DARASA LA ALHAMISI NA DR. CHRIS MAUKI: NAMNA YA KUKABILIANA NA NYAKATI ZA HUZUNI, MASONONEKO, MAUMIVU YA MOYO AU MAOMBOLEZO

NAMNA YA KUKABILIANA NA NYAKATI ZA HUZUNI, MASONONEKO, MAUMIVU YA MOYO AU MAOMBOLEZO

Ni ukweli usiopingika kwamba japokuwa maisha yana nyakati nzuri na zenye kumbukumbu za kufurahisha lakini zipo nyakati ambazo huleta huzuni, maombolezo na masononeko tele. Japokuwa nyakati hizi haziji mara kwa mara maishani mwetu na yamkini ipindi vyake ni vya muda mfupi lakini kama hauna ujuzi wa nini chakufanya nyakati hizi zinapokujia basi fahamu kwamba zitakutesa sana. Leo nataka kukupa baadhi ya vitu muhimu vya kuzingatia ili kubaki imara hata katika nyakati kama hizi na kupunguza madhara yake katika maisha yako. Tukisema tuzuie kabisa nyakati hizi zisitujie tutakuwa tunadanganyana, viko vitu na yako mambo ambayo ni lazima kutokea na hatuwezi kukwepa. Yapo mazingira ya bahati mbaya ambazo hutokea maishani, zipo nyakati tunapata hasara, zipo nyakati tunaumia, tunauguza, tunafiwa na kuwapoteza tuwapendao. Tusisahau pia kuwa zipo nyakati tunakuwa kwenye mapenzi na nyakati nyingine mapenzi hayo yanatusababishia maumivu makali na maranyingine yanavunjika kabisa. Kuna nyakati tunaishi vizuri sana na marafiki zetu na tunashibana mno na muda unafika tunalazimika kuachana nao, labda wanasafiri au sisi tunasafiri au kuhama eneo fulani na unalazimika kusema “kwaheri”, sio marazote neno hili “kwaheri” linafurahiwa, maranyingine linaleta maumivu makubwa na huzuni moyoni Kinachotakiwa ni kufahamu nini chakufanya ili kupenya ukiwa salama.

Wako ambao wanajaribu kila wakati kuepuka kusema kwaheri wakati wa kuagana na wanaowapenda ili tu kukwepa maumivu, wapo wanaosema sio vema kuzungumza habari hizi maana unapozungumzia mambo ya maumivu na masononeko ndiyo unapoyafungulia mlango kuyakaribisha. Pamoja na hayo yote ukweli unabaki pale pale kwamba maranyingine nyakati hizi haazina budi kutujia. Ipo shida pale wengine wanapopingana na ukweli huu au wengine wanapokataa kuachilia yale yaliyokwisha kuwatokea. Hapo unaongeza ukubwa wa tatizo badala ya kuupunguza, unaongeza maumivu badala ya kuyapunguza. Maranyingine uponyaji unakuja kwa kukubaliana na ukweli na kuyaruhusu maumivu yaje kwa jinsi yanavyokuja na kujipanga kukabiliana na maumivu hayo hadi pale yanapokwisha ili yakikuacha basi yakuache jumla na sio kuendelea kukutesa muda wote unaoishi. Kuna mwandishi aliyewahi kuandika akasema kila huzuni inaweza kuwa mzazi wa furaha ambayo haukuwahi kuifikiria, ingawa zipo baadhi ya furaha pia ambazo usipokuwa makini zinaweza kukuingiza kwenye huzuni na masononeko makubwa. Maranyingine usikwepe kuangukia kwenye huzuni maana yaweza kufungua mlango mzuri kama ukiweza kukabiliana vema na huzuni ile. Hapa ninatamani kukusaidia nini chakufanya ili ufungue mlango wa mema baada ya nyakati za huzuni na maumivu ya moyo.

1. Jiachilie, usiweke hisia nyingi kwenye hicho ulichokiacha au ulichokipoteza “Relax”

Unajua maranyingine chini ya sakafu ya mioyo yetu tunajua kabisa kwamba  huyu mtu aameshaondoka, na hatorudi tena, au hii hasara ni dhahiri na hakuna chakufanya ndiyo imeshatokea, ila nafsi zetu zinashikilia hisia za kitu kile na kutotaka kuziachia, na hili huongeza maumivu sana kwetu na maumivu haya yanaweza kudumu kwa muda. Tulia, tuliza hisia zako, kaachini na upumue kwa mafundo makubwa,  pumua ndani na pumua nje taratibu ukiitoa hewa uliyoiingiza, fanya hivi kwa muda kidogo huku ukijiambia “wacha tu itokee”, Jiambie…“hainashida, hili litapita na kila kitu kitarudi kuwa sawa”. Kwa kufanya hivi na kujaribu tena na tena utaona kuwa inafanya kazi na unarudisha nguvu ndani yako, nguvu iliyopotezwa kwa yale maumivu ya kwanza. Unapokutana na machungu, maumivu, au magumu mengine, jambo la kwanza kabla ya kuiangalia hofu na hatari iangalie fursa chanya mbele na kujiambia kwamba hakuna anayekufa au atakayepoteza uhai na kwamba maisha yanaweza kuendelea pia.

2. Weka kipaumbele chako kwenye furaha iliyopo
Hata katika nyakati ngumu na zenye maumivu makubwa ya moyo, vipo vitu hatakama ni vichache ambayo bado vinaweza kukupa furaha au basi hata kukupa tabasamu kidogo. Jiulize na uangalie mazingira uliyonayo, nini huwa kinakupa furaha au kukufanya walau ujisikie vizuri unapokuwa katika magumu. Je ni marafiki? Je ni mpenzi wako? Ni kazi yako?Ni mchezo unaoupenda? Ni chakula fulani? Chochote kile kiwacho, kiandike chini au kichukue na kukitumia nyakati hizi zikujiapo. Kila utakapoweza kuweka akili yako na kipaumbele chako kwenye hivi vitu vidogo vinavyokupatia furaha hata kama ni furaha ndogo utaona jinsi ilivyorahisi kuhama taratibu kutoka kwenye hisia chungu na zenye kukuumiza ambazo zimeletwa na lile lililotokea. Angalizo, kuwa makini sana hapa kwenye kuchagua vitu vyakukupa furaha, unapochagua vitu hasi au vitu vyenye madhara basi nirahisi sana kutumbukia katika janga la tabia ngumu au “addictions”, kwa mfano ukajiingiza katika unywaji au uvutaji au marafiki wabaya ili tu kujifariji. Hapo utajiingiza kwenye tatizo kubwa na la muda mrefu kuliko lile janga la awali. Kuwa makini kwenye uchaguzi wakowa wapi na katika kipi uitafute furaha yako

3. Vuta fikra za tukio lililowahi kukuletea hiyo furaha

Baada ya kuwaza kitu kinachoweza kukupa furaha katikati ya maumivu na masononeko ya moyo, sasa jaribu kuvuta fikra “recall” katika tukio lililotokea na kukusababishia ile furaha uliyoiwaza kwenye hatua ya pili. Kwamfano, kama uliwaza kuwa mke wako au mume wako ndio anaweza kuwa chanzo cha furaha katika nyakati unazopitia, sasa jaribu kuwaza ni tukio gani lilitokea likakukutanisha naye? Je ni michezo? Ni safari?Ni jeshini au shuleni?Waza ilikuwaje? Kama utawaza kuwa nimtoto au watoto wako ndio wanaoweza kukupa furaha katika mapito yako, hembu anza kuvuta fikra za ile siku umegundua una mimba yake au ile siku unamtaarifu mwenza wako kuhusu ujauzito wako, au ilivyokuwa pale hospitali wakati unaambiwa kuwa mwanao ni wakiume au wakike. Kwa kuweza kuweka rekodi ya matukio haya utazidi kupata nguvu ndani yako ya kustahimili nyakati unaazopitia.

4. Endelea kuyatafuta matukio hayo kwenye maisha yako hadi utakapolipata tukio lisilozuri ila lilijeuka chanzo cha furaha
Kumbuka hapa tunajifunza namna ya kujitafutia nguvu itakayotuwezesha kupenya kiushindi katikati ya maumivu na masononeko ya moyo. Kumbuka pia kwamba tumesema hapo awali kwamba yapo matukio tunayopitia tunayaona kama mabaya na yenye kutuumiza ila mbeleni yanaweza kutupeleka kwenye furaha. Hapo awali kwenye hatua za mwanzoni nimekusaidia kuweza kuyatafakari matukio ya nyuma ambayo yanaweza kukupa furaha katikati ya nyakati unazopitia.Ukaweza pia kuvuta fikra za matukio yaliyokuletea furaha hiyo. Sasa katika hatua hii nakusaidia kuendelea kuyatafakari matukio hayo, kuendelea kuyavuta kwenye fikra na kuyachambua mpaka utakapokutana na tukio au matukio ambayo kiukweli usingeyatamani kuyakumbuka kwajinsi yalivyokuwa mabaya, yanayoumiza, yanayokera lakini yalipotokea yalifungua mlango mpya wa furaha maishani mwako. Kwa mfano, katika kuongea na watu mbalimbali kama mshauri wa kisaikolojia “counselor” nimekutana na watu wengine ambao nawasaidia kupitia mchakato kama huu, yupo ambaye baada ya kuwaza sana alisema furaha yangu kwa sasa ni mtoto wangu, ila akichunguza nyuma. Alimpata mtoto huyu baada ya mahusiano na mpenzi wake kuvunjika na mpenzi huyu kumwambia hahusiki katika ujauzito ule, kumbukumbu hii ilimliza sana ila ndio ilikuwa chanzo cha furaha yake.

Mfano wapili ni kijana ambaye furaha yake ilikuwa kazi yake inayompa mshahara mzuri na nikazi anayoifurahia sanasana, lakini anasema akikumbuka maisha aliyoishi hadi kupata shahada yake yalikuwa ni yaliyojaa machozi, ikiwemo kupoteza mzazi wake aliyekuwa anamsomesha, kukataliwa na ndugu aliowaomba wamsaidie kimasomo, kufukuzwa shule mara kadhaa kwa kukosa ada na mengi mengine ingawa leo anapopita katika mapito magumu, ile nguvu ya ustahimilivu iliyompitisha kwenye mapito makubwa na mazito wakati wa masomo inampa kusimama na kumwambia “hata katika hili utaweza tu”. Hembu fikiria kama kijana huyu asingeweza kuzivuta fikra kuyakumbuka matukio ya nyuma kwenye maisha yake, angepata wapi nguvu ya kustahimili katika mapito aliyokuwa anapitia akiwa tayari kazini? Hii inaweza kufanya kazi hata kwako pia. Kila mtu anamatukio kama haya, matukio mazuri, na matukio mabaya ambayo mengine yalionekana kama mabaya sana kwetu ila yakatufungulia milango ya furaha.

5. Zigundue, zitunze na zilee vema nyakati za furaha zinazozaliwa kutoka kwenye mapito yako ya maumivu, na masononeko
Inawezekana sana na nijambo la kibinadamu kabisa kuweka fikra zetu kwenye maumivu, masononeko au haliyakupoteza au hasara tuliyopata na wala hatuangalii fursa zozote nzuri zinazoweza kuibuka kutokana na hasara au mapito yale. Jambo hili limezungumzwa pia bayana na mwanasaikolojia Daniel Gilbert kwenye kitabu chake cha “Stumbling on Happiness”. Watu wanapopoteza mpendwa wao, labda ni mtoto, au ni mzazi, au ndugu mwingine wakaribu, hali huwa mbaya sana siku za mwanzoni, maumivu ya moyo huwa makubwa kama vile mawimbi makubwa ya bahari yavumayo. Wengine hali hii huweza kuchukua hata mwaka mzima, lakini unapokaa nao karibu zipo aina fulani za furaha huibuka baada ya vipindi hivi vya maumivu kuisha, furaha hizi zaweza kuletwa na imani iliyowabeba katika kipindi hicho, au aina ya marafiki waliosimama nao, au kitu kingine chochote. Unapokuwa katikati ya mapito mazito au nyakati zinazofuata baada ya mapito hayo unaweza kuwa kipofu na usione fursa zozote za furaha. Nipo hapa kukutaarifu kwamba usimezwe kabisa na machungu ya moyo ukaacha kufungua macho kuzitambua furaha mpya zinazozaliwa kutoka kwenye mapito yako na mara ukiweza kuzitambua zitunze na uzilee ili ziendeleee kukusababishai furaha kubwa zaidi na kukusahaulisha kiurahisi yale mapito yako makali. Je unajua kwamba katika misiba yetu, maranyingine tunakutana na marafiki wapywa wazuri sana wanaokuja kufanyika furaha kubwa sana maishani mwetu, na kutuacha tukisema “kama sio ule msiba nisingekutana na wewe”, “kama sio ile ajali tusingejuana”. Ukiwa mzembe utaruhusu furaha hizi mpya kufa ila ukiwa makini utazitunza na kuzilea na zitaendelea kukupa furaha zaidi na zaidi na utaonekana mwenye ustahimilivu mkubwa kata upitapo katikati ya nyakati ngumu.

Sasa sijui unapitia nini wakati huu, sijui majonzi yako yanasababishwa nanini, sijui umempoteza nani ambaye amekuuma sana, na yamkini unaona kiza kimetanda na hakuna tumaini tena. Anza sasa kuandika matukio na nyakati zinazoweza kukupa furaha hata kama ni “kafuraha kadogooo”, chunguza mwanzo au chanzo cha cha tukio lililoleta “kafuraha” hako, anza kufikiria kuhusu fursaza furaha zinazoweza kuzaliwa kupitia mapito yako ya sasa. Badili mtazamo wako kutoka kuwa hasi “negative” na kuwa chanya “positive”. “Ruhusu tu litokee, maana liitapita tu. Jitahidi kuliondoa moyoni mwako, liache liende”

 

Imeandaliwa na;

Dr. Chris Mauki

Social, Relationship and Counseling Psychologist

University of Dar es salaam

Chrismauki57@gmail.com

www.chrismauki.co.tz

 Dr. Chris Mauki. An expert in Relationships, Social and Counseling Psychology. Lecturer in Psychology: UDSM. Inspirational & Motivational speaker. Family man


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *