DARASA LA ALHAMISI NA DR. CHRIS MAUKI: IELEWE KANUNI YA 90/10 (THE NINETY-TEN PRINCIPLE)

IELEWE KANUNI YA 90/10

(THE NINETY-TEN PRINCIPLE)

Kanuni hii ni ya muhimu sana na itakusaidia katika huyabadili maisha yako, kubadili namna  unavyoyapokea au kuyaangalia mambo na kuonyesha hisia zako.

Kanuni hii inamsingi ufuatao; Asilimia 10 ya maisha yetu inafanywa na vile vitu vinavyotokea kwetu na tusivyoweza kabisa kuvibadili kwa uwezo wetu.

Asilimia 90 ya vyote vinavyotokea katika maisha yetu vinategemea jinsi tunavyonyesha hisia zetu.  Kamwe hatuwezi kubadili chochote wala kugeuza chochote katika yale yanayotokea kwetu katika ile asilimia 10% mfano, hatuwezi kubadili wala kuzuia pale gari linapoharibika barabarani, hatuwezi kuzuia wala kubadili chochote pale ndege inapochelewa kuondoka uwanjani,  hatuwezi kufanya chochote pale kitu kinapoingilia safari yako barabarani na kukuchelewesha, kwa mfano foleni isiyotarajiwa.

Lakini ile asilimia 90 ni tofauti, sisi tunauwezo mkubwa  katika kuiamua na kubadili hali kutegemea na vile tunavyozionyesha hisia zetu. Huwezi kuzuia taa nyekundu inapowaka barabarani kukuashiria usipite, lakini waweza kuzitawala hisia zako zinazoweza kusababishwa na taa ile. Kamwe usimruhusu mtu au watu wakupumbaze au kukufanya mjinga kwa kuzichochea hisia  zako.  Jaribu kujitawala na kujiweza.

Labda  tutumie mfano huu; Unapokunywa chai asubuhi na familia yako mara  binti yako anagonga  kikombe kwa bahati mbaya na chai inamwagika na kuchafua shati lako la jeupe la kazini.  Hapa kwakweli huna lolote la kufanya juu ya kilichotokea, (maji yamekwisha mwagika), kinachofuata sasa kitategemea na utakavyozionyesha hisia zako. Je, utalaani, utatukana, utabwata, utampiga makofi binti yako?  Kama utamchapa, baada ya hapo labda pia utamgeukia mke wako na kumgombeza kwa kuweka kikombe vibaya mezani, na hapo mtaanza kuzozana  na mkeo.

Mara utaenda chumbani kubadili shati na kwa hasira utatoka na kumkuta binti yako akiendelea kulia, na kwa kulia na kutokunywa chai anaachwa na gari la shule.  Labda mke wako hawezi kumpeleka binti yako shuleni, kwahiyo unalazimika kumchukuwa kwa  hasira kumuwahisha shuleni, kwa sababu umechelewa unaendesha kwa kasi sana kiasi cha kusimamishwa na askari wa barabarani na kutozwa faini. Mara baada ya kucheleweshwa zaidi na askari  mnafika shuleni na mwanao mmenuniana, na kwa hasira anaruka toka kwenyegari bila hata kukuaga na kukimbilia dasani.  Unatoka na kukimbia ofisini, mara unapoingia tu ofisini unakumbuka umesahau begi lako la ofisini, kwasababu tu ulitoka chumbani kwa hasira.  Siku yako imeanza vibaya, itaendelea vibaya na kuwa mbaya zaidi hata mwisho wake.  Unaporudi numbani unakuta mama na binti wote hawana amani na wewe, kwa kile ulichokianzisha asubuhi.

Yote haya kwanini?  Ni kwa vile ulivyozionyesha hisia zako asubuhi.

Kwanini siku yako imekuwa mbaya?

Je ni chai imesababisha?

Je ni binti yako amesababisha?

Je ni askari wa barabarani?

Au ni wewe uliyesababisha?

Ukweli ni kwamba hukuwa na lolote la kufanya kwa kumwagika kwa chai, lakini jinsi ulivyoonyesha hisia katika zile sekunde tano, ndipo ulipoharibu siku yako. Yamkini ingekuwa bora ungefanya tofauti kama ifuatavyo.

  • Chai imemwagika katika shati lako la kazini,
  • Binti yako anataka kulia kwa hofu
  • Taratibu mguse begani na kumwambia asihofu kwasababu hali kama hizo hutokea, ila awe makini wakati mwingine awapo mezani.
  • Chukua taulo haraka jifute, na kubadili shati na utoke na begi lako la kazini na kuagana na binti yako akienda kupanda gari la shule.
  • Ondoka, wahi kazini na upate dakika chache za kusalimiana na wafanyakazi wachache kabla ya kuanza kazi.

Angalia tofauti hapa!

Imekuwa michakato  miwili tofauti, yote ilianza kwa tukiko moja, na yote imeishia katika hali za tofauti.

Kwanini? Kwa sababu ya jinsi ulivyoonyesha hisia zako.

Hapa utaona ukweli kwamba, unanafasi kubwa ya kuzitawala asilimia 90 za yale yanayoendelea maishani mwako, hususani kwa jinsi uzitawalavyo hisia zako.

Jinsi ya kuitendea kazi kanuni hii

Iwapo mtu au watu wanakusema au kukufanyia mambo mabaya,  usiyameze tu na kuyaruhusu yakuumize.  Yaruhusu yakutoke haraka kama vile maji yanavyoachana na glasi.  Usiziruhusu semi mbovu ziumize moyo wako.  Onyesha hisia zako kiusahihi na kwa kufanya hivyo hautaiharibu siku yako.

Kwa kuonyesha hisia zetu vibaya twaweza kupoteza marafiki, twaweza kufukuzwa kazi, twaweza kuharibu jina na sifa yetu au kujiongezea msongo wa mawazo. Unafanyaje pale mtu anapokuendeshea gari vibaya au kukuchomekea ukiwa barabarani unaendesha,  unatukana? unalaani? unagonga usukani au kupiga honi kwa hasira?  Je unapofanya hivyo kuna anayekujali?  Kwanini uruhusu magari ya haribu raha ya uendeshaji wako. (usisahau kanuni ya 90-10).

Umeambiwa unafukuzawa au unapunguzwa kazi,  kwanini upoteze usingizi na kukaa ukihofu?  Inawezekana kubadili hiyo hali.  Tumia nguvu, nishati na muda unaoutumia kuhofu na kupaniki na uanze kutafuta kazi nyingine. Unasafiri na ndege, au basi na kwa bahati mbaya basi au ndege imechelelewa kuondoka, usiruhusu hasira na hisia mbaya kukuharibia safari yako nzima.  Kwa nini umkasirikie mhudumu wa ndege au basi, wakati yeye hana lolote analoweza kufanya katika uchelewaji huo?  Tumia muda huo kujisomea kitu chochote ulichobeba, tumia muda huo kufahamiana na abiria mwenzako, taratibu utajikuta unajenga na wala sio kubomoa.

Kanuni hii ni ya uhakika na imewasaidia wengi, ingawa watu  wengi bado hawajaitumia katika maisha yao ya kilasiku.  Jaribu leo katika maisha yako na utaona tofauti kubwa katika matokeo. Mamilioni ya watu wanateseka katika misongo ya mawazo, majaribu, matatizo, na maumivu mbalimbali.  Kama tukijaribu kuitumia kanuni hii itayabadili maisha yetu kwa kiasi kikubwa sana.  Inagharimu tu utayari wako katika kujiruhusu mwenyewe na kuyaruhusu mabadiliko maishani mwako.

Kumbuka; kile tunachokifanya, kile tunachokitoa, tunachokisema au hata kukiwaza mara zote  huturudia sisi wenyewe na mara nyingine kutugharimu pia. Kama unapenda na unatamani kupokea, lazima ujifunze kutoa kwanza, Yamkini ukitoa utabaki na mikono mitupu, yenye alama ya kuhitaji kupokea lakini moyoni upendo ukiwa umejaa.  Hii ndiyo tabia ya yoyote anayeyapenda maisha.

 

Imeandaliwa na;

Dr. Chris Mauki

Social, Relationship & Counseling Psychologist

University of Dar es Salaam

www.chrismauki.co.tz

chrismauki57@gmail.com

0713 407182

 Dr. Chris Mauki. An expert in Relationships, Social and Counseling Psychology. Lecturer in Psychology: UDSM. Inspirational & Motivational speaker. Family man


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *