NYUMA YA PAZIA (BEHIND THE SCENE) SIMULIZI YA KWELI YA MAISHA YA DR. CHRIS MAUKI: SEHEMU YA PILI

SEHEMU YA 02

“Kuna vitu huwa naamini hupangwa na Mungu, na hatuwezi kuvipangua hata iweje. Ingawa kuna wakati tunasababisha mioyo ya watu kuumia, na labda tunawasabishia watu majuto na makovu yasiyotibika, lakini hatuwezi kuishi na lawama mioyoni kwa ajili ya mambo ambayo ni lazima yangetokea. Pia kuna maamuzi ambayo wakati mwingine tunalazimika kuyafanya, ingawa yanaweza kuwa na matokeo si mazuri sana kwa wengine. Nilijiwekea hilo tangu nilipojitambua, na kuna gharama ilibidi nilipe, ikibidi kuumiza moyo wa mtu, huku nikilinganisha faida na hasara.

Niliwahi kuwa na mahusiano na binti ambaye awali nilihisi ndiye chaguo sahihi kwangu. Tulipendana na huyo msichana na sidhani kama kuna mtu aliyetufahamu ambaye hakufahamu mahusiano yetu. Tulikaa kwenye mahusiano kwa miaka tisa na yule binti, nitampa jina la Joyce, na kila mtu mpaka wazazi waliamini kwamba tungeoana. Sikuwa nimewahi kufikiri kumuacha Joyce, kwani licha ya kuwa nilimpenda, alikuwa msichana wangu wa kwanza. Mwanzo wa mahusiano yetu ulikuwa mzuri sana, lakini baadaye nilianza kuona vitabia ambavyo nadhani taratibu vilianza kuondoa upendo ndani mwangu. Nilianza kumtarajia awe mshauri wangu na mtu wa kunisaidia kwa malengo, unajua mwanaume anayetaka kuoa anategemea tabia fulani fulani kwa mwanamke. Nilianza kuhisi ni mwanamke ambaye nikiwa naye, sitafika pale ambapo ningetamani kufika.

Nilipoanza kujitambua, nilijua kuwa maisha yangu ya mbele yangechangiwa sana kuwa vyovyote yatakavyokuwa na mwanamke nitakayemuoa, hivyo sikutaka kuoa sababu tu huyo binti nimemzoea au ananivutia, nilihitaji mke atakayebeba maono niliyonayo. Nilihitaji mwanamke atakayekuwa na upeo wa kufikiri zaidi kuhusu maisha na maendeleo, na siyo tu chakula cha kupika na mavazi. Na labda huu uwe ushauri wangu kwa mabinti, hasa wanaotafuta kuolewa, au vijana wanaotafuta kuoa. Ndoa siyo kufurahia tendo la ndoa tu, ni maisha, maisha ya kudumu. Unapofikiri kuwa na mwenzi, vema ukafikiri kuishi na yule ambaye unadhani atakufaa, mtaenda pamoja na kufikia ndoto na malengo yenu.

Nilimuacha huyo msichana, na nina hakika nilimuumiza sana, lakini sikuwa na namna mbali na kushikilia msimamo wangu. Kwa miaka tisa tuliyokuwa naye nilijua si mtu wa kubadilika, au ninaweza kusema hakuwa sahihi kwa maono yangu. Nilijaribu kumuacha isivyo kikatili, kwani sikuwa namchukia, na kwa kadiri nilivyoweza nilitafuta amani naye, akanitangazia kunisamehe, ila hakuweza tena kuingia kwenye mahusiano mengine na mpaka hii leo hajaolewa. Kuna kipindi nilikaa na kuwaza juu yake, kwamba huenda nilifanya makosa kuachana naye, lakini nafsi yangu ilikataa kumrudia. Kila nilipofikiri kuwa naye kama mke, sikuona kama ni mtu ambaye ningemuhitaji. Hapo nikawaza kuwa ilikuwa bora nimuumize kwa kumuacha kuliko kuwa na ndoa mbayo ni mwiba kwangu na kwake pia. Na nadhani sikuona usahihi hasa wa maamuzi niliyoyafanya wakati huo mpaka nilipokutana na kuoana na mke wangu Miriam Lukindo Mauki.

Kwa miaka zaidi ya kumi ya ndoa yangu na Miriam, nimegundua kuwa nafasi ya mwanamke katika mafanikio ni kubwa kuliko ambavyo nilidhani hapo awali. Sasa ninagundua kuwa ilikuwa mpango wa Mungu nimuache Joyce, pia ilikuwa mpango wa Mungu hata msichana niliyekuwa naye baada ya Joyce aniache, ili kumpa nafasi Miriam. Baada ya Joyce, nilikutana na binti mwingine ambaye hatukudumu kwa muda mrefu kwenye mahusiano. Sikuwa mwanaume ambaye ninataka msichana ili kuwa naye tu kwa muda, bila malengo. Wakati huo akili yangu iliwaza kuwa na mtu ambaye atakuwa mke wangu na si vinginevyo. Sikuwa na muda wa kupoteza kwa mwanamke, na tangu mwanzo nilijiweka wazi. Maisha niliyopitia nyuma yalikuwa yametosha, na sikuhitaji tena kuishi maisha yasiyo na muelekeo.

Yule binti kwa bahati mbaya alikuwa ana majeraha ya kuumizwa na mwanaume, na yeye kuwa na mimi haikuwa kwa ajili ya ndoa au mahusiano yenye kesho, bali kwa kuufariji moyo wake tu. Namshukuru kwamba alikuwa muwazi kwangu, baada ya kuona kwamba mimi ni mtu niliyemaanisha, mwenye malengo na ninayeangalia zaidi mbele ninapomtazama kama mwanamke, hivyo alikiri kwamba hakuwa akinistahili, akataka tuachane. Niliumia, ila haikunichukua muda kumsahau na maisha yangu yakasonga.

Miaka ya 2000 mwanzoni, nilikutana na Miriam. Nakumbuka kwa mara ya kwanza kabisa namuona, akiwa ni muimbaji wa nyimbo za injili, nilipenda sana uimbaji wake. Sauti yake ilinivutia, nikatamani tu ningepata fursa ya kuwa naye karibu. Sitaeleza kiundani, lakini nilifanikiwa kuwa rafiki wa Miriam na hatimaye tukaanza mahusiano. Sitakuwa sahihi nikisema kuwa huyu mwanamke ni mkamilifu, lakini nina hakika kwa asilimia mia moja ni mwanamke sahihi sana kwangu. Leo hii ningepewa nafasi ya kuoa tena, kwa uhalali kabisa, mwanamke mwingine, bado chaguo langu angekuwa huyu huyu mrembo wangu. Miriam amenifanya nijitambue kuwa mimi si mtu wa kawaida, kwa kuniongezea ujasiri wa kila ambacho hukifanya. Watu wana kawaida ya kusema ukiona mwanaume amefanikiwa, basi kuna mwanamke nyuma yake. Sijui kwa kiasi gani huo msemo una ukweli, lakini kwangu mimi, kumuoa Miriam kumekuwa na mchango wa dhahiri na mkubwa sana kwenye mafanikio yangu, hasa ya kitaaluma na kiuchumi. Unajua hata dunia nzima iwe inakuheshimu, kama mkeo nyumbani anakudharau na kukutamkia maneno mabaya, kamwe huwezi kujenga kujiamini. Mke wangu amenijengea kujiamini kwa kiasi kikubwa sana. Lakini pia ni mwanamke aliyejimilikisha ndoto zangu na maono yangu. Hakuna hatua ya mafanikio yangu ambayo Miriam hahusiki, na ninaweza kusema yeye ndiye hasa amenifundisha nini maana ya kuwa mwili mmoja. Ujasiri nilionao kuzungumza juu ya mahusiano na ndoa, ni kwa sababu mke wangu husimama kwenye nafasi yake kama mke.

Kwa simulizi nyingine nyingi za kweli, imeandikwa na dada Grace Rweyemamu, fuatilia page yake ya Facebook: Grace Godfrey Rweyemam

#BasedOnTrueStory
#Mwandishi: Grace.G.R #Whatsapp+255714460102

 

ITAENDELEA…..Dr. Chris Mauki. An expert in Relationships, Social and Counseling Psychology. Lecturer in Psychology: UDSM. Inspirational & Motivational speaker. Family man


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *