia zile za kunyima au kuwatenga na wanachokipenda (refraining)
 • Wakati wote wa kuadhibu chochea tabia njema iendelezwe, mfano ahidi chochote chema kwa kila kizuri kitakachofanyika.
 • Anayeadhibiwa aelezwe bayana ni tabia gani inayoadhibiwa, mzazi usiadhibu kwa wakati mmoja mkusanyiko wa makosa mengi, adhibu tabia au kosa fulani kwa wakati sahihi.
 • Kamwe usichanganye adhabu na zawadi au kichocheo (punishment and reward) mfano, mzazi anapomchapa mtoto na hapahapo akilia anamwita na kumbembeleza, katika hali hii mtoto huyu hajasaidiwa chochote badala yake anaharibiwa na kuchanganywa zaidi na wala hatojifunza chochote.
 • Kuwa na msimamo pale unapodhamiria kuadhibu, sio kila wakati unaruhusu kushawishiwa kutoadhibu na yule unayetaka kumuadhibu na mara kwa mara unajikuta unasitisha adhabu.

 

Kama mzazi au Mlezi jiulize yafuatayo:-

 1. Je nimeweza kuwasaidia watoto wangu kwa kiasi gani katika kuyafahamu mambo yahusuyo ndoa na familia.
 • Maisha yako wewe baba na mama au hata kama ni mzazi uliye peke yako yanawapa picha gani ya ndoa au familia hao watoto unaowalea?
 • Kufahamu kwao hakutokani tu na yale tunayowaambia bali pia katika vile wanavyotuona tukiishi kila siku (Social learning)
 • Hebu fikiri kama mnapigana kila siku, mnatukanana kila siku, mnagombana na kuachana au kutengana, unalewa na kurudi usiku, unahawara na yamkini watoto wanamjua, fikiri ni picha gani unayowapatia.

 

 1. Je umewasaidia kwa kiasi gani watoto wako kufahamu mambo yanayohusiana na tendo la ndoa na mahusiano?

Je umeamua kufanya siri hatasiku moja hawajasikia mama au baba akisema kitu kuhusu tendo la ndoa, madhara yake, faida zake, wapi lifanywe, imani inasemaje kuhusu jambo hilo nk.  Wazazi wengine wakitaka kusema mambo haya kwa watoto wao huwaomba mashangazi wawasaidie, kumbuka kuwa hata huyo shangazi naye anawatoto wake wa kuwaambia.  Kunatofauti kubwa mtoto anaposikia kitu kutoka kwa mzazi (baba au mama) kulinganisha na anapokisikia kitu kile kile kutoka kwa mtu mwingine.

 

Unawapatia picha gani katika kuyatazama mahusiano ya msichana na mvulana.  Je wanaposikia hisia na mihemko ya kimwili katika mahusiano yao wanauhuru wa kuzungumza na baba au mama?  Wazazi wengi huchanganyikiwa na kuanza kutupiana lawama pale mtoto wao wa kike anapopata mimba au mtoto wa kiume anapompa msichana mimba, ukweli ni kwamba mara nyingi udhaifu umekuwa ni wa wazazi au walezi.

 

 1. Je unawasaidia kwa kiasi gani watoto wako kufahamu umuhimu wa kazi na kujali majukumu katika maisha. Labda mnamali nyingi na watoto wenu hawaamini kuwa kuna haja ya kufanya kazi au kujibidisha ili kuishi.  Labda wamedekezwa katika hali ambayo wanaamini kuwa yuko ambaye kila wakati atawajibika kwa ajili yao.

 

Tunaona jinsi ambavyo watoto wengine wanakua watu wazima na kuoa au kuolewa bila kujua kupika, kufanya usafi, kusaidia kitu fulani n.k. Labda maisha yao mengi yalitawaliwa na kufanyiwa kazi na msichana wa kazi (housegirl) au kijana wa kazi (houseboy).  Mara wazazi au walezi wanapoondoka katika maisha ya watoto hawa kwa kufariki, kutengana, au watoto wanapoanza familia zao wenyewe, hali huonekana kubadilika kabisa na wengi wetu tumekuwa mashahidi tukiona maisha yakiwaelemea watu wa jinsi hii.

 

Mzazi au mlezi muandae mtoto wako wa kike au wa kiume kukabiliana na ulimwengu wa uwajibikaji unaobadilika kila siku.  Tofauti na hilo tunatengeneza vijana ambao hata baada ya kuoa hawawezi kujitegemea bali wanataka kukaa nyumba moja na wazazi wao, na wazazi nao hawaoni kuwa hilo ni tatizo.

 

 1. Je unawasaidia vipi watoto wako kufahamu mambo yanayohusiana na Imani. Maranyingine utakuta baba na mama wana imani au dini fulani, lakini hakuna anayehangaika kujua kama watoto wao wanajali imani au dini hiyo au la. Siku ya ibada kama ni jumapili, ijumaa au jumamosi, hamna mzazi au mlezi anayeuliza kama watoto au vijana pia walienda kuabudu.

 

Mzazi au mlezi anawajibu wa kuwasaidia watoto kuamini au kufuata kile mzazi au mlezi anachokiamini labda tu mzazi au mlezi huyo hana uhakika na kile anachokiamini, si lazima kutumia nguvu na kulazimisha mtoto afuate imani yako lakini yamkini kwa kuelezea faida na mtazamo wako katika kile unachokiamini itasaidia kuliko kukaa kimya na kutokuonyesha kujali.  Kwanini uone aibu kama mzazi au mlezi kuelezea msimamo wa kile unachokiamini kwa mtoto au watoto?  Kweli zikofaida nyingi sana za watoto kuamini kile wazazi wanachokiamini (ikiwa ni chema) kuliko kutokuwahimiza kabisa, wazazi walioliweza hili watakubaliana na mimi hapa.

 

Ni kweli kabisa kuwa wazazi wengi leo wanalia au kulalamika kwajinsi watoto wao wa kike au wa kiume walivyoharibika, lakini yamkini madhara yasingekuwa makubwa kiasi hicho au yasingekuwepo kabisa kama watoto hao wangeelekezwa au kuhimizwa kuyafuata maadili ya imani.

 

Kumbuka!

Kile unachokipanda katika akili na ufahamu wa watoto wako leo aidha kwa kujua au kwa kutokujua ndicho utakachokivuna pale watakapokuwa watu wazima. Kwa wewe kama mzazi au mlezi kutowapatia taarifa zilizobora na zakuwajenga, Ulimwengu utakusaidia kazi hiyo kwa kuwapa taarifa ambazo zaweza kuwaharibu kabisa. Usifikiri hata siku moja kuwa kwasababu ukokimya, hujawaambia kitu kuhusu mapenzi au tendo la ndoa inamaanisha hawajui kitu.

 

Wakati wote kazi ya kung’oa vile ambavyo ulimwengu umeviotesha kwenye akili na mioyo ya watoto wetu huwa ngumu sana zaidi ya kazi ya sisi kuwapandia vilivyo vyema.  Ndio maana ni rahisi kusikia sentensi kama hizi kuhusiana na malezi ya watoto; “watoto hawa wamenishinda” “Mimi nimeshanawa mikono”, “mekubali kushindwa” nk.  Siku zote fahamu kuwa maadili na nidhamu mtoto anayoipata nyumbani anamoishi ni ya msingi na inadumu kuliko ile inayopatikana kokote kule. “Values from home are basic and permanent”.

 

JINSI GANI YA KUWA MZAZI/MLEZI BORA

Utangulizi

Wote tutakubaliana na ukweli kwamba malezi ya watoto sio kazi rahisi kama wengine wanavyoichukulia.  Malezi ya watoto ni jukumu ambalo twaweza kulibeba vyovyote tunavyotaka lakini tunapokuwa watu wazima au wazee tunafikia kujivunia jukumu hilo au kujilaumu kwa kushindwa kuwa wazazi au walezi bora.  Nia yangu katika hili ni kujaribu kuchambua vitu vitakavyo kusaidia na kukuwezesha kuja kujivunia utakapo waangalia wale uliowalea na kuwakuza jinsi wanavyofanyika mifano bora na kuleta sifa kwako au kwenu. Hakuna mzazi au mlezi anayetarajia au kungojea kuaibishwa na mtoto au watoto aliowalea mwenyewe, kila mzazi hata yule asiye na uhakika wa malezi yake anatarajia mema na kuwa na ndoto njema kuhusu watoto wake.

 

Hatua zitakazo kusaidia

Hatua ya 1

Kamwe usiwe na upendeleo kwa yoyote, fanya kila kitu kwa usawa pasipokuonyesha upendeleo wa aina yoyote.  Kumbuka kuwa kila mtoto ana vipawa au vipaji vyake vya tofauti, na uwezo wao pia hutofautiana, vyote hivi havinabudi kutambuliwa mapema utotoni na kutiwa moyo au kuhamasishwa ili kuendelea, watoto wawezeshwe kuendeleza vile wanavyoonekana kuviweza mfano kipawa cha uimbaji, akili ya ufundi, uwezo wa kimichezo nk.

 

Hatua ya 2

Epusha roho za mashindano baina ya watoto, ushindani mdogo mdogo na wa kawaida hauna shida kwa sababu unaweza kuchochea kujibidisha, tatitizo ni yale mashindano yanayoweza kuleta magomvi na uhasama, mara nyingi hili huonekana katika familia zenye watoto au mtoto wa baba peke yake au wamama peke yake na wale wa baba na mama (watoto wa ndoa) wanapoishi pamoja.  Wakati wote ondoa tofauti baina yao katika mahusiano yao ili usije kutengeneza ndugu ambao ni maadui hata watakapo kuwa watu wazima.

 

Hatua ya 3

Chochea ari ya kupenda shule na utamani wa kufaulu, kila mtoto anakiwango cha juu cha uwezo ambacho kinatakiwa kutambuliwa.  Kama mwanao anaonekana kukosa hamasa ya shule aliyoko jaribu shule nyingine, fanya utafiti kwa kuzungumza naye nini anachokipenda katika elimu kwasababu tafiti zinaonyesha kuwa maranyingi masuala ya shule na elimu ni maamuzi ya lazima toka kwa wazazi pekeyao pasipo watoto kuhusishwa au kushirikishwa. Jaribu nyanja mbalimbali za elimu na usikate tamaa mapema.  Jitahidi kuweka akiba ya fedha kwa ajili ya elimu ya watoto wako kwasababu elimu ni bora lakini ni ya gharama, na waswahili wamesema “Ikiwa unaona elimu ni ghali basi jaribu ujinga”.

 

Hatua ya 4

Penda kuwa na muda na watoto wako, hususani wakati wa chakula cha jioni na zungumza nao mambo yaliyoendelea au yanayoendelea katika maisha yao kwa siku hiyo, watoto pia wanayo ya kukushirikisha, kwa namna hii watoto watafurahi na kuongeza upendo na ukaribu kwa wazazi wao. Kwa bahati mbaya tafiti zinaonyesha kuwa wazazi wa kiume hususani wakiafrika hupata nafasi marachache zaidi kula chakula cha jioni na familia zao.  Ikiwa ratiba yako ya usiku haikuruhusu basi jaribu kushiriki kifungua kinywa (breakfast) pamoja na watu wengine wa familia yako.  Najua wako watakaojitetea kuwa ratiba zao hazikubali kabisa ila suala ni kwamba, ukiona umuhimu wa jambo hili basi utalifanya kuwezekana.

 

Hatua ya 5

Kuza baadhi ya mazoea ya kifamilia yanayowaleta karibu zaidi kama vile kufanya na sherehe za krismas au pasaka au sikukuu nyingine kwa pamoja nyumbani au kusafiri pamoja wakati huo.  Kukaribisha nyumbani kwenu marafiki wa mtoto au watoto wako siku za wikiendi au sikuu. Kuwaruhusu watoto kutoka kwa uangalizi maalumu.  Huwezi kuelewa jinsi gani mambo haya yanaumuhimu kwa mtoto wako mpaka apate tatizo fulani ndiyo utaelewa.

 

Hatua ya 6

Kuwa msaada kwa watoto wako bila kujali nini kinaendelea, hata kama unavunjwa moyo na vile watoto wako wanavyoishi au tabia fulani walizonazo, waonyeshe upendo na utayari wako wa kuwasaidia, wawezeshe kufahamu jinsi gani ya kufanya vema zaidi wakati mwingine. Kamwe usiwape kisogo wanapohitaji msaada wako.

 

Hatua ya 7

Ruhusu watoto au mtoto wako ajue na aamini kuwa uko na utakuwepo kwa ajili yake wakati wote, wala asiwe na mashaka kabisa na hili. Najua kila familia hupitia magumu na changamoto mbalimbali katika maisha, pamoja na haya yote mruhusu ajue unampenda na utampenda daima. Hakuna kitu kibaya na kisichotoka kwa urahisi moyoni mwa mtoto kama pale mtoto anapokuwa na mashaka na malezi au ulinzi anaoupata toka kwa mzazi wake.

 

ILI KULEA AU KUKUZA WATOTO WENYE AFYA KATIKA MAISHA;

Yafuatayo hayana budi kufanyika

Ninaposema afya katika mtazamo huu simaanishi tu afya ya mwili kama ambavyo wengi watafikiri. Ninaposema “mtoto mwenye afya” “a healthy child” inajumuisha ujumla wa maisha ya mtoto, yani afya ya kiakili, afya kimwili, afya kiroho, afya katika mahusiano yake ya kijamii, afya ya kihisia (emotional health), afya katika mitazamo yake n.k. Mtoto aliye na afya bora kimwili, kwasababu tu ya chakula kizuri lakini hana tabia njema na wala hahusiano mema na wenzake, mtoto huyu ana upungufu mkubwa, bado ukamilifu wa afya yake kimaisha hauko vizuri.  Ni lazima wazazi wafikirie hatua ya kutoweka akili zao zote kwenye afya ya mwili wa mtoto tu bali katika pia mandeleo ya mtoto katika nyanja nyingine za maisha yake (the totality of a child).

 

Ili haya yawezekane kwa faida ya mtoto na familia kwa ujumla, yafuatayo hayanabudi kuzingatiwa

 1. Kuwepo na muda maalumu wa kula, sio kila wakati mtoto anapojisikia kula kitu anakula na anashindwa kujua ni muda gani maalumu kwake kula.  Kama nilivyokwisha kusema awali, inapowezekana walau katika mlo mmoja kwa siku familia iwe pamoja mezani hii inamaana sana kwa watoto na hata familia kwa ujumla.  Katika muda huu wa kula, vitu kama televisheni au redio visipewe kipaumbele kabisa maana hupotosha kusudi la kule kuwa pamoja katika kula. Utazame muda wa kula kama wakati bora na wa kipekee kwa familia husika.

 

 1. Muwezeshe mwanao kula vyakula bora na wakati wote anapokuwa shuleni apate chakula kizuri, asishinde njaa kwa muda mrefu au kula kitukimoja kwa muda mrefu. Epuka watoto kula viporo mara kwa mara na kila mara sisitiza matunda na mboga za majani. Kunywa maji iwe ni tabia ya kawaida sio mpaka mtoto awe na kiu.  Najua wengi hujitetea kuwa hivi vyote ni gharama lakini vinaweza kufanyika kwa gharama nafuu tu, kina chohitajika sio fedha nyingi bali ni kujali na kuamua kubadilika.

 

 1. Siku zote mtoto anywe maji au kimiminika chochote nusu saa au muda zaidi kabla au baada yamlo, hii inashauriwa kibaiolojia kutokana na urahisishaji wa mchakato wa usagaji na uendeshaji wa chakula tumboni.

 

 1. Weka mipaka katika uangaliaji wa vipindi vya televisheni na filamu au michezo ya video (vieogames) au hata computer, vitu hivi vyote ni vizuri lakini vyaweza kumharibu kabisa mwanao.  Hata kama kuna kinachotazamwa na watu wazima, hakikisha  kinazingatia maadili na umri wa mtoto, ndio maana mikanda na santuri (cd) zote  zimandikwa umri wa wanaoruhusiwa kuangalia filamu ile na vitu vyote vya tahadhari. Katika familia nyingine watoto ndio wanao miliki kifaa cha kuiongozea luninga (remote control).  Usisahau kuwa watoto hunasa zaidi na kupeleka vichwani zaidi kupitia vile wanavyoviona kwa macho kuliko vile wanavyovisikia.  Tafiti kadhaa zimethibitisha kuwa filamu za mieleka, ngumi, vita na mapigano ya aina yoyote, miziki na minenguo mbalimbali huwaingia zaidi watoto na huweza kuwabadili tabia watoto hawa kwa haraka zaidi.

 

 1. Jitahidi kumpeleka mwanao katika ukaguzi wa ujumla wa afya kwa daktari walau mara moja kwa mwaka. Vifaa na mashine tunazomiliki hufanyiwa ukarabati (maintenance) lakini wengi tunasahau kufanya ukarabati wa afya zetu na hususani za watoto wetu.  Wengine husubiri hadi tuone dalili au matatizo ya ugonjwa ndio tuwapeleke watoto wetu kwa daktari.  Usisahau kuzuia ni bora kuliko kutibu.

 

 1. Jitahidi sana kumpatia mwanao kifungua kinywa kilichobora maana imethibitishwa kuwa kile kiendecho tumboni mwa mtoto asubuhi kinamchango mkubwa sana katika kutengeneza akili zake kupokea vyema vile anavyofundishwa shuleni kuliko mlo mwingine wowote.  Wazazi wengi hawafahamu hili kwahiyo huhimiza watoto wao kula zaidi mchana au usiku.  Ni bora hata mtoto akakosa chakula cha usiku kuliko kukosa mlo mzuri wa kufungua kinywa.  Ni vema kinamama kuwa na uhakika wa nini watoto wao wanakula asubuhi na ikiwezekana kukikagua kabla hawajaondoka kwenda shule au kabla wazazi hao hawajaenda makazini.  Kabla hatujaanza kukimbizana na walimu wa watoto wetu na kuhangaika na elimu ya ziada (tuition) hebu kwanza tuangalie hawa watoto wanakula nini asubuhi kila siku.  Ikiwezekana hiyo fedha ya tuition kidogo iboreshe mlo wa watoto wako asubuhi.

 

 1. Mwezeshe na msaidie mwanao kuwafahamu ndugu wanaomzunguka hususani ndugu wa upande wa baba na pia ndugu wa upande wa mama. Mabadiliko ya maisha na maendeleo ya maisha katika kijamii yameleta matatizo makubwa katika familia, ni kawaida sana leo kukuta mtoto hajui ndugu yeyote wa upande wa mama yake au mwingine amewajua wajomba tu bila kuwafahamu baba wadogo na wakubwa. Unakuta maranyingine mtoto anawajua ndugu wa upande wa mama yake kwasababu aliwahi kukaa kwa bibi mkoa fulani na hajawahi hata sikumoja kwenda mkoa atokako baba yake na kwahiyo hajui ndugu wa huko hata mmoja.  Mara nyingi  kwa sisi tunaojihusisha na ushauri wa kisaikolojia (Counseling) tumepata tabu sana  pale tunapodadisi na kukuta baadhi ya matatizo walionayo wateja wetu ni ya mwendelezo kutoka baadhi ya ndugu katika familia (trangenerational problems), ila kibaya zaidi  unakuta mhusika hamjui yoyote wala hajui historia yoyote ya familia yake.  Wengi wamekaa mijini kwa miaka mingi hawajawahi hata kutembelea vijijini waliko ndugu za wazazi wao, na taratibu hali inaonyesha huko mbeleni watoto wataishia kumfahamu baba na mama, kaka na dada, na marafiki wa familia zao tu. Wazazi tujitahidi kuhakikisha tunaliepuka jambo hili.

 

 1. Muda wa kufanya mazoezi ni muhimu sana, mkuze mtoto au watoto wako wakijua kuwa mazoezi ya mwili sio anasa bali ni hitaji muhimu kwa afya yamwili na akili, pale inapowezekana fanya mazoezi marahisi na mtoto au watoto wako, mfano kutembea au kukimbia  jioni, wale wenye maeneo makubwa majumbani mwao wananafasi kubwa ya kulifanyia hili nyumbani. Kumbuka kuwa mtoto hujisikia raha sana anapofanya zoezi na mzazi, pia kile unachofanya nae akiwa mdogo atakiendeleza kirahisi zaidi wakati wa utuuzima.

 

 1. Kagua na kuwa mwangalifu kwa vyakula wanavyokula watoto wako, punguza sana kiwango cha sukari na mafuta katika vyakula vyao.  Tofauti na zamani, sikuhizi ni jambo la kawaida kusikia kijana mdogo amepoteza maisha kwa ugonjwa wa kisukari.  Vyakula vyote viwe kwa kiasi, tukumbuke kuwa tunakula ili tuishi isije ikajeuka na kuwa tunakula ili tufe na pia tusisahau usemi wa wazungu kuwa chochote cha kuzidi chaweza kuwa na madhara “too much is harmful”.

 

 1. Mwezeshe mwanao kufahamu ni yupi rafiki mzuri na ni yupi siye, uzuri au ubaya wa rafiki usiwe kutokana na kile mtoto yule anachokipendelea bali kutokana na maadili ya jamii husika.  Maranyingi watoto hujifunza sana na kwa undani zaidi kutoka kwa wenzao (peer groups), sasa ili wawe na tabia njema, au ili tabia njema waliyonayo isiharibiwe, basi wahusiane na marafiki walio wema. Mzazi, weka mipaka ya wapi unapenda mwanao afike au aende, nani azungumze nae na nani aonane nae. Sio kila mtu anastahili kuwa wakaribu au kuwa rafiki wa mtoto wako, uko msemo uliosema “ndege wanaofanana huruka pamoja” hii ni kukuonyesha uwezekano wa mwanao kujifunza au kuiga kwa urahisi tabia nzuri au mbaya za wale anaopenda kuwa nao.

 

Na. Dr. Chris Mauki

Social, Relationship & Counseling Psychologist

Email: chrismauki57@gmail.com

www.chrismuki.co.tz

 

 

 

 

 Dr. Chris Mauki. An expert in Relationships, Social and Counseling Psychology. Lecturer in Psychology: UDSM. Inspirational & Motivational speaker. Family man


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *