NYUMA YA PAZIA (BEHIND THE SCENE) SIMULIZI YA KWELI YA MAISHA YA DR. CHRIS MAUKI- SEHEMU YA TATU

NYUMA YA PAZIA (BEHIND THE SCENE)
Simulizi ya Kweli ya Maisha ya Dr. Chriss Mauki

SEHEMU YA 03

Jinsi nilivyozidi kumfahamu Miriam, hata kabla hatujaoana, nilijua kwamba huyu mwanamke ameustahili moyo wangu wote. Unajua imeonekana kawaida kwa wanaume kutoka nje ya ndoa, mara nyingine hata wale usiodhani, mimi ni mshauri wa ndoa nafahamu. Lakini asikudanganye mtu, kutoka nje ya ndoa ni maamuzi kuliko udhaifu wa mwili. Sikatai kuwa wanaume huwa na tamaa ya macho, hata kama ana mwanamke mrembo kuliko wote duniani amemuweka ndani. Lakini kama ingekuwa kinachomsukuma mtu kutoka nje ya ndoa ni udhaifu wa mwili na tamaa ya macho, basi watu wangeweza kuzini hata na wanawake mia au zaidi.

Nilikusudia kuwa nitakuwa mwaminifu kwa Miriam, baada ya kuona kuwa hiyo ndiyo zawadi pekee ninayoweza kumpa. Labda haingekuwa rahisi kama si aina ya maisha ambayo kama wanandoa tuliamua kuyaishi. Mke wangu kwangu ni rafiki, kuliko rafiki yeyote yule niliyenaye. Hakuna siri kati yetu na mapenzi yetu hayachagui siku wala saa. Kuna wakati hukwazana, kama ilivyo kwa kila ndoa, lakini kwetu haiwezi kuanza siku tukiwa na makwazo ndani yetu. Tuliweka sheria kwamba hatutalala na makwazo, na ingawa kuna wakati imetuwia vigumu, lakini huo umekuwa msingi mkubwa wa penzi letu. Wengi hutuona na kututamania, na wengine huhisi ni mapenzi ya kujionyesha mitandaoni na kwa watu tu na siyo halisi, lakini kuna kitu kimoja ningemuhakikishia kila mwanandoa, kwamba ndoa nzuri zipo, lakini hazitokei hewani bali hufanyiwa kazi. Ukiona mtu yeyote, ndoa yake ikakuvutia, na ukachunguza ukajua kuwa ni kweli ana ndoa inayofaa kujifunza kwayo fuatilia vizuri, utagundua wanandoa hao walifanya kazi kuwa na ndoa ya namna hiyo. Hakuna mwanadamu asiyebadilika, na hakuna mtu aoaye malaika au shetani. Maadamu uliyeoana naye ni binadamu, basi jua inawezekana kabisa kuwa na ndoa nzuri sana, ya kawaida au mbaya sana, kutokana tu na nini mtakachochagua.”

Akiongea kuhusu mahusiano yake, niliwaza kuwa alichokisema ni kweli kabisa. Watu wengi hawaamini sana juu ya ndoa ambazo kila siku ni Jumapili, yaani yale mapenzi ya muda wote matamu. Huenda ni chache, lakini zipo, na hasa hutegemea na misingi. Wakati mwingine siyo kwamba huwa hivyo mwanzoni, lakini muda unavyoendelea, na namna mbavyo wanandoa hao huijenga misingi yao, inafika kipindi ambacho naweza kusema ni cha mvua zisizokatika. Chris na mke wake wamejitahidi kuwa na ndoa ya mfano, ila nikawa nikijiuliza ni namna gani mwanaume kama Chris huweza kuwa mwaminifu kwa mke wake.

Kwa kipindi nilichomfahamu, ninaweza kusema ni mtu anayezungumza na watu vizuri sana. Ninaamini kwa kiasi kikubwa kuwa si kwangu tu, na wala si kwa wateja wake tu, bali ni haiba yake. Mauki ana haiba ya kuzungumza na watu kwa lugha nzuri. Ingawa nimemfahamu akiwa tayari mtu maarufu, na ambaye huingiza pesa nyingi kwa kutumia muda wake, yaani kwa kuzungumza tu na watu, ila sijawahi kuona dalili yoyote ya maringo kwake. Hata siku moja, hapuuzi ujumbe unaoweza kumtumia kwenye simu, endapo ni wa muhimu kujibiwa, lakini pia kuna mara kadhaa aliniruhusu nimuone na kutumia muda wake bila kuulipia, muda ambao kimsingi ndio biashara yake. Hizo ni baadhi ya tabia ambazo binafsi zilinivutia kwake, nikahisi ni mtu ambaye pengine watu wenye majina makubwa wangepaswa kujifunza kutoka kwake. Yeye huthamini kila mtu, bila kujali daraja au cheo chake.

Niliwaza kwamba mtu kama huyo ni rahisi sana wasichana kujilengesha kwake, wakihisi kuwa huweza kuuteka moyo wake kwa urahisi. Ni kweli, hiyo ndiyo changamoto kubwa aliyoniambia hukutana nayo, hasa katika taaluma yake kama mwana saikolojia na mshauri wa mahusiano na ndoa. “Ninashughulika na hisia za wateja wangu, walioumizwa katika mahusiano au ndoa zao. Wengi ninawasaidia kuendelea mbele, na kufanya maamuzi sahihi, lakini kuna ambao katika kuumizwa hudhani kwamba ninaweza kuchukua nafasi ya wapenzi wao. Hiyo imekuwa changamoto kubwa sana kwangu. Watu wanashindwa kuelewa kuwa hii kwangu ni kazi. Ni sawa kabisa na kumuhukumu daktari wa wanawake kwa sababu hupata fursa ya kuona maumbile ya ndani ya mwanamke. Daktari mwenye taaluma hiyo na aliye makini na kazi yake, hata siku moja havutiwi na mwanamke eti kwa sababu ameona maziwa yake, au sehemu kadhaa za mwili wake. Kuzungumza kwangu na watu au wateja wangu ni sehemu ya taaluma yangu, na hata namna ninavyowachangamkia wateja, na hiyo haitakiwi kutafsiriwa kama huenda ninawatamani au wananivutia. Huwezi amini, kuna wanawake wengine huthubutu kulipia kipindi kama wateja na kumbe lengo lao ni kunitaka kimapenzi. Kikawaida ninachofanya huwa ni kumsoma mtu anataka nini haswa, halafu naenda naye sawa sawa. Sitaki kupoteza wateja, lakini usafi wangu ni muhimu sana kuliko wateja, nadhani unanielewa.

Kama nisingekuwa makini nadhani kazi yangu ingeweza kunivunjia ndoa, ila nilihakikisha namjengea Miriam kuniamini sana tangu mapema. Unajua hii kazi kwangu siyo tu taaluma, bali zaidi sana ni karama au kipaji, kwani sijaianza baada ya kusomea saikolojia. Nikiwa sekondari ilitokea tu watu wakaanza kuniletea masuala yao binafsi, yakiwemo ya kimahusiano, na kunitaka ushauri. Unajua kuna wakati huwezi kujua kama una kipaji fulani, lakini watu walio karibu nawe wanakujua. Nakumbuka nikiwa kidato cha sita, niliwahi mpaka kuwa naletewa kesi za ndoa nisuluhishe. Nikaanza kuona kwamba huenda nina kitu cha kipekee ndani mwangu. Si kwamba nilikuwa nimekomaa kwenye mahusiano, au nina uzoefu mwingi, lakini nina uhakika ni kipaji ambacho Mungu aliweka ndani mwangu.

Sasa hii imejingea kuaminika sana na watu wengi, kiasi kwamba kuna wakati inakuwa changamoto tena. Ninaendelea kukua na natamani kama ningeifanya hii kazi na watu, sababu unajua ili uongezeke kiuchumi, ni vema na lazima ukubali kufanya kazi na watu na sio peke yako. Lakini ugumu unakuja kwa kazi kama yangu, watu hawako tayari kumuamini mtu mwingine endapo wanataka kuzungumza na mimi. Kuna wakati ninaweza nikawa nje ya nchi na mtu akawa tayari kusubiri hata miezi miwili, mitatu au zaidi, mradi tu azungumze na mimi binafsi. Wengine najaribu kuwaunganisha na wanasaikolojia wengine, lakini hawataki. Naelewa kwangu hayo ni mafanikio, lakini upande mwingine ni changamoto kubwa. Nasema ni mafanikio sababu jambo la msingi sana katika taaluma yangu ni kuaminika na watu. Ukifanikiwa kupata imani ya mteja, ni rahisi sana kumsaidia, na siku zote lengo langu la msingi si kupata wateja wengi na kutengeneza pesa nyingi, bali kuaminika na kumsaidia kila anayeamua kuja kuniona.”

Kwa simulizi nyingine nyingi za kweli, imeandikwa na dada Grace Rweyemamu, fuatilia page yake ya Facebook: Grace Godfrey Rweyemam

#BasedOnTrueStory
#Mwandishi: Grace.G.R #Whatsapp+255714460102

 

ITAENDELEA…..Dr. Chris Mauki. An expert in Relationships, Social and Counseling Psychology. Lecturer in Psychology: UDSM. Inspirational & Motivational speaker. Family man


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *