DARASA LA ALHAMISI NA DR. CHRIS MAUKI: SIMULIZI YA KWELI YA MAISHA YA DR. CHRIS MAUKI-PART ONE: 29.03.2018

 

NYUMA YA PAZIA (BEHIND THE SCENE)

Simulizi ya Kweli ya Maisha ya Dr.  Chris Mauki

SEHEMU YA 01

“Tumchukue Chris bwana.”
“Hapana, Chris kila sherehe, safari hii tujaribu MC mwingine.”

Baada ya kubishana kwa muda waliamua kumchukua, ikawa mara yangu ya kwanza kabisa kumuona, akisherehesha sherehe ya kumuaga binti wa rafiki yake mama wa karibu ambaye amekuwa kama mama yetu mdogo. Nilivutiwa tu na namna alivyokuwa akiendesha sherehe ile, ikaisha salama tukaondoka. Siku ya siku nilihudhuria tukio fulani la vijana, kwa mara nyingine nikamkuta akiwa mmoja wa waongeaji. Hapo nilipata fursa ya kumsikiliza kwa muda mrefu zaidi, nikahisi kitu cha tofauti sana katika uzungumzaji wake. Ni mtu aliyeongea kwa kujiamini, na alionekana anajua vitu vingi sana. Alizungumza kwa muda zaidi kuliko wazungumzaji wengine, lakini mpaka anamaliza tulitamani kuendelea kumsikiliza. Nilihamasika kuanza kumfuatilia, nikiamini ni mtu ninayeweza kujifunza mambo kadha wa kadha kutoka kwake, nikawa nikimfuatilia mitandaoni na kwa bahati nikawahi tena kukutana naye katika matukio kadhaa.

Kipindi fulani nilianza biashara ya chakula, nikawa nikipika na kuuza vyakula kwa wafanyakazi. Nilifanikiwa kupata ofisi kadhaa za kupeleka vyakula, lakini shangazi yetu mmoja akanishauri nimtafute Chris Mauki na huenda akanisaidia kwa ushauri na kupanua soko langu. Nilipopata namba yake na kumpigia, nilishangaa kuona muitikio wake ukiwa chanya na wa ukarimu. Alinipa nafasi ya kuonana naye, na nakumbuka siku hiyo akiwa ofisini kwake chuo kikuu cha Dar es Salaam, nilipofika na vipeperushi vyangu, alinitembeza ofisi kadhaa huku akiwaeleza watu kuhusu biashara yangu na kunitafutia soko kana kwamba ni mdogo wake au rafiki wa karibu. Nilianza kupeleka chakula mimi mwenyewe pale chuo, huku nikiacha wafanyakazi wangu wapeleke hizo ofisi nyingine. Yeye alikuwa mmoja wa wateja wangu kwa kila siku ambayo angekuepo ofisini kwake, na nikapata na wateja wengine wa kudumu. Nilifanya biashara hiyo kwa miezi kadhaa, kabla ya kuanza masomo yangu, ambapo sikuweza tena kuendelea baada ya kuanza kusoma badala yake nikawa nikipika kwa sherehe au matukio tu.

Baada ya kuumwa na kufanyiwa upasuaji, nikiwa ninaanza kupona, nilimtafuta tena Chris, ambaye hata namba yake sikuwa nayo tena. Wakati huu nilimtafuta kwa ajili ya masuala ya kitaaluma zaidi. Nikaanza kumfahamu kama mtu asiye na maringo, mchangamfu na ambaye hukunjua mikono yake kutoa msaada kwa kadiri anavyoweza. Ingawa muda kwake ndio biashara yake, na una thamani sawa kabisa na pesa, lakini alikuwa tayari kunipa muda ilhali akijua kabisa kuwa simuingizii faida yoyote kifedha. Hapo nilianza kuona huyu ni mtu wa tofauti pengine na watu wengi ambao huonekana kuwa na umaarufu fulani. Muitikio ambao hutoa kwa watu ni tofauti na watu wengi wenye majina makubwa mitandaoni na kwenye jamii kwa ujumla. Alialikwa mara kadhaa kanisani kwetu kufundisha, na mara zote ambazo nilimfuata kumsalimia, alinichangamkia kana kwamba tunafahamiana kwa ukaribu.

Kwa nasibu, mwaka juzi au mwaka jana mwanzoni kama sikosei, Mauki alihamia kanisa ambalo tunasali. Mara kadhaa akawa akipewa fursa kuzungumza kanisani, na nakumbuka kuna kipindi alipewa kufundisha shule ya jumapili kwa muda wa wiki nne mfululizo juu ya somo la msamaha. Kwangu hiyo ilikuwa fursa ya pekee na nisingeacha kuhudhuria. Mambo aliyofundisha yangenigharimu kiasi kingi cha pesa kuyapata, lakini hatukuhitajika kuchangia hata shilingi, muda wote huo, na bado mwisho tulipewa vyeti kama wakufunzi. Tukiwa kwenye hilo darasa, kuna siku akizungumza juu ya jinsi gani Mungu husamehe hata wale wasiostahili kusamehewa, Chris alitoa mfano wa maisha yake binafsi jinsi ambavyo Yesu alimtoa kwenye tope la tabia zilizoshindikana hata kwa wazazi wake waliokuwa wameokoka na ni wachungaji. Hakueleza kiundani, ila hiyo sentensi ilinifanya nitamani kujua zaidi kuhusu maisha yake. Ninafahamu vijana wengi ambao tabia zimekuwa vikwazo vikubwa vya kufikia malengo yao, na nilihisi wangepata mfano hai toka kwa mtu aliyefanikiwa kama Mauki, huenda wangesaidika.

Nikiwa nimeanza kuandika simulizi zangu za kweli fesibuku, niliwaza kama ninaweza kupata fursa ya kuandika simulizi ya Mauki, nikamtafuta na kumpa wazo langu hilo. Nilitamani tuzungumze juu ya maeneo mawili ya msingi, ambayo binafsi nilihisi yangefaa sana kuwafikia na kuwasaidia watu wengi. “Kama mshauri wa saikolojia, wengi huweza kujifunza zaidi kutoka kwenye uhalisia wa maisha yake kuliko hata ushauri anaotoa,” niliwaza. “Ikiwa atakubali niandike kiundani kuhusu mahusiano yake ya mapenzi, na taaluma yake, nadhani itawafaidia jamii kubwa sana.” Kukubaliana na wazo langu hilo kwangu ilikuwa fursa nzuri sana, na kama ambavyo binafsi nimejifunza mambo ya msingi kupitia simulizi ya kweli ya maisha ya Dr. Chris Mauki, ningependa iwafikie watu wengi iwezekanavyo, kwani nina hakika kuna mambo ya msingi ya kumfaa kila atakayesoma.

Kwa simulizi nyingine nyingi za kweli, imeandikwa na dada Grace Rweyemamu, fuatilia page yake ya Facebook: Grace Godfrey Rweyemam

#BasedOnTrueStory
#Mwandishi: Grace.G.R #Whatsapp+255714460102

 Dr. Chris Mauki. An expert in Relationships, Social and Counseling Psychology. Lecturer in Psychology: UDSM. Inspirational & Motivational speaker. Family man


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *