DARASA LA ALHAMISI NA DR. CHRIS MAUKI: JENGA TABIA YA KUJUA KUWASILIANA KULIKO BORA

 

JENGA TABIA YA KUJUA KUWASILIANA KULIKO BORA

Ni ukweli usiopingika kwamba hakuna aliyezaliwa anajua kuwasiliana, wote hatunabudi kujifunza namna bora za kuwasiliana ili kuboresha mahusiano na maisha yetu ya kila siku. Yamkini unaweza kujiuliza kwanini wengi wetu ni wabovu sana kwenye mawasiliano? Ukweli ni kwamba hatujafundishwa mbinu bora za kuwasiliana, mifumo yetu ya elimu au mafundisho ya awali hayatuandai kujua jinsi bora ya kuwasiliana. Jambo la pili ni kwamba bado wengi wetu tumekuwa vipofu kuhusu suala zima la kutamani kuwa wawasilianaji wazuri, hatujajiruhusu wenyewe kujua mbinu bora za mawasiliano. Hapa namaanisha kwamba ili kuwa mtu unayejua namna ya kuwasiliana kuliko bora inabidi uamue kwa nia thabiti, haikutokei tu gafla. Kama kweli unataka kuona mabadiliko katika maisha yako ya mawasiliano na watu wanaokuzunguka basi amua kubadilika, amua kuweka jitihada katika kuwa muwasilianaji aliye bora “an effective communicator”.

 Hapa nataka kukupa baadhi ya faida chache utakazo zipata ukishajua mbinu bora za kuwasiliana, kiujumla ni kwamba, ukiwa mtu mwenye kuwasiliana vema utavuna faida tele zisizo na kipimo.

 • Kwanza kujua kuwasiliana kunarahisisha maisha yako
 • Kujua kuwasiliana kuliko bora kunakutengenezea mazingira bora ya kujulikana na kukukutanisha na wengi, kwa lugha nyingine kunapanua wigo wako wa kujuana na wengi “it creates and expand your networks”.
 • Kujua kuwasiliana kunakuwezesha kufikisha ujumbe kwa mlengwa au walengwa pasipo tatizo lolote na kwa kueleweka vema
 • Unapojua kuwasiliana kuliko bora unauhakika wa kupata matokeo yaliyo bora katika kila unalolifanya
 • Kujua kuwasiliana kuliko bora kunakusaidia kupunguza msongo wa mawazo
 • Kujua kuwasiliana kunakusaidia kupunguza kutokuelewana na magomvi yasiyo na msingi
 • Kujua kuwasiliana kuliko bora kunakusaidia sana katika kujenga na kukuza mahusiano yenye afya

Vitu muhimu vya kuzingatia

1. Jifunze kuzungumza na sio kulumbana.

Ipo tofauti kubwa baina ya kuzungumza “conversation” na kulumbana. Mazungumzo ni maongezi ambayo muongeaji ana nia ya kufikia suluhu au lengo jema. Kwenye kulumbana maongezi huweza kuumiza hisia au kuamsha magomvi kwasababu nia iliyopo ni kumtafuta nani mshindi na nani mshindwaji.

2. Kuwa msikilizaji mzuri na taka sana usikilizwe pale inapowezekana.

Wengi wetu ni watu wanaopenza zaidi kuongea na sio kuwasikiliza wengine. Hili ni tatizo kubwa. Katika kuzungumza mtake yule unayeongea naye akusikilize kwanza kile unachotaka kumwambia na akuache umalize unachokizungumza na baada ya hapo yeye pia ataongea ili na wewe umsikiliza. Ni vema ukajua kwamba kwamwe hamtofikia suluhu yeyote kama ninyi wote mtakuwa mkiongea kwa wakati mmoja.

 

  Jinsi gani ya kuwa msikilizaji bora?

 • Sikiliza vema na umuelewe mzungumzaji
 • Elewa kiufasaha lengo la kinachozungumzwa
 • Uliza bila woga pale unapodhani haujaelewa vema
 • Baada ya kuelewa kile kilichosemwa, kizungumze kwa muhtasari kwa maneno yako ili kumwonyesha aliyezungumza kuwa umempata vema
 • Onyesha wazi kukubaliana kwako, na kama haukubaliani basi toa sababu za kutokukubaliana kwako.

3. Jifunze kuwa mzungumzaji jasiri

 1. Ujasiri wako unaupa nguvu ujumbe wako. Kwa maneno mengine ni kwamba jinsi unavyoonyesha ujasiri ndivyo jinsi ujumbe wako hupata nguvu katika kumshawishi au kuwashawishi wanaokusikiliza.
 2. Ujasiri wako hukamata akili na nafsi za msikilizaji wako kwa urahisi zaidi.
 3. Kamwe usimruhusu msikilizaji/wasikilizaji wako kuona au kugundua kwamba hauna ujasiri.

 Nini cha kufanya ili kuwa mzungumzaji mwenye ujasiri

 1. Tumia sentensi za “mimi” zaidi ya kutumia zile zenye “wewe”. Kwa kawaida mzungumzaji jasiri huweza kuelekeza hoja kwake binafsi na sio kukwepa hoja au jambo. Kwamfano, tumia sentensi kama vile “Ningependa kuongea na wewe” au “Sijafurahishwa na jinsi ulivyofanya”.
 2. Tumia sentensi na sio maswali. Hii itaonyesha kwamba una ujasiri juu yako mwenyewe na katika kile unachokizungumza. Kwamfano, Badala ya kusema “Hivi wewe unaionaje yabia yako sikuhizi” unaweza kusema “Sikuhizi siridhishwi kabisa na tabia yako”
 3. Tumia sentensi za ukiri/kukiri zaidi ya zile zenye kuonyesha lawama.

Sentensi zenye ukiri/kukiri “Confession” ni zile zinazoelezea kile mzungumzaji anachotamani  kuona kinafanyika, wakati sentensi zenye lawama “complaints” ni zile zinazo onyesha kile mzungumzaji asichokitaka. Kwamfano, “Sipendi kabisa unavyonifanyia” Hii ni aina ya sentensi yenye lawama. Mfano wa sentensi ya ukiri ni kama vile “Ningetamani kuona unabadilisha mtazamo wako juu yangu”

4. Jifunze kutumia vema lugha ya mwili  

 1. Vile unavyotumia mwili wako unaweza kufikisha ujumbe fulani, kumbuka mwili wako pekeyake huzungumza. Zaidi ya asilimia 50 ya mawasiliano hufanywa pasipo kuhusisha kinywa, na hata tunapotumia vinywa nyetu, zaidi ya asilimia 60 ya ujumbe tulionao hupenya kupitia mianya mingine ikiwemo lugha ya mwili “body language”. Hapa namaanisha kwamba, mtu anaweza kusema kwa kinywa “Usihofu, nitakusaidia kwasababu ninakupenda” lakini ukiutazama uso wake na macho yake wakati anasema maneno haya unajua fika kuwa hakuna msaada wowote hapo. Tunaposema lugha ya mwili tunahusisha vitu kama vile muonekano wa uso, macho, mikunjo ya juu ya paji la uso “wrinkles”, midomo hususani sehemu ya nje “lips”, pua, jinsi ulivyokaa au ulivyojiweka “posture”, mikono, n.k. Maranyingine hata muonekano wa ulivyovalia unaweza kutuma ujumbe.

Na: Dr. Chris Mauki

Lecturer in Psychology and counseling

University of Dar es Salaam

chrismauki57@gmail.com

www.chrismauki.co.tz

 Dr. Chris Mauki. An expert in Relationships, Social and Counseling Psychology. Lecturer in Psychology: UDSM. Inspirational & Motivational speaker. Family man


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *