DARASA LA ALHAMISI NA DR. CHRIS MAUKI: IFAHAMU SAIKOLOJIA YA PESA (VITA ILIYOPO KATI YA MAWAZO NA HISIA): 16.08.2018

 

IFAHAMU SAIKOLOJIA YA PESA

(Vita iliyopo kati ya mawazo na hisia)

Wengi wetu tumeishi au tunaishi katika vitakubwa katika suala zima la matumizi ya fedha tuliyonayo, wengi tumekuwa na maswali mengi katika hili na wengine wetu tunajikuta tunafanya baadhi ya maamuzi bila kujua chanzo na kwanini tunafanya hivyo. Kwamfano maranyingine unajikuta kwenye njiapanda ambayo ndani yako unatamani sana kununua kitu na wakati huohuo kuna sauti ya ndani inakwambia hiyo hela unaweza kuisamehe na kuihifahdi kwa matumizi mengine ya muhimu zaidi baadae. Baadhi yetu wako ambao wanaweza kuishinda vita hii na kuamua kutotumia pesa hiyo ila wengi hushindwa na kujikuta tunatumia kiasi kile na ndani yetu tukijipooza kwamba tutapata nyingine tu. Hali hii ndiyo inanipa dhumuni la kuandika makala hii ili kujaribu kuwasaidia baadhi yetu.

Katika kuangalia mtazamo mzima wa matumizi ya binadamu ya fedha, zipo nadharia mbalimbali zinazojaribu kulielezea swala hili. Kwamfano iko nadharia inayoamini kwamba binadamu hufanya maamuzi ya busara kabisa akiangalia faida na hasara kila anapotaka kufanya matumizi ya pesa yoyote, akiangalia umuhimu wa pesa aliyonayo inapotumika leo na kama ingetumika siku zijazo. Wakati huohuo ikonadharia ambayo inapingana na hii ambayo inasema mwanadamu wa kawaida hana busara hii, bali hutumia kutokana na umuhimu unaojitokeza na jinsi anayoona kwa mtazamo wake yeye mwenyewe. Ile raha na furaha ya kuona unafanikiwa au unaweza kuhifadhi fedhayako kwa matumizi ya muhimu tu nasiyo kila matumizi ukisukumwa na hamu zako inategemea kama hii busara iliyosemwa kwenye nadharia ya kwanza unayo. Kama hauna busara hii basi wewe kila kitu unaona sawa tu, fedha ulionayo itumike vyovyote vile unaona sawa kwasababu pia ilitengenezwa ili itumike.

Tafiti kadhaa zinaonyesha kuwa jinsi miaka inavyozidi kwenda uwezo wa wengi wakuisimamia busara hii ya kupigahesabu au kuzihusisha fikra zao katika kila wanapotaka kufanya matumizi ya pesa inapungua kwa kasi sana. Hii ndio sababu ya malalamiko ya wazazi wengi juu ya kizazi cha sasa kilivyo cha matumizi makubwa hata pale ambapoanayetumia siyo aliyezalisha au anatumia zaidi ya anavyozalisha. Hali hii inaweza kuendelea kuwa mbaya zaidi siku zijazo kufuatana na hitimisho la tafiti hizi.

Yako mambo machache ambayo ni muhimu na ya msaada sana tukiyafahamu. Ni vema tujue siri iliyopo kati ya sababu inayotusukuma tufanye matumizi fulani na wakati huohuo sababu hiyo inashindana na hisia zetu. Katika hali hii kuna sauti mbili zinazosikika ndani ya mtu, ya kwanza inasema nunua kitu hiki, ni kizuri sana, na utakifurahia, na wakati huohuo sauti nyingine inakwambia sio lazima ukinunue leo, jitahidi kuihifadhi fedha hiyo utaihitaji sana baadae. Mchakato huu mzima wa mazungumzo na ushindani huu unaendelea ndani ya soko au duka tena wakati macho yako yakikiangalia kwa tama kitu kile ambacho sauti moja inakwambia kichukue, hali hii siyo nzuri kwa wengi kwasababu hatuipendi, tunatamani sauti hii ya pili isingekuwepo, tuwe huru tu kuchomoa hela kwenye pochi zetu na kilakitu kiende sawa. Mchakato huu mzima huwa unafanya misuli ya uwezo wetu wa kujizuia (self-control) ilemewe na mzigo zaidi na misuli hii inaposhindwa nguvu na msukumo huu wengi wetu hujikuta tunaamua kununua tu, ndani yetu tukijiambia “liwalo na liwe, kwanza sinimekipenda? Hizi hela zipo tu, je nikikiacha hichi kitu leo halafu kesho nikikikuta hakipo, bora nikibebe leo hii hii!!”

Pia unahitaji kufahamu mambo yafuatao:

  1. Kuongezeka kwa kufikiria na kuwaza sana juu ya nini ninunue au nisinunue hupunguza kwa kasi uwezo wetu wa kujizuia (self control)

Kama ulikuwa hujui basi ni vema ujue leo kwamba hii mbinu ndiyo wanaitumia sana watu wa matangazo ya biashara na wale wanaojihusisha na mambo ya masoko au mauzo. Angalia kwenye maduka makubwa  “malls au supermarkets” angalia kwenye “promotions” za bidhaa mbali mbali, mara zote utakuta picha nyingi za bidhaa mbali mbali na bei zake, kelele za kukwambia nunua hiki kwasababu hizi na zile, sauti nyingine tamu na yamkini za jinsia tofauti na yako zikikwambia usiende kwa mtoa huduma flani vitu vyake sio kama hivi, njo tukuonyeshe. Picha, makelele na vishawishi vyote hivi niayake ni kuku “destruct”, kukuongezea mzigo wa ndani ya akili “cognitive load” na mara unapowaza sana kwenye sijui nichukue sijui niache unakuta uwezo wako wa kujizuia (self-control)  unashuka na hapo unaingiza mkono nyuma (kama wewe ni mwanaume) au kwenye pochi (kwa wanawake) nakutoa pesa ili kununua bidhaa au huduma. Maranyingine nimegundua hata kule kujaza bidhaa tele kilakona katika maduka makubwa kuna athari fulani kisaikolojia, jaribu kujichunguza vita iliyoko ndani yako unapokuwa kwenye duka la kawaida ambako vitu au bidhaa zake haziyamezi macho yako, na angalia wakati unapokuwa kwenye “malls au supermarkets” ambako bidhaa zake ni nyingi na huyameza macho yako.

 

  1. Uwezo wetu wakujizuia unaukomo

Mara kwa mara uwezo wetu wa kujizuia, uwezo unaotuwezesha kuamua kutonunua kile ambacho busara yetu inatuambia sio cha muhimu kwa sasa, uwezo huu huchoka na kushindwa nguvu pale unapotumika mara kwa mara au pale unapolemewa na mzigo mkubwa. Vitu vingine vinavyoweza kupunguza nguvu za uwezo huu ni matumizi ya vilevi kama pombe, sigara, dawa za kulevya, mwili kukosa usingizi wa kutosha n.k.

  1. Uwezowetu wa kujizuia unaweza kuathiriwa na hisia zetu

Unapokuwa na huzuni nirahisi sana kujikuta unatumia pesa nyingi katika kiu ya kutamani kujiburudisha ili ujisikie afadhali. Nimeongea na wengi ambao walipokuwa katika huzuni walikunywa sana pombe, labda zaidi sana ya matumizi yao ya kawaida. Hii ni pamoja na matumizi mengine ili tu kujifurahisha. Imegundulika pia kwamba katika hali ya huzuni wengi hujikuta wakiwa rahisi kuuza walivyo navyo kwa bei ya chini sana na isiyo ya faida hata kama vitu hivyo ni vya garama sana, au kununua kitu kwa garama zaidi wakati vitu hivyo ni rahisi. Hali ya kukinai pia inaweza kukufanya kujisikia kuto kutaka tena kitu fulani na hivyo kutaka kipya, hali hii iko sana kwa jinsia ya kike, ambao wao wakijisikia kukichoka kitu (mfano nguo, viatu n.k) basi hapalaliki mpaka kitu kipya kinunuliwe. Kukinai huku sio kwenye bidhaa tu bali hata katika huduma au eneo, inawezekana umezoea kula au kukaa maeneo fulani ambayo ni garama nafuu, ikitokea unajisikia kupakinai basi kwenda eneo linguine la garama zaidi kwako haitokuwa ni tatizo.

Hisia nyingine inayoweza kuathiri uwezo wetu wa kujizuia ni hofu. Mara tunapokuwa na hofu kinachofuata ni jitihada za kujiwekea mazingira ya kutoihisi hofu hiyo hata kama mazingira hayo ni garama sana. Mfano angalia mtu mwenye hofu ya kuibiwa, hata kama hofu hiyo sio halisi sana ukilinganisha na mazingira basi nirahisi kwake kutumia garama yoyote kwenye kujilinda. Ukizingirwa na hofu wala hupotezi muda kuwaza kutumia au kutotumia hela, bali unachokitaka wewe unahakikisha unakipata.

Jinsi gani unaweza kufanya maamuzi ya busara kuhusu pesa zako

Jizoeze kujiwekea mipaka au vikomo “limits”.

Katika matumizi yako ya kila siku jifunze kujiwekea vikomo au mipaka, kujiwekea mipaka au vikomo katika matumizi hukusaidia sana katika uwezo wako wa kujizuia. Kwa mfano katika nchi mbali mbali zilizoendelea, hata hapa Afrika ya kusini  ambapo watu hufanya manunuzi kwa kutumia kadi, kila mtu anapewa uhuru wa kuamua kikomo cha manunuzi yake kwa siku kutokana na jinsi anavyoyajua matumizi yake. Mara unapofikia kikomo hicho katika siku ile basi hakuna hela itakayotoka kupitia mashine za pesa “ATM” au katika kuchanja “swiping” kwenye manunuzi ya bidhaa. Profesa Ariely ameongea sana na kufanya tafiti nyingi juu ya kuongeza uwezo wetu wa kujizuia kupitia kujiwekea vikomo vya matumizi. Mfano mwingine ni vile vikopo, au visanduku watu wanajiwekea manyumbani, ambapo kila mtu anapopata hela fulani aliyojipangia huitumbukiza kwenye kopo na mazingira ya kuitumia au kuichukua fedha ile huwa yamedhibitiwa au kufwanywa kuwa magumu ili tu hela ile ifikie malengo fulani.

Jipe muda wa kutulia na kupoa “cooling off periods”

Kama nilivyokwisha kudokeza awali, hisia zetu za kilasiku ziwe mbaya au nzuri ninaweza kuathiri sana mchakato mzima wa maamuzi yetu ya kutumia pesa. Katika hili tunashauriwa sana kuchukua muda hususani kabla yakufanya maamuzi makubwa ya kifedha, kupoa kidogo na kujiuliza na kufikiri kwa kina kama kweli unachotaka kufanya kina faida kwa leo na kwa kesho. Usifanye maamuzi ya nayohusiana na matumizi ya pesa baada ya kushauriwa na kuhamasishwa sana na muuzaji. Ikibidi kama ni biashara ambazo wana vipeperushi “fliers” omba kimoja nenda nacho nyumbani pumzika, kisome na ukitafakari. Wengi wetu wamejuta sana baada ya kufanya maamuzi ya msingi sana yahusianayo na matumizi ya pesa pasipo kuwaza kwa kina au wakati ambapo nafsi na akili zao zilikuwa hazijapoa.

Chunga sana uwezo wako wa kujizuia “self-control”

Nimesema kwamba uwezo wetu wa kujizuia huweza kuchoka pale unapotumiwa sana. Ni lazima kujifunza kuukagua uwezo wetu huu kila mara. Kama utaona uwezo wako wa kujizuia umechoka basi usifanye maamuzi yahusuyo matumizi siku au muda huo. Kwa mfano siku ambayo umeshinda kwenye maduka muda mrefu, siku ambayo umeshawishiwa sana na wauzaji wa bidhaa fulani, siku uliyochoka sana akili yako au ukiwa mwenye huzuni. Tulia, amua kufanya maamuzi hayo wakati ukiwa sawa.

 

Dr. Chris Mauki

University of  Dar es Salaam

chrismauki57@gmail.com

www.chrismauki.co.tz

 

 

 Dr. Chris Mauki. An expert in Relationships, Social and Counseling Psychology. Lecturer in Psychology: UDSM. Inspirational & Motivational speaker. Family man


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *