DARASA LA ALHAMIS NA DR. CHRIS MAUKI: NINI KINACHOWAFANYA WANAUME WENGI KUWAKIMBIA WANAWAKE MWANZONI MWA MAPENZI?

NINI KINACHOWAFANYA WANAUME WENGI KUWAKIMBIA WANAWAKE MWANZONI MWA MAPENZI?

 

Utangulizi:

  • Kila mwanaume aingiapo katika mahusiano huanza uchunguzi kimyakimya, wakati wanawake wao huweza kuchunguza kwa kuuliza au kudadisi.

 

  • Mara mwanaume anapogundua kuwa mazingira aliyopo hatoyaweza basi huanza kufungasha virago vyake kimya kimya na akishafanya maamuzi ya kukukimbia basi utaona visingizo na sababu tele zisizo na mashiko zikimiminika. Kwa mfano utasikia maneno kama vile; “Mimi nahisi tofauti ya dini zetu itatusumbua huko mbeleni”, “Naona wazazi wangu wanakuwa wagumu sana kwenye mahusiano yetu”, “Ndugu zangu wamenishauri nisubiri kwanza”, “Nimepata nafasi ya kwenda kusoma mbali”, “Kwa sasa nashindwa kufanya maamuzi magumu maana nina mipango fulani ya maisha naifanyia kazi”, “Nahisi bado sijajipanga kifedha kuweza kuanza familia”.

 

  • Kama hatotoa visingizio hivi basi anaweza kutafuta kitu anachojua fika kwamba hautokikubali na akaamua kukisimamia hicho ili ukikikataa uwe mwisho wa mahusiano yenu, kwa mfano atasema; “Mimi ninaona tuzae kwanza halafu baadae tutafunga ndoa” (hapa kama amejua fika kuwa wewe hauna mpango wa kuzaa nje ya ndoa), au atasema “Tuishi pamoja kwa sasa halafu nikiwa sawa tutaanza mchakato ya harusi”.

 

Fahamu kwamba: Sababu hizi zinaweza kujidhihiridha kwenye mahusiano kabla ya kuingia kwenye ndoa au hata mkiwa kwenye ndoa na hivyo kusababisha ndoa nyingi kuvunjika mapema sana, hususani zile zinazopasuka chini ya miaka mitano.

 

Sababu:

  1. Wanapohisi au kuona utegemezi

Utegemezi huu unaweza kuwa katika maeneo mengi ya maisha lakini wenye madhara sana ni utegemezi wa kiuchumi. Ingawa mwanaume anajua kuwa anawajibika kwa mpenzi wake lakini mara nyingi huwa mwoga na mwenye kuhamaki sana pale anapoona kila dakika anaombwa fedha au kuombwa msaada wowote ambao kwa namna mmoja au nyingine utamgharimu fedha. Wanaume wengi hupendelea na wanahisi usalama zaidi pale ambapo wapenzi wao wa kike wanaonyesha kujitegemea au kujiweza katika baadhi ya mambo. Mara nyingine hata kama mwanaume anaonyesha kuwa tayari kuwajibila kwa asilimia zote kwa mpenzi wake, lakini bado ndani yake anatamani kuona ule utayari wa mpenzi wake kujisimamia na kujitegemea. Wale wakinadada wenye tabia ya kuanza kuwakilisha shida zao nyingi mbele ya wapenzi wao wa kiume kama vile wamewapenda ili wawe watatuzi wa matatizo yao binafsi nay a familia zao pia, wakina dada hawa mara kwa mara kupata shida ya kupendwa au hata kuchumbiwa mara nyingi na kuachwa pasipo kujua kwanini wanaume wanawakimbia.

 

  1. Pale wanapohisi au kuona kuwa unawakwepa au kutowafurahia wazazi/ ndugu zake

Hata kama kuna changamoto fulani kutoka kwa ndugu zake, wanaume wengi wanatamani kuona jitihada zako kwenye kuwa karibu na wazazi au ndugu zake, na kama kuna vikwazo basi muwasiliane kwa pamoja katika namna ya kuvishughulikia. Iwapo utaamua tu mwenyewe kuwakwepa au kujiepusha nao pasipo sababu yenye mashiko, au ukaamua kumwambia wazi kuwa hauwapendi au hauwahitaji ndugu zake basi utaona wazi hofu yake ya kuwa na wewe. Wako wakina dada walioifahamu siri hii na utawakuta wakijipendekeza na kujipeleka zaidi kwa wakwe au ndugu wengine wa mwanaume ili tu mpenzi wake wa kiume afurahi, ni kweli wamefaulu katika hili lakini ni vema upendo wako ukawa halisi na sio ulio wa uongo au feki.

 

  1. Wanapohisi au kuona dalili za mtu mbishi na mpinzani

Kwa kawaida wanaume wana asili ya ubishi na kupinga hoja za wengine, sio za wanawake tu hata za wanaume wenzao, hii ni kwasababu ya kiasili kwamba wanaume ni watu wanaosukumwa na kutaka au kuona ushahidi au sababu za uthibitisho katika kila kinachosemwa. Kwa bahati mbaya wakiona au kuhisi tabia hii kwa mwanamke basi ghafla huhamaki na kuhofia kujikita kwenye mahusiano na mtu wa aina hii wakiogopa kuja kushindana au kukwaruzana huko baadae.

 

  1. Wanapoona au kugundua dalili za kutawaliwa au kukaliwa

Kwa kawaida wanaume wanafuata mapokeo ya asili kwamba wao ni viongozi na watawala wa familia, wao hutaka kuliona hili hata kabla hamjaingia kwenye ndoa. Kwa bahati mbaya wako wanawake au kwasababu za kiasili au malezi na makuzi wamekuwa ni wenye kutaka kupewa nafasi, kutaka kuamrisha, kuongoza au kufanya maamuzi kwa wengine na wasio rahisi kuongozwa. Wanawake wa jinsi hii nio rahisi sana kukimbiwa na kila mwanaume anayetaka kuwanao kwenye mahusiano, au hata kama wameishia kuoana basi hukutana na mashindano au misuguano mikali kwasababu mwanaume huona ni bora ndoa ife kuliko kuipoteza nafasi yake ya uongozi au ukuu wa familia hususani katika nguvu ya kufanya maamuzi. Katika kujitutumua huku mwanaume anaweza kuonyesha tabia nyingi sana zenye kumuumiza mwanamke, kama vile hasira za mara kwa mara na za ghafla, fujo, matusi, na visasi vya aina nyingi.

 

  1. Wanapoona ukaribu au utegemezi mkubwa wa wazazi au ndugu zako

Ndoa imetengenezwa katika hali ya kwamba wanandoa wote wanatakiwa kuwaacha wazazi au ndugu zao na kushikamana na wenza wao katika mambo yote ikiwemo maamuzi yao. Wanaume wengi huwa makini sana tena kimya kimya kuangalia jinsi wapenzi wao wa kike wanavyohusiana na wazazi wao na ndugu zao wengine. Iwapo watagundua umemezwa, umekamatwa na kushikwa jumla na nduguzako, hauwezi kufanya maamuzi yeyote bila wao kuyaridhia, hatayale yamhusuyo mumewako basi wao huhamaki na kuwa na hofu kubwa huku mioyo yao ikiona kama wao ndio wameolewa badala ya kuoa. Hisia hizi ni mbaya sana kwa mwanaume, na hivyo kuweza kujihami kwa kurusha mishale ya maneno na kuamsha misuguano mingine, sawa sawa na ile niliyoisema kwenye sababu ya nne. Kushirikiana na ndugu zetu sio kitu kibaya ili mradi nafasi ya mume ibaki pale pale na kuheshimiwa hata kama mchango wake kiuchumi hauonekani kuwa na mashiko. Kwa upande mwingine katika hili, inaweza kumuwia ngumu kuolewa binti anayetegemewa kwa asilimia 100 na ndugu au wazazi wake, kwa maana kila kijana anayejileta kwake hata kama binti ni mzuri, bado kijana anaona mzigo mkubwa mbeleni na kuamua kumwepa au mumkimbia.

 

  1. Wanapogundua ugumu au matatizo fulani kwenye tendo la ndoa

Ni ukweli usiopingika kwamba wanaume wameumbwa kupenda na kutamani kufanya tendo la ndoa mara kwa mara, wao ni rahisi sana kukimbizwa katika mahusiano yao na mwanamke pale wanapogundua au kukutana na ugumu wowote kwenye suala zima la ufanyaji wa tendo la ndoa, ingawa ni mara chache sana wanaweza kuwa wazi wakwambie nini kinacho wasumbua au wasichokipenda, labda muwe na kiwango cha juu sana cha mawasiliano. Baadhi ya vitu vinavyoweza kuleta ugumu au changamoto kwenye tendo la ndoa na kumfanya mwanaume akimbie ni kama vile, umbo kubwa au uzito wa mpenzi wake wa kike, harufu mbaya ya sehemu za siri au maeneo mengine ya mwili kama vile chini ya matiti, mdomoni au puani, changamoto nyingine ni kama vile ukavu uliopitiliza, au uchafu mwingine wa mwili usiovumilika.  Mambo haya na mengine yanayofanana na haya huweza kumkimbiza mwanaume mapema sana, tena akakimbia kimya kimya na labda baadae ndiyo unaweza kusikia akilalamika pembeni kuhusu kisa kilichomkimbiza kwako.

 

  1. Akigundua unamtoto/watoto au uliwahi kutoa mimba

Wanaume wengi huwa na kiu ya kuja kuanza familia zao wao wenyewe na sio kukuta mtoto wa mwingine. Ni rahisi sana mwanamke akamkuta mtoto wa mumewe na akaendelea kuishi naye kuliko mwanaume kumkuta mtoto wa mke wake na kuishi naye bila matatizo. Hii ndio maana kinadada wengi wakisha pata ujauzito kabla ya kuolewa wanahisi au wanakumbana na changamoto kubwa sana katika kuchumbiwa na wanaume wengine kwasababu tu mtoto anakuwa kikwazo. Vilevile mwanaume anapogundua kama mpenzi wake amewahi kutoa mimba huwa anakuwa na hofu ya kuendelea na mahusiano maana anakuwa kwenye njia panda ya uhakika wa kupata mtoto au la. Sio tu kutoa mimba bali hata sababu au mazingira yeyote yanayoweza kumpa mwanaume hofu au mashaka ya kuja kupata mtoto, haya yanaweza kumkimbiza mwanaume kutoka kwenye mahusiano mliyonayo, ingawa akianza kuchomoka huwa anatumia visingizio vingi na sio sababu halisi. Ushauri wangu katika hili ni kwamba, kama unamtoto basi usifiche, jaribuni kuongea mapema na kuelewana, kama mtoto ni wa mwanamke au mtoto ni wa mwanaume, yawekeni mezani mapema, kwamaana yakija kujulikana huko mbeleni huwa yanaleta maumivu makali na visa visivyoisha na vinavyoendeleza machungu katika ndoa na hata kupelekea ndoa kuvunjika.

 

Na: Dr. Chris Mauki

Social, Relationships and Counselling Psychologist

Chrismauki57@gmail.com

www.chrismauki.com

 

 

 

 Dr. Chris Mauki. An expert in Relationships, Social and Counseling Psychology. Lecturer in Psychology: UDSM. Inspirational & Motivational speaker. Family man


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *