DARASA LA ALHAMISI NA DR. CHRIS MAUKI: MAMBO MATANO MUHIMU YATAKAYO KUSAIDIA KUYALINDA MAHUSIANO YAKO

 

MAMBO MATANO MUHIMU YATAKAYO KUSAIDIA KUYALINDA MAHUSIANO YAKO

Wakati wowote mahusiano baina ya mume na mke au wapenzi wowote ni kitu cha maana na kinachotakiwa kuheshimiwa na wote. Kila mahusiano haya yanapoanza wawili walioko kwenye mahusiano hupeana maneno ya kumaanisha kwao, na kujitoa kwao katika kuhakikisha mahusiano hayo yana dumu na kusimama. Hakuna wanaoanza mahusiano ili waje wayaone mahusiano hayo yakifa, hiyo sio furaha ya yeyote yule, kinyume chake kila mtu huumia sana anapoona mahusiano yake yanayumba au hata kufa kinyume na alivyotarajia. Swali linakuja, ninani amesababisha kuyumba au kufa huku?

Ifahamike kwamba sio watu wote wanaowaona mkiwa mnapendana wanafurahia na kuwaombea muendelee kupendana, wapo ambao wako radhi kujaribu kwa jitihada zozote kuona mnatengana au mnapitia misukosuko. Watu hawa unaweza kuwapa majina yeyote unayotaka lakini ninapenda kuwaita watafunaji au wauaji wa mapenzi ya watu. Hawa wako wengi sana kiasi ambacho hauwezi kuamini, yamkini wengine ni marafiki zako wanaokuzunguka wewe ukihisi kuwa ni ndugu wema. Watu hawa ambao yamkini wasiwe watu wabaya kwenye mambo mengine au tabia nyingine lakini wanaweza kuwa mtego mkali sana kwa wewe uliyeko kwenye mahusiano na kama hautokuwa macho utajikuta umenaswa na kuanza kumwaga sumu kwenye hayo mahusiano uliyokuwa nayo na mume au mke wako.

Kama unadhani ni muhimu kuwafahamu na kuwa makini na watafunaji au wauaji hawa wa mapenzi ya watu basi haya hapa mambo matano yatakayokuwezesha kuyalinda mahusiano yako.

  1. Fahamu kwamba watu hawa sio ma razote wanajua ubaya wa wayafanyayo

Kama ilivyo kwa wanyama wanaokula wenzao huko porini ndivyo ilivyo hata kwa watafunaji hawa kwasababu nao pia huangalia mtu ambaye hauko makini na mahusiano yake, mtu ambaye hamaanishi vyakutosha awapo na mpenzi wake, watu hawa wanaweza kuanza kukusoma na kukuchukulia kasi uwapo kazini, wanawezakuwa ni wafanyakazi wenzako, majiraji, marafiki wa kawaida, wanafunzi wenzako, au hata waumini wenzako huko unakosali, taratibu bila wewe kufahamu wanajisogeza karibu yako, kama vile kitu cha kawaida, wanakuwa wema sana na wenye msaada kwako, na hatimaye mnajikuta mmeunganisha hisia, na penzi linaweza kuanza kumea. Hawa hawaendi wala kumchagua mtu asiye na mahusiano, la hasha, wanamtafuta mtu aliyeko kwenye mahusiano, aliyeoa au kuolewa.

Watafunaji hawa wanaweza kuwa wanaume au wanawake. Wanaweza kuwa wazuri, warembo, wanaovutia au hata wasiovutia kwa mtazamo wan je. Wanaweza kuwa watu wa rangi yeyote, kabila lolote, dini yeyote na maisha ya aina yeyote. Mara nyingi wanaweza wasifahamu sawia uhalisia wa nia zao na nini kinachoweza kuwa madhara ya ukaribu huo kwa mke au mume au watoto wa huyu wanayemkaribia. Wao wanawezakuwa wanafurahia tu ile hali ya hisia nzuri na raha ya ukaribu mlionao.

  1. Aina hii ya watu kiu yao ni kuwa na mamlaka au kumtawala yule waliyemnasa ili tu wajisikie kuwa wao ni wathamani

 Furaha waliyonayo watafunaji au wauwaji hawa wa penzi ni pale wanapoona kuwa unawasikiliza, unawaheshimu, wakisema unafanya, wakikuita unaenda, taratibu bila wewe kujua watahakikisha wamekufanya uanze kuhisi hisia kwao na jambo hilo linawafanya wenye furaha sanaaaa, hususani pale wanapojua kabisa kuwa wewe unampenzi, unmake au mume lakini bado wameweza kukufanya ukawapa na fasi na wao kuzishika hisia zao, ingawa mara nyingine hali hii inaweza kuwasababisha kutamani kukuminya zaidi ili uongeze hisia kwao na ikibidi kuwasahau wengine, usisahau wakale walisema “mwamba ngozi huvutia kwake”.

Pamoja na ukweli huu, ifahamike kwamba mara nyingine watafunaji hawa wanaweza kuwa makini sana wakizuia uhusiano wenu usipanuke sana au kujulikana sana. Wakati mwingine unaweza kushangaa anakuwa karibu na wewe sana lakini hahitaji mfanye tendo la ndoa au umtambulishe kwa rafiki zako. Hii ni kwasababu wanajua kwamba kwa kujulikana zaidi na kwa kina, au kwa kuamua kuanza kushiriki tendo la ndoa au kukuruhusu ushinde au ulale kwake inaweza kufanya mahusiano hayo yakashitukiwa na mke au mume wako na hivyo kusitishwa. Hawako tayari kuona hisia zao kwako zinaingiliwa na kitu chochote kwahiyo wanaamua kuwa makini kuzilinda. Ni bora uyalinde mahusiano yako kuliko waingie wao na kuanza kulinda mbegu walizozipanda wao.

 

  1. Nia ya watafunaji hawa mara nyingi sio kuvunja ndoa yenu bali kiu yao ni kujishikiza na kufaidi kama kupe

Aina hii ya binadamu huamua kuwa kama kupe, kiu yao sio kula nyama yote au labda wamuue mnyama waliyejinasa kwake, la hasha, wao wanafurahia kule kujinasa pasipoonekana, kunyoya taratibu na kuendelea kuwa hapo muda wote. Lakini ni vema kujua kuwa wadudu hawa wanakunyonya damu ambayo ni nguvu yako, fahamu wanakunyonya nishati ya hisia ambayo ungeitumia vema kwa mkeo au mumeo lakini unajikuta inafyonzwa taratibu na wao. Hii ndio maana mara nyingine unamshangaa mumeo au mkeo anaporudi kutoka kazini au kwenye mizunguko yake anakuja mkavu, mwepesi, hana hamasa na chochote tofauti na alivyozoea kuwa, yale maneno matamu alizoea kukurushia, vile vikumbato alizoea kukuonyesha vimefyonzwa na wanyonyaji wa hisia huko alikotoka, wamemmaliza wamemwacha mtupu ndio wamemruhusu akurudie wewe. Hapo basi kitu kidogo tu kinaweza kuibua ugomvi mkubwa na ukashangaa nini kinaendelea. Hali hii sio afya kabisa kwenye mahusiano au ndoa yenu, msipoishitukia mapema na kuamua kuishuhulikia basi mnaweza kuvuna mabua.

 

  1. Hatua ya kwanza ya kuwakimbiza watafunaji hawa ni kwa wewe, mume au mke kutambua mapema wizi huu wa hisia

Kama ukihisi tu ya kwamba wewe au huyo mpenzi wako ni mhanga wa wezi hawa wa hisia, au ameshakutana watafunaji wa penzi, cha kwanza na cha muhimu kitakuwa ni kutambua mapema kuwa kunakitu kisicho sawa kinaendelea kwenye penzi lenu na hivyo hamna budi kuchukua hatua za haraka. Kama unahisi kwamba wewe au mwenzako mnatumia muda mrefu zaidi wa maongezi au chochote na mtu mwingine nje ya penzi lenu na yamkini hali hiyo inaanza kumuathiri mwenzako au ameshaanza kulalamika kuhusu hilo, fahamu kwamba hali hiyo ni dalili tosha ya kujua kuwa tayari mmoja wenu ananyonywa.

  1. Baada ya kufahamu uwezekano wa uwepo wa watafunaji hawa, chukua hatua ya kusitisha mahusiano hayo yasiyo na afya.

Unatakiwa kufanya chochote kiwezekanacho kuhakikisha mahusiano na mtafunaji huyo yanasitishwa mara moja, na kama wote mmeshikiliwa na mmeanza kutafunwa basi hakikisha unamshawishi na mwenzako nayeye kuhakikisha ameondokana na mtu huyo kabisa. Baada ya kukubali na kukiri uwezekano wa kuwepo kwa watafunaji hawa, labda hatua hii ya mwisho ndiyo inaweza kuonekana kuwa ngumu zaidi, lakini ina umuhimu sana kwa manufaa ya penzi lenu na ni pale tu mtakapoweza kuondokana na wadudu hawa au mdudu huyu ndipo ninyi wawili mtakapoweza kuendelea na mchakato wa kuboresha na kunawirisha penzi lenu ambalo labda lilikwisha kutobolewa na wadudu.

Zijaribu mbinu au hatua hizi tano ili kuyaweka mahusiano yako salama mbali na wadudu watafunaji wa penzi.

 

Na. Dr. Chris Mauki

Social, Relationship & Counseling Psychologist

Email: chrismauki57@gmail.com

www.chrismuki.co.tzDr. Chris Mauki. An expert in Relationships, Social and Counseling Psychology. Lecturer in Psychology: UDSM. Inspirational & Motivational speaker. Family man


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *