DARASA LA ALHAMISI NA DR. CHRIS MAUKI: VITU 10 AMBAVYO HUTAKIWI KUMWAMBIA MWANAMKE KATIKA MAHUSIANO

VITU 10 AMBAVYO HUTAKIWI KUMWAMBIA MWANAMKE KATIKA MAHUSIANO

  1. Sio jambo jema kabisa na linalopendelewa na mwanamke kuulizwa “naweza kukubusu?” wao hupendelea kuona busu linamwagika muda wowote, popote labda ukute mmekwaruzana. Mara unapomuuliza unamfanya mpenzi wako wa kike akushangae na kukufananisha na mvulana wa umri mdogo na sio mtu mzima. Kama huyo mpenzi wako uliyemuuliza swali hili ni mwema na mwenye busara basi atakujibu “ndiyo” ingawa sio kihamasa, na kama ni wale wasio weza kukufunikia jambo atakwambia wazi NO! tena labda na maneno mengine tele ya kukushushia hadhi.

 

  1. Jinsia ya kike imeumbwa kutegemea na kumtazama mwanaume kama kiongozi anayeweza kuanzisha na kuyaweza mazingira kirahisi. Inamshangaza sana mpenzi wako wa kike pale ambapo kila kitu, hata vile vinavyotegemewa kuwa rahisi katika kutoa mwongozo au maamuzi fulani wewe unauliza, nini kifanyike, au unahitaji kibali. Kwamfano, kama umewaza kumtoa “out” mpenzi wako, haina haja ya wewe kumuuliza “je naweza kukutoa out siku yoyote?” hapa lazima akuone hujakua kifikra. Unachotegemewa kufanya kama mwanaume uliyepevuka ni kupendekeza “ku propose” unachotaka mfanye na wapi unadhani patafaa nyie kwenda. Inawezekana sana yeye akawa na mawazo tofauti na pale ulipopendekeza na mkaamua kwa pamoja sehemu nyingine lakini tayari ulishaanzisha pendekezo wewe. Na pale unapotoa pendekezo fulani toa kwa ujasiri na kwa kujiamini na kwa upendo pia, sio kwa kujionyesha wewe ndiyo mwanaume na kwamba ukisha sema umesema. Kwa mfano unaweza kusema “Mpenzi kunasehemu nimeiona nimeipenda sana, unaonaje tukienda wote wikiendi hii?”

 

  1. Unapokuwa na mpenzi wako wa kike usiwekeze zaidi mazungumzo yako kwenye mali zako, gari lako, kazi yako, nyumba yako, shule yako n.k. Tabia hii hutoa taarifa kwa jinsia ya kike kwamba unajionyesha, unatafuta kuonekana katika mtazamo ambao sio ulionao kiuhalisi. Majigambo au hadithi za ulivyonavyo au unavyomiliki huwafanya wanawake walio na busara wakuweke kwenye kundi la wasiojua mapenzi, kwasababu unaonyesha dhahiri kuwa hauna kingine cha kuweka ladha kwenye mahusiano na maongezi yenu mbali na hizo hadithi zako za “nina hiki” nina kile”. Ukiona mwanamke anazifurahia hadithi hizi ujue huyo ametua kwako kutafuta kitu “she is a gold digger”. Ni kweli yamkini umependwa lakini anayekupenda angetamani sana usivitaje ulivyonavyo kwasababu yamkini sivyo alivovifuata kwako.

 

  1. Watu wengi husema kwamba mwanamke hupenda mwanaume mwenye mpangilio, jambo hili linaukweli na nimelihakikisha. Usiseme au kufanya jambo lolote mbele ya mpenzi wako wa kike litakaloonyesha kuwa wewe hauna mpangilio, kwamba hujawaza chochote cha kufanya na unataka kusikia kutoka kwake kama yeye ana ajenda yoyote. Kwamfano, kama umeamua kwenda na mwenzako mtoko “outing” hakikisha kichwani una ratiba nzima ya nini kitafanyika, na nini mtakiongea kama mmetoka ili mzungumze kitu. Usije kuwa kama wale ambao tunawakuta wametoana “out” kwenye mahoteli au kwenye fukwe, halafu unawaona wameketi kila mtu anaangalia anachokijua, hawana cha kuzungumza wala cha kufanya, wanaishia kuweka muda wao kwenye simu zao kuwasiliana na walioko nje ya mazingira yao. Kuna haja gani ya kusema mmetoka “out” halafu mnaishia kila mtu kuwa kisiwani kwake. Kama unatabia ya kupendekeza kwenda sehemu halafu unashindwa kufanya mtoko huo kuwa wenye hamasa, unamfanya mpenzi wako wa kike kukuona na kukuhesabu kuwa hutoweza kamwe kumpa nyakati za furaha katika mahusiano yenu, na kama ndiyo mnaanza mahusiano hapo fahamu umemkosa.

 

  1. Mara nyingi sio sentensi yenye kupendwa na jinsia ya kike kuuliza “je unanipena?” au “je unavutiwa na mimi?” Ingawa yeye akikuuliza swali hili kwake ni sawa na yamkini lisilete madhara yale yale kama ambavyo wewe ungeuliza, na pia anaweza kukuuliza hata mara 10 kwa siku. Sentensi za namna hii kwa kawaida huizima kabisa hamasa na msisimko wa mwanamke alionao kwako. Sentensi za jinsi hii huweza kutoa picha kwamba hauna ujasiri, unahofu kuwa hupendwi na yamkini unamlaumu yeye. Hatakama hauna uhakika kama unamvutia au la, au kama anakupenda au la, amini hivyo na anzia hapo kuelekea mbele.

 

  1. Haileti picha nzuri kwa mpenzi wako wa kike pale unapomuuliza “nilituma ujumbe wa simu “sms” au nilipiga simu muda fulani na hukupokea wala hukusema chochote baadae, vipi kulikuwa na shida?” Sentensi au swali hili wala halina shida kabisa ila tatizo likielekezwa kwa mpenzi wa kike laweza kuleta shida, na wanaume wengi tumejikuta tunajibiwa vibaya au hali inabadilika gafla baada ya kuuliza swali hili. Hata kama una kiu ya kujua nini kilimfanya asijibu, inakuwa vema zaidi ukiendelea na mazungumzo mengine kama vile huhupiga simu wala kutuma ujumbe kwasababu kwa mwanamke swali hili hutafsiriwa tofauti. Jambo la kwanza analoweza kutafsiri ni kwamba umekasirishwa na kule kutorudishiwa ujumbe au yeye kutotoa taarifa mapema, hii tayari inampa kujihami “defensiveness” dhidi yako, na kama ndiyo mnaanza mahusiano basi anakutafsiri kuwa wewe ni mtu unaye kasirika kwa haraka na kuweka msisitizo kwenye vitu vidogo. Pili kupitia sentensi hii unamfanya ajihisi mkosa “sense of guilty” jambo ambalo mara nyingi humfanya mwanamke ajione au ajihisi kuwa hayuko katika mikono salama “she feels insecured”, hali ambayo yaweza kupunguza hisia za penzi kwako.

 

  1. Sio swali lenye afya sana katika akili ya mpenzi wako wa kike pale unapomuuliza “eti umeshawahi kufanya mapenzi na wapenzi wangapi kabla yangu?” Nasema hivi kwasababu najua wapo wanaume wanawauliza wapenzi wao wa kike wakidhani ni swali la utani tu. Baadhi ya vijana niliowahi kuzungumza nao na waliowahi kuuliza swali hili kwa wapenzi wao, niliwauliza “je kwa kuuliza swali hili ulikuwa unataka kujua idadi? Na je ukijua kinafuata nini?” hakuna aliyewahi kuweza kunijibu. Swali hili hata kama liko sawa kwa wewe unayeuliza, linapoulizwa kwa jinsia ya kike linamfanya akose raha na kukosa uhuru na amani ndani ya moyo wake anapokuwa na wewe, anaweza pia kuuogopa uwepo wako hasa kama swali hili limeulizwa mwanzoni mwa mahusiano yenu. Yeye anaweza kukuuliza swali hili, wala usihofu kumjibu kama kweli unamajibu sahihi kwasababu halileti matokeo sawa kama wewe ukiliuliza. Kamwe usianze kuuliza wewe kwasababu matokeo yake hautoyapenda.

 

  1. Mnapokuwa katika mahusiano, hususani kama hamna muda mrefu sana na mko kwenye mchakato wa kujuana vema, sio vizuri na nihatari kwa mahusiano yenu kama utaonyesha sentensi za kupinga au kushusha hadhi zile ndoto au mipango ya siku zijazo aliyonayo mpenzi wako wa kike, au vile vitu ambavyo katika maongezi yenu ameonekana kuvithamini na kuvitamani sana. Kwamfano katika maongezi yenu unagundua mpenzi wako anakiu sana ya kuolewa, au kukutambulisha kwa ndugu zake, hata kama wewe bado huna wazo hilo usianze gafla kuropoka “Ahh! Mimi biashara ya kuoa kwa sasa ndo kabisa sina wazo ”, “kwanza kuoa matatizo tu”. Au labda umegundua mpenzi wako anatamani sana kujiendeleza kimasomo, na labda anategemea wewe kama mpenzi wake utamtia moyo katika hilo, badala yake unapayuka tu “kwanza mwanamke akishasoma tu hatulii, anajifanya yeye ndiyo kaoa kumbe kaolewa”. Kwa sentensi hizi ndugu yangu utaachwa sana.

 

  1. Wengi wetu tuna njia tofauti za namna ya kumalizia mazungumzo tunapoongea na wapenzi wetu wa kike katika simu. Nakutahadharisha tu kamwe usimalizie mazungumzo yako ya simu kwa mpenzi wako wa kike kwa kusema maneno kama “nitakupigia tena siku flani”. Hitimisho la namna hii ni zuri kwenye biashara, pale unapomuuzia mtu kitu au kumfuatilia kwa manunuzi fulani lakini kwa kusema hivi kwa mwanamke unasitisha hamu na uwezekano wayeye kukupigia au kuongea na wewe kabla ya hiyo siku uliyoisema, kwasababu umesema wewe basi inamaana yeye akae tu akisubiria kukusikia siku uliyochagua wewe. Na kama akitaka kukupigia kabla ya siku hiyo atajihisi labda anaonekana anasukuma, analazimisha au anakiu sana na wewe. Kwanini usimalizie mazungumzo yako kwa maneno kama “Nimefurahi kuongea nawewe” Nimefurahi kukusikia” n.k.

 

  1. Wanaume wengi wamekuwa wakifanya kosa la kuzungumza sentensi ngumu na za kuwashushia hadhi au kuwaumbua rafiki wa kiume wa wapenzi wao. Hapa namaanisha kwamba unampenzi au mke wako na yeye ana marafiki zake wa kiume labda anaofanya nao kazi, aliosoma nao au kujuana nao kwa namna yoyote, yamkini unawafahamu au wengine huwafahamu, sasa kila anapowataja mnapozungumza unahamaki, unaanza kukasirika na kutoa maneno ya kejeli dhidi yao. Hii inamfanya mpenzi wako wa kike kukuhisi usiye na ujasiri, na yeye kujihisi kukosa amani na utulivu moyoni mwake awapo na wewe. Anakuona pia ni kati ya wale wanaume wasiojiamini, wanaoogopa ushindani dhidi ya marafiki hao. Kwanini usinyamaze hata ukisikia anamtaja au kuwataja hao marafiki zake, maadam unajua hamna kibaya kati yaona kwamba yeye anakupenda. Kwanza kwa kule kuwataja, anaonyesha anaamini wewe ni zaidi yao, sasa mbona unajiabisha kirahisi. Usionyeshe udhaifu wa nafsi na moyo wako kirahisi kiasi hicho

Imeandaliwa na;

Dr. Chris Mauki

Social, Relationship & Counseling Psychologist

University of Dar es Salaam

www.chrismauki.co.tz

chrismauki57@gmail.com

0713 407182Dr. Chris Mauki. An expert in Relationships, Social and Counseling Psychology. Lecturer in Psychology: UDSM. Inspirational & Motivational speaker. Family man


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *