DARASA LA ALHAMISI NA DR. CHRIS MAUKI: JE UNAIJUA ASILI YA UONGO WA KIMAPENZI? (A SECRET BEHIND CHEATING)

JE UNAIJUA ASILI YA UONGO WA KIMAPENZI?

(A secret behind cheating)

Wako baadhi ya watu  wanaoamini kuwa kama ukweli  huuma basi uongo hauna budi kutumika katika baadhi ya maeneo au mazingira. Watafiti na waandishi mbali mbali wakekuwa wakijiuliza kwanini watu husema uongo? Na imefahamika kuwa uongo husemwa katika nyakati tofauti tofauti na kwa makusudi tofauti kabisa. Watu hudanganya ili kuficha makosa fulani makubwa wakihofia matokeo ya kile kilichofanyika,wengine hudanganya ili kumuepusha mwengine kutokufanya kitu kibaya, wako pia wanaodanganya ili tu kuficha hisia na matakwa yao yasijulikane na wengine, wakati wengine husema uongo ili kuficha na kuzifunika nafsi zao zinazohisi kufanya makosa.

Kwa bahati mbaya uongo ni uongo tu ingawa wako wanaoamini pia kuwa kama uongo unasemwa kwa nia ya kumuonea mwingine huruma basi huo sio uongo mkubwa wala wenye athari bali ni ucheleweshwaji tu wakusema ukweli, kwa maana nyingine ni ukweli uliocheleweshwa tu. Wengi tunajua kuwa wanasiasa  wanaaminika kuwa wataalamu wa uongo, wengi wametoa ahadi mbalimbali zisizo za kweli ambazo wakati zinatolewa kila mmoja aliona picha dhahiri ya ukweli na baada ya muda kidogo watu wakagundua kumbe ni uongo, wako ambao hawaaminiki tena katika kila wasemacho kwasababu watu wameshawajua kuwa hakuna wasemacho ambacho ni chakuaminika, lakini swali ni je? Waongo ni wanasiasa tu? Ukweli ni kwamba wako wengi na hata katika mapenzi ndiyo kwenye mizizi mingi ya uongo.

Katika eneo la mapenzi baina ya wale wanaopendana kumekuwa na utumikaji wa uongo sana, uko uongo mwingine unajulikana kuanzia mwanzoni kuwa huu ni uongo lakini mwingine unakuwa na sura ya ukweli kabisa na kuaminika, uko uongo ambao baadae ulikuja kujulikana kuwa haukuwa ukweli na ukaleta maumivu kwenye mioyo yawengine na baadhi ya uongo mpaka leo aliyedanganywa hajagundua kuwa alidanganywa ingawa aliyedanganya anajuwa kuwa alidanganya, watu hawa yamkini wanakaa pamoja na kucheka pamoja ingawa kuna mmoja anajua uhalisi wa upande mmoja wa shilingi wakati mwingine hajui kitu kabisa. Swali sasa ni je? Umedanganywa mara ngapi pasipo wewe kujua na utaendelea kudanganywa hadi lini? Na pia je unajua yanayoendelea nyuma ya uongo huo?

Labda nitumie uzoefu kidogo wa eneo la saikolojia kukuonyesha maeneo maarufu ambayo walioko kwenye mapenzi  kudanganyana sana, yamkini na wewe utagundua kuwa ndiyo unakodanganya zaidi au itakusaidia kufungua macho pale utakapohisi kuwa na wewe unadanganywa eneo fulani. Kwa mfano; watu wengi husema uongo katika kutoa sababu za kwanini hawapati muda wa kuwa pamoja  kama wapenzi, kama ujuavyo maranyingi wapenzi huwa na mida ya kuwapamoja na kuliwazana sana nyakati za mwanzo wa mapenzi yao, hukutana mara kwa mara, hutoka mara kwa mara, na hata kuwa na nyakati za tendo la ndoa maranyingi zaidi, lakini hali hubadilika baada ya kitambo fulani pale ambapo mpenzi mmoja hususani mwanaume anapoanza kuwa haonekani, mida mingi anadai yuko bize, kazi zinaongezeka, vikao na mikutano na safari za kikazi zinaongezeka tofauti na zamani. Sasa mara nyingi mpenzi mmoja anapouliza kutaka kujua sababu za mpenzi mwingine kutokuwa na ule muda wa mapenzi kama wa mwanzoni ndiyo hapo sababu nyingi za uongo zinapotolewa. Kama wewe ulisha wahi humuuliza mpenzi wako sababu za kwanini sikuhizi hamfurahii muda mwingi pamoja kama zamani, fahamu kuwa asilimia zaidi ya 90 ya sababu zilizo tolewa nay eye zilikuwa za uongo hatakama zilikuridhisha sana na nyingine mkapanga kuzitafutia ufumbuzi, mwaweza kujikuta mnatafutia ufumbuzi kitu kisicho halisi wakati ukweli anaujua yeye moyoni.

Wako wapenzi ambao huwafikiria wapenzi wao wa zamani hususani wakati wanafanya tendo landoa, ingawa kamwe hawatotaka ijulikane na kwahiyo wataufunika ukweli huu kwa kuzungumza uongo, hata maranyingine pia mwaweza kuwa mnatembea na mpenzi wako na akamuona mtumwingine mwenye umbo zuri na akavutiwa naye, hata kama umegundua na ukamuliza atapindisha hadithi na kutafuta uongo wa kufanana na mazingira yaliyoko na kasha utakubali anachokisema, hii yote ni kuficha ukweli kwamba hisia zake ziliguswa na yule mtu aliyemuona. Hii kufanywa ili kuzuia aije kukuumiza hisia zako pale utakapo gundua kuwa uko na yeye kama mpenzi na wakati huo huo hisia zake zikatekwa na mtu mwingine.

Wanaume wengi wamekaririwa kusema uongo kuhusiana na tabia zao za kujichua (masturbation). Wengi wamegundulika kujihusisha na tabia hizi hata wale walio na wapenzi wao pia, wako walioanza taratibu tu na baadae ikawa tabia sugu (addiction) na kuacha imekuwa ngumu hatakama wao sasa hawapendi tabia hiyo. Lakini hakuna anayeulizwa hususani na mpenzi wake akakubali kuwa anafanya matendo hayo. Wako wanaume wengi pia ambao kudanyanya zaidi kuhusu hisia zao za kutamani kufanya tendo landoa na wapenzi wao kinyume na maumbile, hata kama wakiulizwa unatamani kituhicho hukataa na kuruka wakati ndani yao wengi hujua kuwa wanatamani. Wanapoulizwa kuwa wamewahi kufanya tendo hilo? Pia husema uongo kuwa hawajawahi kabisa lakini ukweli maranyingi ni kwamba wamewahi na sio mara moja.

Wapenzi wengi hudanganyana sana kuhusiana na idadi ya wapenzi waliowahi kuwa nao kabla hawajakutana na kuanza mapenzi waliyonayo sasa hivi. Wengine hawatokwambia kabisa kama aliwahi kuwa na mtu na wengine watakwambia alikuwa na mtu mmoja na labda unamjua, ingawa katika kuendelea na mapenzi yenu siku baada ya siku utagundua mmoja baada ya mwingine na kujua kuwa alikuwa na idadi tele ya wapenzi, na kama ulidhani wewe ni wapili tu au watatu katika moyo wake unajikuta ni wa idadi isiyohesabika. Najua inauma kugundua kuwa umedanganywa, lakini ndiyo hivyo tena, umeshadanganywa, na ukweli umechelewa kukufikia.

Vitu vingine ambavyo  wapendanao kudanganyana ni katika idadi ya mara walizowahi kufanya ngono isiyosalama na wapenzi wengine, hata kama mpenzi mmoja akifahamu kuwa mwenzake aliwahi kufanya mapenzi na mtu mwingine, pale atakapouliza kama walitumia kinga, hakuna atakaye kataa, kla mmoja husema tulitumia kinga, uongo huu hutumika hapa ili kuzuia maumivu ya moyo kwa mpenzi mwingine pale atakapogundua kuwa mwenzake hakufanya ngono salama. Kwahiyo mara unapoambiwa mambo kama haya usifurahie sana na kuamini kwasababu kwa asilimia kubwa unadanganywa, na kuhatarishwa zaidi. Wapenzi wengi hususani wa kike husema sana uongo kuhusiana na hali zao za ubikira, kwamba walivunja ungo lini na katika mazingira gani, wengi pia hudanyanya kama hawakuwahi kutoa mimba, hii imeleta matatizo sana hata baada ya wapenzi kuamua kuoana,kwa wengi inakuja kujulikana pale ambapo matatizo ya kupata motto yanapoanza kutafutiwa ufumbuzi kupitia madaktari na inagundulika kuwa mwanamke aliwahi kutoa mimba. Wako waliofikia pabaya hata kuachana baada ya ukweli uliofichwa muda mrefu kudhihirika kuwa waliwahi kutoa mimba na yamkini siyo moja.

Baadhi ya wapenzi pia hususani wakike hudanganya kama waliwahi kunyanyasika kijinsia wakiwa wadogo, wako mabinti wliowahi kubakwa na ndugu zao wadamu au hata na mzazi wao, wapo waliowahi kufanyiwa mambo mabaya nay a kikatili ambayo hawawezi kuyasema kwa wapenzi wao na hivyo kujikuta wanadanganya tu. Bahati mbaya yako baadhi ya mambo yaliyotokea utotoni au ujanani yanayoweza kuathiri mahusiano baina ya wapendanao kama yasipowekwa bayana mapema na kushuhulikiwa.

Nikweli kuwa wapenzi wengi hudanganyana sana kuhusiana na vipato na vyanzo vya vipato hivyo, wapo pia wanaodanganya kuhusu madeni waliyonayo. Kwahiyo katika ujumla wa yote haya tunaona kuwa kusema uongo inaonekana kuwa ni asili ya binadamu  ingawa kuna baadhi ya mipaka na mipaka  hiyo inaelezewa kutokana na aina ya uongo mtu anaouongea. Baadhi ya vyanzo kama Wikipedia .com vimejaribu kuzungumzia aina 21 za uongo na hapa nitajaribu kutoa baadhi tu.

  1. Uko uongo ambao niuongo kwa wale wanaousikia tu (barefaced lie)
  2. Uko uongo ambapo mzungumzaji hujifanya kuwa anauwezo fulani au anajua siri fulani au ufahamu fulani wakati sio kweli (Bluff)
  3. Uko uongo ambao huonekana kuwa uongo sio kwa yale yanayosemwa bali kwa mazingira yanayohusishwa na kile kinachosemwa, ambayo mazingira hayo ndiyo yanayoudhihirisha uongo huo (contextual lie)
  4. Uko uongo ambao huonekana pale mtu anapotoa taarifa kama vile ni za kweli wakati yeye mwenyewe hana uhakika kama anachokisema ni cha kweli au sio kweli (Fabricated lie)
  5. Upo uongo ambao mdanganyaji anautoa ana kwa ana akijua kabisa kuwa anadanganya, na akijaribu kwa kila hali kuuficha uhalisi kwa tabasamu na vicheko na sauti ya upole kama vile anachokizungumza ninkweli kabisa (Lying through your teeth)
  6. Uko uongo ambao huzungumzwa kwa makusudi ya kuepusha mtumwingine hususani mpenzi kuumia moyo (White lie).Wengi huamini kuwa uongo huu unakubalika na kuvumilika, sijui wewe mtazamo wako ukoje.

 

Na: Dr. Chris Mauki

Social, Relationship and Counselling Psychologist

University of  Dar es Salaam

chrismauki57@gmail.com

www.chrismauki.co.tz

 

 Dr. Chris Mauki. An expert in Relationships, Social and Counseling Psychology. Lecturer in Psychology: UDSM. Inspirational & Motivational speaker. Family man


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *