DARASA LA ALHAMISI NA DR. CHRIS MAUKI: JE WEWE NI WA TABIA IPI?

 

 

JE WEWE NI WA TABIA IPI?

 

Watu wowote unaokutana nao katika mzungumko wa maisha kama vile shuleni, katika biashara, safarini, maeneo ya ibada au sehemu nyingine yoyote lazima wataonyesha moja ya aina tatu za tabia. Aina hizi ni; 1. Wale watukutu (wajeuri), 2. Wale wapole, waliotayari kushuka na kukubali  na 3. Wale wabishi na wenye misimamo binafsi.

 

Kama unataka kujua jinsi yakuishi na watu wenye tabia ngumu basi ni lazima ujue aina hizi za tabia ambao zinajumuisha karibu aina za watu wote na pia kufahamu namna ya kupunguza athari zake. Njia moja kubwa na nzuri ya kufanya hili ni wewe mwenyewe kuwa katika kundi la pili la aina za tabia (mpole, unayeweza kukubali na kushuka) bila hivyo itakuwia vigumu. Tuangalie tabia hizi kwa undani na namna ya kuzishuhulikia.

1. Watu watukutu na wajeuri (Aggressive)

Hawa ni watu wapendao kuwa na ubabe hasa katika maneno, wanaweza wakakutoa machozi bila kukupiga bali kupitia maneno yao yaumizayo, yaliyojaa dharau, kashfa na hata matusi. Hufanya hivi kufurahisha roho zao tu na wakati huo huo kuwaumiza wengine mioyo. Watu hawa hufurahia sana hisia za kinguvu na kibabe walizonazo na kufikiri kuwa wanauzezo wa kumpelekesha yeyote yule kufanya lile walipendalo wao wakati wowote.

Kamwe hawawezi kulikubali hili lakini ndani ya mioyo yao wanajua bayana kuwa wanawaonea wale walio dhaifu zaidi ya wao. Mara nyingine hupenda kutumia ubabe na ujeuri wao kuficha uoga wao. Pia hupenda kujinyanyua na kujiona walio juu ili tu kificha woga na hofu zao za moyoni. Ukiwatazama na tabia zao utadhani ni watu wenye nguvu na wanaojiweza kumbe ni waliojaa hofu na woga unafunikwa na tabia zao. Unaweza kukuta mara nyingine kuwa watu wenye tabia hii ni waliopweke kwa sababu mara nyingi tabia zao huwatawanya na kuwakimbiza wale wanaowazunguka katika maisha yao mfano; Katika biashara, mashuleni, makazini au hata marafiki wa kawaida.

Hili hutokea kwasababu pia watu hawa hutumia muda wao mwingine kuwaonyesha wengine kuwa wao ni namba moja, hujifanya wanajua na kuelewa vyote, huwa wapinzani wa yeyote. Wao huamini kabisa kuwa, chochote kinachoenda vibaya au kinachoharibika nikosa la mtu mwingine na sio la kwao, hii huwafariji na kuzidisha kiburi chao, ingawa ndani yao wana kiu ya kuwa na marafiki (company) ila ni ngumu kulikiri hili kwa sababu huogopa kuonekana kuwa wadhaifu.

Watu wenye tabia ya ujeuri na utukutu ni watu wenye nguvu na       nishati nyingi mwilini, kama wangetumia nguvu na nishati waliyonayo katika mambo ya maendeleo basi wangefaidika sana, tatizo hutumia nguvu na nishati yao katika mambo ya uharibifu. Tabia hii inapozidi na kukomaa fujo, ujeuri na kiburi kinachokuwa kwenye maneno ya kinywa huhama kwenda kwenye vita za kimwili mfano kupigana, kuvunja vitu nk. Ingawa watu wenye tabia hizi mara nyingine hawajipendi (hujichukia kwa yale wayafanyayo) ni kweli kwamba watu hawa huwa na athari kwa kila anayewazunguka.

Hata kama umewahi kuumizwa na mtu wa tabia hii ni vema kutambua kuwa lawama na madai mengi ya mtu jeuri, mtukutu na mwenye tabia kama hizi siyo ya kweli na hayana uzito. Haina haja ya kupoteza muda kuzifikiria lawama zao. Hakuna anayependa kusahihishwa, kugombana au kukemewa mbele za watu, hii ndiyo tabia ya watu wajeuri na walio na tabia za kitukutu. Mara nyingine hudhani wanapata sifa. Wako watu wa jinsi hii ambao hawawezi kukugombeza au (kukupa vidonge vyako) mkiwa wawili peke yenu, watangoja watu wengine wawepo ndio waanze kubwabwaja, chakufanya jiepushe nao.

Kwa kule kukimbiwa na marafiki, na kuwa pweke, huongeza tabia za kitukutu na kijeuri na hii huwafanya watu hawa kutambulika haraka na kiurahisi zaidi. Zifuatazo ni Alama zitakazokutambulisha mtu jeuri na mtukutu

 1. a) Alama za kimaneno

Mara kwa mara hupendelea kusema maneno haya vinywani mwao.

Nakwambia bora unge………………”

Wewe sichochote, silolote……………”

Nakwambia, lazima u………….”

Fanya vile ninavyokwambia mimi…………”

Nataka u…………….”

Wewe endelea tu tutaona…………..”

1. Ala za kimwili

Hupendelea kusimama wima

Huwa wenye pozi kavu, ngumu (still and rigid pause)

Hupenda kukunja mikono

Hupenda kupayuka au kupigia wengine kelele

Hupenda kuwanyooshea wengine vidole.

Hupenda kuwazodoa wengine na vidole (hawezi kukuelekeza hadi kidole chake kikusukume)

Hupenda kupiga aukugonga meza na viti akizungumza

 

2. Watu wapole, waliotayari  kukubali kushuka (Submissive)

 Hawa ni watu wanaopenda kujitoa sadaka kwa ajili ya manufaa ya wengine. Kwa hali hii ni rahisi watuhawa kujikuta wanatumiwa vibaya na watu wengine hasa wale wejeuri na watukutu tulio waangalia awali. Mara nyingi watu walio wapole na wanaokubali kushuka hupenda kuwatia moyo wengine wawe kama wao. Katika vizazi vilivyopita, wanawake walitegemewa zaidi kuwa watu wa kundi hili. Ni mabadiliko ya maisha na ya jamii ya leo ambayo yamemfanya hata mwanamke kuwa mjeuri na mshindani tofauti na jamii za awali. Kwa upande mwingine mfumo wa maisha wa vizazi vya nyuma ulimweka chini mwanamke na kuzuia maendeleo yake hasa katika kujiendelezea vipawa alivyonavyo kwa vigezo tu kwamba yeye ni wakukubali chochote na wakati wowote sasa tunayaona mabadiliko kwa kiasi fulani.

Mara kwa mara watu wapole, na waliotayari kushuka wamekuwa wenye hisia za kinyonge na kutengwa, wakijihisi kutokuwa salama wakati mwingi. Kujijali, kujipenda na kujithamini kwa watu hawa sio kwa kudumu, bali kunakuwa na nyakati za kuyumbayumba kutokana na mazingira. Hawa sio watu wenye ujasiri ndani yao wenyewe na hata katika vile wavifanyavyo.

Mara mtu wa kundi hili anapokutana na mtu mjeuri na mtukutu, hofu na ujasiri wake hupungua sana, na anaweza kukubali kupingwa hata kama alikuwa ana haki. Kwa sababu mara nyingi watu wa jinsi hii wanajua kuwa kwa upole wao watu wengi wamekuwa wakiwatumia na kuwachezea, hii imewafanya wawe ni watu wenye vihasira vya mara kwa mara. Hasira hii sio kwa kugombana na watu au wale wanaowaudhi bali huwaka ndani yao wenyewe kwa kule kuiruhusu hali ya kutumiwa visivyo. Ingawa hakuna wanachoweza kukibadilisha katika uhalisi huu, hali hii huwafanya wachanganyikiwe zaidi.

Watu hawa ni wazuri katika kuficha hisia zao, hufanya shuhuli zao za kila siku, kama vile kila kitu kiko sawa ingawa ukweli ni kwamba wanakuwa na hofu, woga, vijihasira vya ndani, ambavyo kujikusanya na mara halipuka (kutokana na mazingira) na kuudhihirisha uhalisi wao. Watu hawa wamekuwa kitoweo cha wale wajeuri na watukutu ambao wanasubiri kumpata mtu dhaifu anayekubali kosa lolote hata lisilolake. Mtu ambaye huamini kila kosa lililofanywa ni la kwake au anahusika kwa namna moja au nyingine.

Mtu wa hivi (aliyempole, tayari kushuka na kukubali) hupenda kujitenga mbali na wengine wa kijihisi kuwa hawastahili kuwa na wengine wenye hali ya juu. Wakidhani kuwa hata hao wengine hawana hoja ya kuwasikiliza wala kuwajua.

Jaribu kumsifia mtu wajinsi hii hata mara moja, kamwe hatopokea sifa hiyo zaidi ya kujibaraguza kwa aibu tu. Au anaweza kuigeuza sifa hiyo kuwa kejeli, kwa sababu tu haamini kuwa anastahili sifa ya aina yeyote. Kwamfano mtu anamwambia; “Napenda alivyovaa, umependeza kweli” badala ya yeye kusema asante. Mtu wa kundi hili atasema. “Ah! kwanza nguo zenyewe zimeshazeeka hizi ”. Kwa sababu ya hali zote zinazomzunguka mtu huyu, amekuwa asiye na ladha na msisimko wa maisha, hana muda wa kujifurahisha mwenyewe badala yake hutumia muda wake wote kufanya yale ambayo wengine wanamhitaji afanye.

Watu wengi huwaonea huruma watu hawa na mara nyingine kujaribu kuwasaidia ili nao wapate kupumzika isipokuwa tu wale wajeuri ambao kamwe hawaoni huruma bali hufurahia hali ya mtu mpole ilivyo. Ni ngumu kidogo kuishi au kufanya kazi na mtu mpole anayependa kushuka na kukubali, maana mara nyingi hujiona asiyefaa, hasa pale anapojutia tabia zake mwenyewe, hali hii huwafanya wengine kuwakwepa isipo kuwa tu katika mazingira ya lazima. Jambo hili huongeza hisia za kutengwa na kuwafanya kuhisi unyonge zaidi.

 

Utamtambuaje mtu huyu?

Alama za maneno

 • Oh jamani…………..”
 • Samahani sana kwa usumbufu lakini………..”
 • Sijui kama waweza kunisaidia…………….”
 • Samahani, samahani sana……………….”
 • Lakini ……… lakini…………

Alama za mwili

 • Hawapendi kukutazama machoni
 • Hupenda kukunja miguu na kushika tama
 • Huzungumza taratibu na pole pole sana.

 

3. Watu wabishi wenye misimamo binafsi

Hawa ni watu wanaojijali wenyewe na kujali haki za wenzao pia.  Katika aina zote tatu za tabia watu wa kundi hili ndio pekee wanaoweza kufikia lengo walilojiwekea. Watu hawa huwaheshimu wengine ingawa huilinda misimamo walinayo ili isiyumbishwe na mtu yeyote, na katika mambo yote wao hutafuta kujua haki iliko. Katika wengi kiu yao huwa ni ushindi kwa hiyo wako tayari kufanya mapatano katika hali iliyo njema siyo ya vurugu kama wale walio wajeuri na watukutu. Kwa sababu wameunganishwa na hisia zao zaidi, ni rahisi wao kuzielezea hisia zao kwa mtu mwingine, hata kama hisia zao ni za kujutia kile walicho kifanya wenyewe.

Mara nyingi husikia amani kwa yale wanayofanya au kuyaamua. Ingawa mara nyingine mambo huwaendela tofauti na walivyopanga, watu hawa hufahamu kuwa hawanabudi kukubali kosa au na kuwa tayari kujifunza kutokana na yale makosa. Mambo yanapowaendea vema hupenda kujisifia na kujiona walio juu. Mara nyingine misimamo yao huwashawishi na kuwavutia wengine watazame kama wao, sio watu wanaopenda kuwatumia wengine vibaya “being manipulative” kama vile kuwasema au kuwasengenya wengine, hii huwafanya kuwa na wafuasi au washabiki wengi zaidi.

Kule kujiamini kwao na kuwa na ujasiri hupunguza sana msongo wa mawazo maishani mwao na hii huwasaidia kuelekeza nishati na nguvu zao zote katika kufikia malengo waliojiwekea. Mara kwa mara sio watu wenye mabadiliko ya hisia (change of attitude) na hii hufanya mahusiano yao na wengine kuwa yasiyoyumba na mawasiliano baina yao na wengine huwa wazi, sio watu wakuficha wanachokiona, uwazi walionao kuwaweka huru. Hujisikia vema hujipenda na kujithamini muda mwingi. Hujijengea hisia za usalama na imani kwa sababu ya mawasiliano bora walionayo na wale wanaowazunguka, hii pia husababishwa na wao kuelewa fika wajibu wao na wajibu wa wengine pia.

Ingawa wanaweza kuwa wabishi, lakini huheshimu misimamo ya   wengine na kupenda ya kwao iheshimiwe pia na hii huwafanya kuwa na ushirika na wale wanaowazunguka. Mara nyingi ni wazuri katika kuwatia wengine moyo kujitahidi zaidi.

 

Alam za kuwatambua.

Alama za maneno

 • Nahisi……. Najisikia ku……………”
 • Ningependa ku…………”
 • Wewe unaonaje hapa/mawazo yako nini…………..”
 • Unadhani njia gani bora kulishuhulikia hili ………..”
 • Nafikiri………..”
 • Hembu tu……………..”

Alama za kimwili

 • Hupenda kuwa wima ila wenye pozi laini (relaxed stance)
 • Huangalia kijasiri na kuangalia usoni (kukodoa macho).
 • Huwa na hisia za upole, kujitawala na kujimiliki wenyewe

Kwa vyovyote vile, mara zote unapokutana na mtu mwenye tabia yeyote kati ya hizi tatu kumbuka una haki ya kufanya yafuatayo;

 1. jifunze kuelezea hisia zako vyema (usiogopoe au kuona aibu kwa kuwa hutokuwa umejitendea haki)
 2. Jifunze kuzielezea hisia zako mbaya au za hasira, kamwe usifunike au kuzika hisia. Mfano, unaweza kumwambia; “Sipendi kabisa unavyokula”
 3. Jifunze kusema hapana, Mfano; “Hapana sitaweza kufika leo”
 4. Toa wazo la kweli, usipake watu mafuta kwa mgongo wa chupa. Mfano;  “Mimi siliafiki hilo jambo hata kidogo”
 5. Kiri kuwa umekasirika, hasa pale ambapo haunabudi kukasirika. Mf. “Kweli umeniudhi sana baada ya kusema hayo maneno”. Usitoe tabasamu la mamba tu, kutabasamu wakati ndani yako unahisi kuungua moto.

 

Dr. Chris Mauki

University of  Dar es Salaam

chrismauki57@gmail.com

www.chrismauki.co.tz

 

 

 

 

 Dr. Chris Mauki. An expert in Relationships, Social and Counseling Psychology. Lecturer in Psychology: UDSM. Inspirational & Motivational speaker. Family man


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *