DARASA LA ALHAMISI NA DR. CHRIS MAUKI: JINSI YA KUJIJENGEA UWEZO ULIO BORA NA WENYE UFANISI KATIKA KUWASILIANA

JINSI YA KUJIJENGEA UWEZO ULIO BORA NA WENYE UFANISI KATIKA KUWASILIANA

“Becoming an effective communicator”

 

Ni vema tukikubaliana na ukweli kwamba hakuna hata mmoja kati yetu ambaye alizaliwa akijua kuwasiliana. Wote tunajifunza, na inabidi mtu kuamua kukubali kujifunza kuwasiliana ili kuwa muwasilianaji bora. Yamkini ukajiuliza, ni kwanini wengi wetu tunashindwa kuwasiliana vema? Ukweli ni kwamba wengi wetu hatujawahi kufundishwa namna bora za kutuwezesha kuwasiliana vema na pia hatujakubali kujiruhusu kufahamu mbinu bora za mawasiliano yenye ufanisi. Kwahiyo kitu cha muhimu na cha maana kwa sasa ni kama unataka kuyaona mabadiliko ndani yako basi amua kubadilika. Amua leo kuanza safari ya kuelekea kuwa muwasilianaji aliye bora. Zifuatazo ni faida utakazo zipata mara utakapoweza kufanya mawasiliano yaliyo bora na yenye ufanisi:

 • Mawasiliano bora na yenye ufanisi yatarahisisha maisha yako
 • Mawasiliano bora na yenye ufanisi yatakupanulia wigo wa kujulikana
 • Mawasiliano bora na yenye ufanisi yatakusaidia kufikisha ujumbe ipasavyo
 • Mawasiliano bora na yenye ufanisi yatakusaidia kapata matokeo mazuri
 • Mawasiliano bora na yenye ufanisi yatakupunguzia misongo ya mawazo katika maeneo mbali mbali
 • Mawasiliano bora na yenye ufanisi yatakusaidia kupunguza misuguano na kutoelewana na wanaokuzunguka
 • Mawasiliano bora na yenye ufanisi yatakusaidia kuboresha mahusiano yako

Baadhi ya mambo ya kuzingatia

1. Jitahidi kuwa mtu wa kuzungumza na sio mtu wa kubishana

Mazungumzo ni kule kuongea kwenye lengo la kufikia lengo au hitimisho fulani wakati mabishano ni kule kuongea ambako kunapelekea mtu au watu kuumizwa kihisia na pia kumtafuta mshindi na mshindwa.

2. Jitahidi kuwa msikilizaji na tamani sana na wewe kusikilizwa pale inapowezekana.

Wengi wetu tunapenda sana kuongea na sio kusikiliza, hili ni tatizo kwasababu asiye sikilizwa huhisi kuumia sana ndani yake. Kama ambavyo unahisi unahaki ya kuzungumza kwenye hilo jambo unalotaka kulizungumza basi vivyo hivyo unahaki pia ya kusikiliza wakati mwingine anaongea. Kama mtu anaongea na wewe, baada ya yeye kuongea au hata anapokuwa anaonyesha kuchukua muda mrefu zaidi kwenye kuongea muombe akupenafasi na wewe uzungumze ili na yeye akusikilize. Yakupasa kufahamu kwamba kamwe hamtafika popote kwenye hicho mnachokiongelea hatakama ni cha muhimu kwa kiasi gani kama wote mtakuwa mnazungumza kwa wakati mmoja.

Jinsi gani ya kuwa msikilizaji mzuri

 • Sikiliza vema na muelewe mzungumzaji
 • Elewa kwa ufasaha madhumuni ya kinachozungumzwa
 • Uliza pale ambapo unaona haujaelewa vema
 • Fanya tathmini ya kile kilichozungumzwa, kiseme kwa muhtasari na

kwa maneno yako ili kuonyesha kama umekipata sawia

 • Onyesha wazi kukubaliana au kutokukubaliana kwako na utoe sababu za kule kukubaliana au kutokubaliana

Jinsi gani ya kuwa mzungumzaji mwenye ujasiri

 • Kwa kule kuwa mzungumzaji mwenye ujasiri kunaupa nguvu ujumbe wako
 • Ujasiri wako katika kuzungumza huziteka hisia za msikilizaji/wasikilizaji wako kiurahisi
 • Usiruhusu kamwe mtu anayekusikiliza akaigundua ile hali ya wewe kutokuwa jasiri

Mambo ya kuzingatia ili kuwa mzungumzaji mwenye ujasiri

1. Jitahidi sana kutumia sentensi za “mimi” zaidi ya kutumia sentensi za “wewe”. Wakati wowote mzungumzaji aliye jasiri ataielezea hali fulani akiihusisha na yeye na sio kukwepa au kujitetea. Kwamfano badala ya kusema “Najua wewe hunipendi ndio maana umenifanyia hivi” basi unaweza kusema “Mimi sifurahii vile unavyovifanyia.

2. Jitahidi na jifunze kutumia “sentensi” zaidi ya kutumia “maswali”. Hii itaonyesha kuwa una ujasiri katika kile unachokizungumza na kwa wewe mwenyewe pia. Kwamfano, badala ya kusema “Hivi mnamwonaje boss wetu sikuhizi?” Unatakiwa kusema “Mimi sifurahishwi na tabia za boss wetu”

3. Jitahidi kutumia sentensi za ukiri zaidi kuliko kutumia sentensi za lawama. Sentensi za ukiri ni zile ambazo zinaelezea nini mzungumzaji angependa kuona kinafanyika au kinatokea, wakati kwa upande mwingine sentensi za lawama ni zile zinazoonyesha kile ambacho mzungumzaji hapendi kukiona. Kwa mfano, mtu kusema “Sipendi jinsi unavyonifanyia” hii ni sentensi ya lawama. Kwa upande mwingine mtu akisema “Ninatamani uwe na mtazamo mzuri juu yangu” hii ni sentensi ya ukiri.

 

Jifunze kutumia vema lugha ya mwili wako (body language)

Je unatumia mwili wako kwa namna gani au kwa kiwango gani katika kufikisha ujumbe? Kumbuka kwamba mwili wako waweza kuongea na kutuma ujumbe mkubwa sana pasipo hata kuzungumza kwa kinywa chako. Wataalamu wa mawasiliano wanasema kwamba zaidi ya asilimia 50 ya mawasiliano hufanyika nje ya mawasiliano ya kinywa (verbal) na hata nyakati tunapotumia vinywa vyetu zaidi ya asilimia 60 ya ujumbe hupenya kupitia maeneo mengine ukihusisha lugha ya mwili (non-verbal). Maeneo haya ni kama vile muonekano wa uso wako (facial impression), namna ndita zako zilivyo au zinavyofanywa, macho yako, pua yako, au vile unavyouweka mwili wako (pose). Mara nyingine hata namna tunavyovaa huhusika pia.

 

By: Chris Mauki (PhD)

University of Dar es Salaam

chrismauki57@gmail.com

www.chrismauki.co.tzDr. Chris Mauki. An expert in Relationships, Social and Counseling Psychology. Lecturer in Psychology: UDSM. Inspirational & Motivational speaker. Family man


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *