NYUMA YA PAZIA (BEHIND THE SCENE) SIMULIZI YA KWELI YA MAISHA YA DR. CHRIS MAUKI-SEHEMU YA TANO

NYUMA YA PAZIA (BEHIND THE SCENE)
Simulizi ya Kweli ya Maisha ya Dr. Chriss Mauki

SEHEMU YA 05

Matokeo yanatoka na kwa mshangao wa kila mmoja, nimefanya vizuri. Napata fursa ya kuendelea na kidato cha tano shule ya Malangali Iringa, na ingawa nataka sana kuacha kila kitu kiovu nilichoanza, bado sina hizo nguvu. Huku nakutana na marafiki wapya na angalau wanajielewa zaidi, lakini tayari tabia yangu imeshatengenezwa na vijana niliowapa fursa ya kuitengeneza, miaka kadhaa iliyopita. Nashindwa kuacha pombe na sigala, kwani damu yangu imeshazoea hivyo vitu.

Likizo yangu inafika nami nakusudia kwenda kumsalimu baba yangu mkubwa wilayani Njombe kwa wakati huo. Nikiwa huko nakutana na habari za Yesu. Ni kama sijawahi kuzisikia kabla, na ingawa maisha yangu ya kukulia kwa mchungaji nimekuwa mtu wa kusikia mahubiri mara zote, safari hii yananijia kwa nguvu ya tofauti sana. Nashindwa kustahimili nguvu ya yale mahubiri, ni nguvu kubwa kuliko nguvu ya wale rafiki zangu waliobadili tabia yangu. Hii ni nguvu ya badiliko linaloanzia ndani. Sielewi ni wapi nianzie kurudi kwa Kristo. Nahisi nataka kukimbia sauti ya ushawishi ninayoisikia, lakini inaniita kutoka ndani. “Chris, unamuhitaji Yesu, unamuhitaji Yesu tu.” Nasikia sauti hiyo tena na tena, na ingawa ningetamani kuziba masikio nisiisikie, lakini ninajua inatokea ndani yangu. Siyo sauti ya mawazo yangu, wala ya hisia zangu. Siyo sauti ya yale mahubiri niliyosikiliza, nimekuwa nikisikiliza mahubiri mara kadhaa lakini haikuwahi kutokea hivyo. Nashindwa kuipinga hivyo nakubali kutii. Nanyoosha mikono yangu na kutubu dhambi zangu. Nadhani ni maneno tu ya kufuatisha sala ya toba, na siamini kwamba hiyo sala itanifanya niache sigala na pombe. Ukweli ni kwamba sitaki tena kuendelea kuwa mlevi, sitaki tena kuendelea kuwa mvutaji wa sigala, lakini hakuna namna ninaweza kuacha. “Kama huyu Yesu atanisaidia kuacha sigala na pombe, basi nitamfuata kweli,” ninajisemea moyoni, huku nikimfuatisha anayeniongoza sala ya toba.

Kwa mshangao wangu, sisikii tena hamu ya kuvuta sigala wala kiu ya pombe. Ninafikiri moyoni kuwa huenda itarudi baada ya siku kadhaa, lakini mpaka naondoka kwa baba yangu mkubwa, sina hamu tena. Nawaza labda nikirudi shuleni ningeanza tena, napata hofu kuhisi huenda nitatamani tena sigala na pombe. Nafsi yangu ina kiu ya kushinda hizi dhambi zangu kuu, nami ninajua sina nguvu za kuzishinda. Sielewi kwamba kuna nguvu ndani yangu iliachiliwa pale nilipofanya maamuzi ya kumkubali Kristo. Haikuwa nguvu ya dini wala ya dhehebu, haikuwa nguvu ya mchungaji wala askofu, ni nguvu ya mwana pekee wa Mungu, aliyekuwa tayari kutoa maisha yake ili tu mimi niache dhambi. Nguvu hiyo ya ajabu iliachiliwa kunipa ushindi dhidi ya dhambi, nikagundua nimepata uhuru ambao sikuwahi kuupata maisha yangu yote.

Sikuhitaji tena mzazi ili nisilewe au nisivute sigala. Sikusumbuliwa tena na watu walioniona nimeshindikana. Ndani mwangu nilianza kupata ujasiri juu ya maisha yangu ya wakati huo na ya baadaye. Hofu ya kuwa mwanaume nisiye na thamani yoyote kwenye jamii ilianza kuondoka na hatimaye kuisha kabisa. Nilifanikiwa kupata kanisa lililonilea kwenye misingi ya kumjua Mungu zaidi. Nilianza kujifunza Mungu anasema nini juu ya maisha yangu, nikajifunza ahadi zake kwangu kupitia Neno lake. Furaha yangu ilianza kuongezeka nilipogundua kuwa mimi si hasara tena kwa wazazi na familia yangu. Upeo wangu wa kufikiri nao ukaanza kuongezeka. Ghafla nilianza kujikuta mara kadhaa nikitoa ushauri kwa wenzangu, kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo mahusiano. Mungu aliifunua hii karama kwa watu hata kabla mimi mwenyewe sijaijua, nikaanza kufuatwa na watu niwashauri, hadi watu wazima wenye ndoa.

Ni kweli nina mke mzuri wa muonekano na tabia, na nina watoto wazuri ambao pia ni marafiki zangu wa karibu. Nafasi ya wanangu na mke wangu katika taaluma yangu ni kubwa sana, na kwa kiasi kikubwa wao ndio wamenifanya kufika hapa nilipo. Lakini hakuna ninayeweza kumlinganisha na Yesu katika taaluma na mafanikio yangu yote, yakiwemo mafanikio ya mahusiano niliyonayo. Watu wengi huniuliza siri kubwa ya mafanikio makubwa kitaaluma, na licha ya kuwa nimesomea, na hufanya kile ambacho ni kipaji changu na taaluma yangu wakati huo huo, ila msingi mkuu ni Kristo. Yeye ndiye nyuma ya pazia au behind the scene kwa kila jema linaloonekana kunihusu.

Mungu amenipa neema ya kuchanganya taaluma na imani yangu, na hicho ndicho hunitofautisha na wana saikolojia wengi sana. Tukubali tukatae, kuna mambo ambayo misingi yake ni rohoni, na hata ukutane na mwanasaikolojia wa namna gani, hawezi kukupa suluhisho usipomruhusu Mungu aingilie kati. Kuna wakati nawashauri watu halafu nawambia kwa kitaaluma hapo ndio mwisho, lakini kitakachokutoa hapo ni nguvu ya Mungu, sasa kama uko tayari nikuunganishe na watu watakaokusaidia kiroho.

Nimemuona Mungu akinipa hekima ya kuzungumza na watu, kwani hakuna ajuaye siri za mioyo ya watu zaidi yake Muumbaji. Nimetumia Neno la Mungu kuongeza maarifa yangu katika saikolojia, kwani ndani ya Neno kuna kila kitu. Nimekuwa nikimuomba Roho mtakatifu kabla ya kukutana na wateja wangu, na amenipa uwezo mkubwa wa kusuluhisha matatizo ya watu. Wengi hudhani ni uzoefu na kusomea, lakini nina hakika, iwe ninayezungumza naye ni mkristo au muislamu, muamini au mpagani, Roho mtakatifu huwa msaada mkubwa sana kwangu katika kuwashauri na kutatua matatizo ya watu.”

Tulimaliza mazungumzo yetu nafsi yangu ikiwa imeridhika kabisa, huku nikitamani niiandike na kuirusha simulizi hii haraka niwezavyo. Ni matumaini yangu itawafikia na kuwafaa wengi sana, na ninatoa shukurani za kipekee kwa Dr. Chris Mauki kuniamini na kukubali wazo langu hili.

Kwa simulizi nyingine nyingi za kweli, imeandikwa na dada Grace Rweyemamu, fuatilia page yake ya Facebook: Grace Godfrey Rweyemam

#BasedOnTrueStory
#Mwandishi: Grace.G.R #Whatsapp+255714460102

 

MWISHO…….

 Dr. Chris Mauki. An expert in Relationships, Social and Counseling Psychology. Lecturer in Psychology: UDSM. Inspirational & Motivational speaker. Family man


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *