DARASA LA ALHAMISI NA DR. CHRIS MAUKI: MBINU ZA KUKUZAIDIA KUWEKA UWIANO MZURI BAINA YA KAZI YAKO NA MAISHA MENGINE

MBINU ZA KUKUZAIDIA KUWEKA UWIANO MZURI BAINA YA KAZI YAKO NA MAISHA MENGINE

“Work – life balance”

Maranyingi ni kitu kinachoonekana hakiwezekani na ni kigumu kwa wengi. Ugumu huu sio tu kwa watu wamaisha ya chini bali hata kwa wenye vipato vikubwa, watu wanchi zinazoendelea nanchi zilizoendelea tayari. Wote bado inatuwiangumu kuweka uwiano wa kazi tunazozifanya na maisha mengine. Hapa kazi namaanisha majukumu yako ya kila siku, kazini kwako, kwenye biashara zako au kokote ulikojiajiri mwenyewe. Je unawezaje kuweka uwiano wa maisha yako ya kazi na maisha mengine kama vile maisha ya kijamii, kuwaona na kuwatembelea ndugu, kuwa na muda na familia, kushiriki ibada, kushiriki michezo, kupumzika au hata kuwa na nyakati za likizo “holidays” na familia yako?.

Bado kuna mvutano na mjadala mkubwa sana kwenye hili suala la kuwa na uwiano mzuri kwenye mazi na maisha mengine, wapo wanaosema hakuna haja ya kuwa na uwiano mzuri kama kweli unapenda unachokifanya, kama kweli unaipenda kazi yako basi komaa nayo, na kama unaipenda familia yako zaidi basi kuwa nayo zaidi. Wengine wanasema haiwezekani ukaweka uwiano wakati unandoto zako unazikimbiza na unataka zote zitimie. Wengine wanasema kama unavitu umepanga kuvifanya kabla haujafa ili uviache kwenye ulimwengu na kuweza kukumbukwa kwavyo basi ningumu sana kusema eti uwe na uwiano wa kile unachofanya na maisha mengine. Pamoja na ukweli wa yote yanayopendekezwa katika mijadala hii bado ukweli unabaki pale pale kwamba wapo waliokimbizana na ndoto zao, wapo waliokimbizana kutimiza majukumu yao ili waaache majina makubwa yanayokumbukwa duniani lakini mashinikizo na misongo ya mawazo ya majukumu hayo hayakuwaruhusu kusimama, wengine wamepata matatizo ya moyo, wengine mashinikizo ya damu na wengine magonjwa ya sonona “depression”. Hii inatuonyesha kwamba kuweka uwiano mzuri wa majukumu yetu ya kila siku na maisha mengine ni jambo la muhimu sana na lisiloepukika. Tunahitaji kile mfanyabiashara na mwandishi maarufu Nigel Marsh anachokiita eneo la katikati “middle ground” ambalo tunaweza kuikusanya furaha ya kazini kwetu na furaha yakutoka maeneo mengine ya maisha, ili kuepuka kuwa na furaha iliyoegemea upande mmoja tu na kupungua pande zingine.

Je tunafikiaje eneo hili?Au tunafanikiwaje katika hili?

1. Tenga muda maalumu wa vitu vinavyokupa furaha

Kama wanavyosema wachumi kwamba kama ukiamua kuwalipa fedha wengine kwanza ili itakayobaki iwe yakwako basi ujue hakuna itakayobaki kwa ajili yako, lakini kama ukianza kwanza kuhifadhi inayokuhusu utakuta fedha ya kumalizanana na wengine inapatikana. Vivyo hivyo kwenye maisha mengine, ukisema utumie muda kwanza kwa mambo yanayowahusu wengine, yanayohusu ofisi au kazi au biashara yako na labda sikumoja utapata muda wako wa kupumzika, nataka nikuahidi kwamba muda huo kamwe hautatokea maana kila siku kitaibuka kitu chakufanya na cha kukuweka bize. Anza kwa kuutenga muda huo kwanza, ruhusu akili yako iufahamu muda huo na kuuheshimu. Muda ambao utafanya vile vitu ambavyo nafsi yako inavikubali sana, inavipenda na kuvifurahia. Vitu hivi vinavyopangwa kwenye muda wa kuitafuta furaha yako binafsi ni pamoja na muda wa mazoezi, kupata kahawa na marafiki jioni, muda wa kusoma kitabu unachokipenda, chakula cha mchana na rafiki, au kupata muda wa kuoga pekeyako kwa furaha nk.

2. Punguza au epukana na vitu vinavyokuongezea mizigo, ongeza vile vinavyokupunguzia mizigo

Viko vitu vingi sana tunajihusisha navyo pasipo kujiuliza au kuvitathmini kwa kina, hatupati muda wakujiuliza kama vitu hivyo ni vya msaada kwetu au vinatuongezea hasara, hatuchunguzi kama vitu hivyo vinatuongezea au kutupunguzia mizigo. Mwanasaikolojia mkongwe Marilyn Puder-York anashauri kila mtu kuweza kujitathmini kama vitu anavyofanya vinamwongezea thamani au vinampunguzia thamani hata kama ni kidogokidogo na kwa muda mrefu. Unaweza kuwa hauoni kwamaana hasara, mzigo au kupunguziwa thamani kunakoletwa na vitu hivi hakutokei ghafla bali taratibu na ukija kugundua ni hatari kubwa. Kwamfano; umeshawahi kutathmini faida au hasara ya kukaa kazini kwa muda mrefu, tena hadi usiku na kuchelewa kurudi nyumbani?, kusikiliza umbea, kupoteza muda kwenye mitandao ya kijamii, au kukaa muda mrefu ukiongea na simu. Vitu hivi hupunguza ufanisi wetu pasipo sisi kujua. Kwa kuamua kujitathmini na kubadili namna tunavyofanya mambo itatusaidia kuhakikisha tunafanya kazi kwa umakini mkubwa, tunamaliza majukumu yetu haraka, tunatoka ofisini au makazini kwetu haraka na kupata muda wa kufanya yale mambo tunayoyafurahia.

3. Jitahidi kutokufanya kila kitu peke yako, na vile uvifanyavyo vifanye kwa ufanisi na kwa muda mfupi

Kila mmoja atakubaliana na ukweli kwamba teknolojia imekuwa sana na inaendelea kukua kila siku. Teknolojia ina faida kubwa ingawa ina hasara zake pia. Teknolojia inatuwezesha kuwa karibu sana na watu wanaotuhusu na pia inatuwezesha kufanya mambo kwa ufanisi mkubwa na kwa muda mfupi zaidi. Kwamfano sikuhizi hauhitaji tena kupoteza muda kufanya manunuzi kwa wewe kuzunguka madukani au kwenye masoko makubwa “shopping malls”, unaweza kuagiza vitu kwenye mtandao na ukaletewa ulipo kama tu unahuduma ya mtandao “internet”. Hauhitaji kuwatembelea watu kumi au ishirini kuwapa taarifa fulani au kupanga nao mpango fulani badala yake unaweza kuwaunganisha kwenye grupu la mtandaoni na wote mkaongelea linalowahusu kila mmoja akiwa alipo, kiufanisi zaidi na mwa muda mfupi sana.

 

Jitahidi pia kugawa majukumu ili usiwe na mambo mengi mezani kwako ya wewe kuyashuhulikia. Ukifanya mambo mengi pekeyako ni dhahiri kwamba utachoka sana na hautopata muda wa kufurahia mazoezi jioni, au kama unatamani kuwahi nyumbani ili ucheze na watoto wako hautoweza kuupata muda huo maana ukirudi unakuwa umechoka sana na ukifika tu unawaza kitanda. Hii ndiyo hali ya familia nyingi leo, wazazi wanarudi nyumbani wameshoka sana hawawezi hata kusema neno la kuchekesha kwa watoto wao au kusoma nao hadithi, unashangaa wiki imeisha watoto hawajamwona baba ingawa kila siku wanasikia gari imetoka na kurudi au wanasikia sauti yake nyumbani. Kama kuna mambo unaweza kusaidiwa na mtumwingine kufanya basi gawa majukumu na ujipunguzie kutokakwenye sahani yako, kwa kufanya hivi utajikuta unayafanya yale yanayobaki kwako kwa ufanisi na kwa muda mfupi. Ili kulifanikisha hili jambo la kugawa majukumu yetu, naomba nikushauri ujitahidi kuwaamini wengine, jifunze kuamini kwamba wao nao wanaweza kufanya mambo kama wewe na yamkini zaidi ya wewe. Usipomwamini mtu katika utendaji kamwe hautoweza kumwachia mwingine jukumu lako maana ndani yako unahofu tu kwamba wataharibu.

4. Weka kipaumbele kwenye muda wa kupumzika na kulala

Wengi wetu tunaweka kipaumbele na mkazo zaidi kwenye kuyatimiza majukumu yetu ya kila siku nakusahau kuweka kipaumbele kwenye muda wa kulala. Hapa ninaposema kulala simaanishi kujiegesha kitandani bali kulala na kupata usingizi kabisa tena kwa muda wakutosha. Kukosa usingizi wa kutosha ni njia mojawapo ya kupata tatizo la kiafya kama vile, msongo wa mawazo, kuchoka kwa fikra, kupungukiwa na nguvu za mwili au hata kuchanganyikiwa.

Kwa bahati mbaya sana maisha yetu yaleo yamefanya kulala kuwe kitu kigumu kwa wengi, na wengine hususani watu wenye mali wanajisifia sana uwezo wao wa kulala muda mfupi sana, utasikia mtu anajigamba, yani mimi naweza kulala masaa matatu tu na ninafanya kazi bila tatizo, hili ni tatizo kubwa na hatari kwa muhusika. Katika maandiko ya raisi mstahafu wa Marekani Bill Clinton anasema “Kila kosa kubwa nililowahi kulifanya maishani mwangu, nililifanya nikiwa nimechoka, hususani kwakukosa kulala vizuri” na hapo Bill Clinton anashauri angalau mtu apate muda wa zaidi kwenye kupumzika usiku, na kwakufanya hivi utaona matokeo yake na furaha iliyomo ndani yake.

Kwa kuweza kupata uwiano mzuri wa kazi na maisha mengine “work-life balance” haimaanishi unatakiwa kufanya mambo makubwa na yaajabu sanaaa. Fahamu tu kwamba vitu vidogo vidogo vinaumuhimu sana kwenye kulifanikisha hili. Kuwa makini sana ni wapi unawekeza muda wako na nguvu zako, na kwakufanya hivi utaboresha sana mahusiano yako na mpenzi wako, na watoto wako, na ndugu zako au hata jamii inayokuzunguka na maisha yako kwa ujumla yatabadilika sana.

Jifunze na jitahidi kuuweka mbele muda wako na yale mambo yanayokupa furaha. Viachilie vile vitu vinavyokuongezea mizigona baki na vile vichache vinavyokuongezea thamani yako. Pata muda mzuri wa kupumzika au kulala, fanya mambo machache na kwa ufanisi, na gawa majukumu. Pamoja na kwamba ofisini kwako wanakuhitaji sana, nyumbani kwako pia wanakuhitaji zaidi na Mungu wako pia anakuhitaji vile vile, usimnyime muda wako. Haya ndio maisha yenye uwiano mzuri na haya ndio mafanikio

By: Chris Mauki (PhD)

University of Dar es Salaam

chrismauki57@gmail.com

www.chrismauki.co.tzDr. Chris Mauki. An expert in Relationships, Social and Counseling Psychology. Lecturer in Psychology: UDSM. Inspirational & Motivational speaker. Family man


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *