NYUMA YA PAZIA (BEHIND THE SCENE) SIMULIZI YA KWELI YA MAISHA YA DR. CHRIS MAUKI-SEHEMU YA NNE

NYUMA YA PAZIA (BEHIND THE SCENE)
Simulizi ya Kweli ya Maisha ya Dr. Chriss Mauki

SEHEMU YA 04

Akizungumza kuhusu taaluma yake, maswali kadhaa yaliendelea kichwani mwangu. Ni kweli, ni mara chache sana mtu kufanikiwa katika eneo la kutoa ushauri kama ambavyo imekuwa kwa Chris. Kusema kwamba akiwa kidato cha sita tu alianza kuaminika kwa utatuzi wa kesi kubwa kubwa, kulinifanya nihisi kuwa pengine maisha yake yalikuwa yamenyooka sana tangu utoto. Ila nikakumbuka kuwa aliwahi kusema alishindikana kwa wazazi, na sasa swali likawa ni namna gani kijana aliyeshindikana kwa wazazi ghafla akabadilika na kuwa mshauri wa kuaminika kiasi hicho, tena katika umri mdogo.

“Ninaingia kidato cha kwanza na kukutana na vijana waliochangamka akili na tabia, kuliko ambao niliwahi kukutana nao wakati wowote wa maisha yangu. Napata marafiki kadhaa, na najiona niko tofauti. Huenda utofauti wangu ni mzuri, na ingekuwa vema ningewaambukiza wenzangu, lakini nguvu ya tabia zao inakuwa kubwa kuniliko, na hivyo najikuta ninavutwa. Naonekana mshamba na muoga, wengine wananicheka mara kadhaa ninapokataa kujiunga nao, nami taratibu naanza kuwafuata ili kuepuka aibu. Nasahau kule nilikotoka na malezi ya wazazi wangu. Ninapiga hatua kuelekea tabia za wenzangu. Mwanzoni nahisi hofu, lakini nguvu ya ushawishi inakuwa kubwa kuliko nguvu ya hofu, hivyo naendelea mbele. Mara kadhaa nasikia sauti ya mama ndani mwangu ikinipigia kelele masikioni mwangu, inanikosesha raha kwa muda, ila naipuuza nimuonapo mwenzangu akishika sigala na kuivuta kwa madaha. Kichwani naona sura ya baba ikinihubiria juu ya dhambi, nafsini nachomwa na yale mahubiri, ila pia napuuza nionapo wenzangu wanayafurahia maisha zaidi yangu. Niko katikati ya machaguo hayo, kuwa kijana mzuri na kubadili wanaonizunguka, au kuwafuata wao. Sina nguvu ya kujitenga nao kabisa, najipa moyo kwamba huenda nitaweza kuwabadili taratibu, lakini miezi michache mbele nagundua hata sikuwapa fursa kujua kwamba mimi ni mtoto wa mchungaji, na nimelelewa maisha ya kikristo.

Nashika sigala kwa mara ya kwanza, moyo wangu unaenda mbio sana, lakini rafiki yangu pembeni ananihimiza, “vuta, haina shida.” Ninaanza kuvuta na kukohoa sana, ananitia moyo kwamba nitazoea taratibu. Nikiwa peke yangu najiuliza na kujilaumu kwanini nilivuta, lakini kesho yake tena nashawishiwa na kuwasha nyingine. Hii ya pili inakuwa rahisi zaidi kuimaliza kuliko ile ya jana, na sikohoi sana kama jana. Baada ya wiki nagundua nimeanza kuwa mzoefu, na sasa naanza kuhisi utofauti ninapovuta. Siruhusu kujilaumu tena niwapo peke yangu, na nikiona nina lawama ndani mwangu basi nitatafuta wenzangu, nisijipe nafasi ya kujutia chochote ninachokifanya. Tunatoroka shule mara kadhaa na kwenda kwenye starehe. Sigala na pombe ndio yanakuwa maisha yetu.

Napata marafiki wengine, wananishawishi kujaribu kidogo, lakini ninakataa kwani niliwahi kusikia bangi ni hatari kwa akili. Siku baada ya siku nguvu yao ya ushawishi inaongezeka, naona wakifurahia sana wanapovuta bangi. Inatokea siku moja nimefanya vibaya darasani, hivyo napata msongo mawazo sana. Mwenzangu ananishangaa inakuaje kufeli tu kunaniwazisha kiasi hicho, kikawaida mimi si mtu ninayestahimili kufeli kirahisi, lakini wenzangu wote hawanielewi. Rafiki ananishawishi kwa mara nyingine nivute bangi, akinihakikishia kuwa itaniondolea msongo wa mawazo na kunipa furaha. Hiyo inakuwa hatua nyingine kubwa ya uharibifu wa maisha yangu, na sasa sioni kitu kizuri maishani kushinda bangi.

Taarifa zinawafikia wazazi juu ya tabia zangu mbaya, baba anaumia kupata hasara ya uzao. “Ni heri usingekuwa kijana wa kwanza, labda ungejifunza kwa wakubwa zako. Lakini sasa unadhani wadogo zako watajifunza nini?” anazungumza mama yangu kwa uchungu. Maneno yake yananiingia sana, lakini zile tabia zimeshakuwa kama minyororo iliyonifunga miguu na mikono, na kamwe siwezi kuacha. Nimemaliza kidato cha nne, na sasa siko tena na marafiki zangu walionisababisha kuwa mlevi, mvutaji na kijana mchafu. Kile walichoweka kwenye maisha yangu hakiwezekani kuondoka, na hata kama wako mbali kiasi gani, vifungo vya tabia walizonifundisha siwezi kujifungua. Kuna wakati nasikia uchungu na kutamani kubadilika, ila kila ninapowaza kufanya hivyo, najikuta nikitoroka na kutafuta sigala initulize. Hakuna anayedhani nitafanikiwa japo kufaulu kidogo kuendelea na kidato cha tano na sita, wazazi na ndugu wamenikatia tamaa. Natumika kama mfano mbaya kwa majirani na hata kwa wadogo zangu, kijana aliyeharibika asiyefaa kuigwa kwa lolote. “Utaishia kuwa kama Chris” inakuwa sentensi ya kutoa onyo kwa watoto.

Nawaza kama ningepata fursa ya kurudi nyuma miaka minne, nisingechagua njia ya maisha niliyoichagua, lakini nilipofika hakuna wa kunirudisha kuanza upya tena. Najifananisha na ndoo ya maji baridi iliyomwagwa ndani ya bahari, hakuna namna ambayo mtu huweza tena kuitoa ile ndoo. Maneno ya watu yananifanya nijione kijana nisiye na faida, nahisi kwamba nitakuwa mwanaume asiyestahili hata kuwa na mke. Nafikiri ni namna gani nitaweza kubadili kile ambacho watu wanaamini kuhusu mimi. Kichwani linanijia wazo la kupanda mlima Kilimanjaro, naliona ni wazo jema kwani nimeshasikia kuna watu kadhaa waliwahi kujaribu hawakuweza kufika kileleni. Nawaza kuwa nikifanikiwa kupanda, na kufika kileleni, katika umri nilionao, basi nitaonekana walau kuna jambo nimelifanikisha katika maisha. Huenda hii ikawa fursa ya kuwaaminisha watu kuwa si kijana nisiyefaa kwa lolote.
Ninatafuta njia na kufanikiwa kupanda mlima Kilimanjaro, mpaka kufika kileleni. Uzoefu huo unafanya akili yangu iamini kuwa kumbe ninaweza kufanya yale ambayo huonekana ni magumu. Nawaza juu ya jambo gumu sana ambalo siku zote nimetamani nilishinde, lakini sikuweza, na sasa ninafanya maamuzi kuwa kama nimefanikiwa kupanda mlima Kilimanjaro na kufika kileleni, basi nitafanikiwa kuacha bangi. Kwa miaka kadhaa niliyovuta bangi nimekuwa mtu wa majuto, nimepata furaha ya muda mfupi lakini matokeo yamekuwa kama adhabu. Ninafanikiwa kuacha bangi mara tu baada ya kushuka kutoka mlima Kilimanjaro.

Kwa simulizi nyingine nyingi za kweli, imeandikwa na dada Grace Rweyemamu, fuatilia page yake ya Facebook: Grace Godfrey Rweyemam

#BasedOnTrueStory
#Mwandishi: Grace.G.R #Whatsapp+255714460102Dr. Chris Mauki. An expert in Relationships, Social and Counseling Psychology. Lecturer in Psychology: UDSM. Inspirational & Motivational speaker. Family man


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *