DARASA LA ALHAMISI NA DR. CHRIS MAUKI: MAMBO MATANO MUHIMU YA KUFANYA KABLA YA KUFIKIA MIAKA 40

 

MAMBO MATANO MUHIMU YA KUFANYA KABLA YA KUFIKIA MIAKA 40  

 1. Jiwekee malengo ya kifedha

Weka maamuzi binafsi ya nini unachokihitaji na wapi unakotaka uwe kimaisha hapo mbeleni. Yaweke malengo yalio ya kifedha katika makundi yafuatayo

 • Malengo ya muda mfupi
 • Malengo ya muda wakati
 • Malengo ya muda mrefu

Malengo haya yanaweza pia kugawanywa kufuatana na mahitaji uliyonayo. Vile vyenye uhitaji mkubwa vikapewa umuhimu katika malengo n.k. Tafiti za maeneo mbali mbali zimejaribu kuweka mifano ya malengo haya kama ifuatavyo.

Mipango ya muda mfupi (short term goals)

 • Kununua gari jipya (ingawa hii hutegemea na uwezo binafsi)
 • Kuandaa harusi
 • Kuendelea na shule ya juu (Graduate school)

Malengo ya muda wakati (Mid term goals)

 • kupata watoto
 • kujenga nyumba
 • kuanzisha biashara

Malengo ya muda mrefu (long term goal)

 • Kuweka fedha kwa ajili ya kustaafu (Retirement pension schemes)
 • Kujenga nyumba kwa matumizi ya likizo (vacation home)
 • Kufungua akaunti ya watoto wakiwa wadogo
 1. Tengeneza fungu la fedha la dharura

Wengi wetu hatuna tabia za kujiandaa kwa majanga na dhama mbali mbali na hivyo mambo haya yanapotokea tunakuwa katika hali mbaya zaidi. Hii ndio maana wengi wetu wanapojikuta wako katika misiba, au majanga mbali mbali, hukimbilia kukopa au kuchukua advance za mishahara nahii huwaacha wengi katika madeni sugu.

Fikiri ni kiasi gani cha fedha kinahitajika kwa majanga au dharura ambazo zaweza kutokea katika mzunguko wa maisha ya kila siku. Inashauriwa kuwa, ujaribu kuweka fedha inayolingana na matumizi yako ya mwezi kwa miezi 3 – 6 kama fungu la dharura. Hii ni fedha ambayo itakuwa tayari kutumika mara tu upatapo dharura yeyote kama vile, Ugonjwa wa mwanafamilia, ajali kupoteza kazi, msiba wa ghafla n.k. (najua wengine wenye imani zao wana mitazamo tofauti na hili lakini piga hesabu jinsi unavyosumbuka na hata kusumbua wengine pasipo sababu muhimu pale dhahama inapokukumba na haujajiandaa hata kidogo.

 1. Anza kuwekeza

Hatua ya pili ya kuandaa fungu la dharura na majanga ni lazima iwepo tayari kabla hata haujaanza kuwaza kuwekeza. Kuwekeza kunatupa kipato cha nyongeza ili kutia nguvu kile kidogo kinachopatikana toka kwenye mshahara au fedha ulizojiwekea benki hii inakusaidia kuanza mchakato wa kuwa tajiri.

 1. Anza kuwekeza kwa maandalizi ya kustaafu

Hii ni zaidi kwa wale wanaofanya kazi katika ajira mbali mbali za kuajiriwa pamoja na waliojiajiri. Takwimu zinaonyesha kuwa, mtu wa maisha ya kawaida anahitaji asilimia 70% za kipato chake cha kabla ya kustaafu ili kumsaidia kuendelea maisha katika hali ile ile aliyokuwanayo, mara tu atakapo acha kufanya kazi. Mfano; Mtu anayepata sh. 500,000 kwa mwezi atahiraji shilingi 350,000 kwa mwezi mara atakapoacha kufanyakazi ili tu kuweza kuishi maisha ya aina angalau sawa na aliyokuwa akiishi kabla ya kuacha kazi.

Fedha za malipo ya uzeeni pensheni hazitoshi kukidhi mahitaji yako hata kidogo. Na inabidi usisahau kuwa takwimu zinaonyesha kuwa mtu wa kawaida anategemewa kutumia 1/3 ya maisha yake yote katika muda wa kustaafu kazi (muda ambao hata mwili wako hauwezi kuzalisha kama awali)

 1. Piga hesabu ya uwezo wako wa kuwa tayari kupoteza; je ni kwa kiasi gani uko tayari kupoteza. (How much are you ready to take risk?)

Tafiti zaonyesha kuwa watu wenye umri mdogo wana uwezo wa juu wa kukubali au kuwa tayari kupoteza (taking risks) kuliko watu wazima. Pia takwimu zinaonyesha kuwa wengi waliofanikiwa duniani walikuwa tayari kupoteza. Huwezi kujiita mfanyabiashara kama hauna ujasiri wa kuwa tayari kuziwekeza fedha zako katika mtaji ambao hauna uhakika wa kurudisha faida. Inahitji kiwango cha juu sana cha kukubali kupoteza na kuwa tayari kupata hasara. Kwa ajili hii ili uweze kupata upenyo mapema unashauriwa kuanza kuwekeza ukiwa kijana wakati ambapo uwezo wako wa kukubali kupoteza uko juu, kinyume na kusubiri ukiwa mtu mzima sana wakati ambao utakuwa unahofia kila kitu unachokiona au kukiwazia.

Kwa hiyo: Fahamu uwezo wako wa kuwa tayari au kukubali kupoteza.  Fahamu uwezo wako wa kuweza kuvumilia pale hasara yakupoteza inapotokea. Umri wa ujana unampa mtu uwezo mkubwa kwa kuwa tayari kujaribu vitu vipya mara kwa mara, na kuweza kujirekebisha kwa urahisi pale makosa yanapotokea kuliko umri wa utu  uzima sana. Wakati ambapo majukumu huzidi idadi ya nywele za kichwani na kiwango cha msongo wa mawazo huwa juu sana.

 

Imeandaliwa na;

Dr. Chris Mauki

Social, Relationship & Counseling Psychologist

University of Dar es Salaam

www.chrismauki.co.tz

chrismauki57@gmail.com

0713 407182

 Dr. Chris Mauki. An expert in Relationships, Social and Counseling Psychology. Lecturer in Psychology: UDSM. Inspirational & Motivational speaker. Family man


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *