DARASA LA ALHAMISI NA DR. CHRIS MAUKI: IELEWE MILIMA NA MABONDE YA KWENYE MAHUSIANO

IELEWE MILIMA NA MABONDE YA KWENYE MAHUSIANO

Katika ongezeko la kuvunjika kwa ndoa nyingi lililopo duniani sasa, ambalo linahusisha kila nchi, kila kabila, kila tamaduni na hata kila imani, ziko sababu ambazo watafiti wengi wamezigusia kuhusika na changamoto hii. Baadhi ya watafiti hawa ni maprofesa wa chuo kikuu cha Pasific nchini Marekani, Profesa Les na Lesile Parrot. Hawa wametanabaisha kwamba wanandoa wengi huingia kwenye mahusiano pasipo kuwa na ufahamu bayana wa nini maana ya upendo halisi.

Viko vitu vya muhimu sana vihusuvyo mapenzi ambavyo wanandoa wengi na wengine walioko kwenye mahusiano hawavijui na kwahivyo kujikuta wanakutana na wakati mgumu kila wakati. Penzi ni kitu kinachohitaji umakini mkubwa, ni kitu kinachotakiwa kuangaliwa au kulindwa wakati wote na wapenzi husika, sio kitu cha kukidharau tu ukadhani kwasababu kipo basi kitaendelea kuwepo milele, penzi lina kupanda na kushuka, penzi linaathiriwa na vilivyo ndani ya wapendanao na hata vile vilivyonje yao, leo linaweza kuonekana katika hali hii na baada ya miezi michache likawa la tofauti kabisa. Wewe jaribu kufikiria jinsi mlivyokuwa mnapendana kabla ya kuoana au zile siku za kwanza za ndoa yenu, halafu angalia jinsi mlivyo sasa. Kuna tofauti kubwa sana na yawezekana hata hujui kwanini na nini kilitokea. Pamoja na miyumbo yote iliyoko ndani yake, pamoja na milima na mabonde yake, yatupasa kufanya kazi ya ziada na kuwa na jitihada za dhati katika kuhakikisha mahusiano au ndoa inasonga hata katika nyakati ambazo mnaona penzi limeshuka sana baina yenu.

Tafiti zinaonyesha kwamba hapo awali raha na furaha ya penzi kwa wanandoa vilikuwa vinaanza kushuka au kupoa wakati ndoa ina miaka 15 hadi 20. Ukweli ni kwamba sikuhizi hali imebadilika sana na wanandoa wengi wanachokana mapema sana na hii inaenda na tafiti za sasa kwamba wanandoa wengi wanaamua kutengana chini ya miaka 10 ya ndoa na hata kama hawatotengana basi migogoro baina yao huwa ni mikubwa katika hali ya kuwafanya kama wataliki “divorcees” waishio chini ya dari moja. Kitendo cha kustahimili zaidi ya miaka 10, 20, 30 na kuendelea kinagharimu jitihada za dhati na uamuzi wa dhati kabisa wa wanandoa hawa katika kuamua kulilinda penzi lao na kuilinda ndoa yao. Haya mambo hayatokei tu kwa bahati nzuri, la hasha, ni mamuzi ya dhati baina ya wanandoa. Na hili linawezekana sana.

Kati ya tatizo kubwa ambalo watafiti hawa wanaliona ni pamoja na wanandoa kushindwa kujitosheleza au kuzishuhulikia hisia zao binafsi kwanza kabla ya kuanza kutaka kutimiziwa mahitaji ya kihisia na wapenzi wao. Kwa kawaida kuna mahitaji ambayo hainabudi kila mwanandoa kuweza kuyatimiza au kujitosheleza yeye kwanza kabla ya kuwa na kiu ya kutoshelezwa na mwenzako. Kwamfano, unahitaji kujipenda vya kutosha kabla ya kuhitaji upendo toka kwa mwenzako, unahitaji kujithamini kabla ya kuthaminiwa, hali kadhalika kujiheshimu, kujiona unaweza, kujipongeza na mengi mengineyo. Wanandoa wengi huingia kwenye ndoa wakiwa na kiu binafsi ambazo hazijaguswa kabisa, ndani yao wakijua kuwa huyu wanayeingia naye kwenye mahusiano ndio mwenye wajibu wakujaza lile ombwe la mahitaji hayo ya kihisia. Najua fika kuwa mpenzi wako anawajibu wa kujali, kuziheshimu na kuzijaza hisia zako, lakini anajaza kile ambacho wewe umeshakitengeneza tayari, sio yeye ndio anakuja kuwa mtengenezaji wa kwanza, mwisho wake sasa unakuwa na matarajio makubwa kupitiliza kutoka kwa mpenzi wako, yamkini kuliko uwezo wake wa kuyatimiza matarajio hayo na hiyo inakuwa chanzo kikuu cha msongo wa mawazo “stress”. Hakuna mwenye uwezo wa kuzijaza na kuzitimiza kiu zako zote za moyoni isipokuwa Mungu mwenyewe. Tunapoingia kwenye mahusiano, tunaingia tukiwa na lengo la kusaidiana kuzijaza nafasi zenye uhitaji ndani yetu, kila mmoja akimsaidia mwenzake na sio mmoja akiwa na jukumu pekee la kumwezesha mwenzake.

Je wewe upo kwenye mahusiano na mpenzi wa aina gani?

Kutokana natafiti iliyofanywa na kina Parrots, kuna aina nne za mahusiano na wengi wetu tuna mchanganyo wa zaidi ya aina moja ingawa lengo ni kuwa mpenzi halisi.

1. Mpenzi mwenye kiu ya kukufurahisha au kukutimizia “The Pleaser”

Mpenzi wa aina hii wakati wote kiu yake ni kuyatimiza mahitaji yako, mara nyingine anakiu ya kuyatimiza hata yale mahiyaji ambayo sio yako. Watu wa namna hii wanapenda kwa moyo wote lakini sio kwa akili zao. Ni warahisi sana kutoa hitimisho bila kufikiria kwanza, “they easily jump into conclusions”. Kiukweli ukichunguza utakuta watu hawa hawatimizi kiu na mahitaji yako bali mahitaji yao binafsi ila wewe unaweza kuona kama wanatimiza kiu au mahitaji yako. Kwa kutimiza yale mahitaji yako na wao wanajisikia ahueni zaidi kwamaana wanakiu ya kuondokana na kule kujisikia vibaya au kuhukumiwa ndani kwa kushindwa kukufurahisha wewe. Hii inamaana kwamba kwa wewe kufurahi yeye anaondokana na ile hali ya kuhukumiwa ndani “guilty conscious”.

2. Mpenzi msimamizi “The controller”

Mpenzi wa namna hii anatofauti kidogo na yule ya kwanza, huyu anapenda zaidi kwa akili na sio kwa moyo. Watu hawa hawana sana hisia za kuhukumiwa ndani “guilty conscious” ila hawathamini mapenzi pia. Wapenzi wa aina hii wanaweza kuliona tatizo na kulitathmini kabisa lakini inakuwa ngumu kubeba hisia za mhusika, utatamani ahisi au aone unavyosikia au unavyohisi lakini inakuwa ngumu kwake kwahiyo utaendelea kulaumu sana kwamba hajali hisia zako. Wapenzi wa aina hii wakovizuri zaidi katika kuhakikisha mahitaji yao yametimia kwanza kabla ya mahitaji ya mtu mwingine.

3. Mpenzi mmezaji wa vitu “The withholder”

Mpenzi wa aina hii yuko pia tofauti na wengine, inahitaji uvumilivu mkubwa sana kuwa na mtu wa namna hii kwenye mahusiano (sisemi kwamba haiwezekani kuhusiana naye”). Wengi wa watu wa namna hii ni wale ambao wamewahi kuumizwa katika mahusiano yao ya awali na kwa kila mbinu wana kwepa kuumizwa tena au kutoneshwa majeraha yao ya ndani. Wao kila dakika ni kuangalia au kuuliza “mbona umenifanyia hivi au vile”, “unataka nifanye hivi, je wewe umenifanyia hivyo

 4Mpenzi halisi “Genuine Lover”

Huyu ndiye mpenzi pekee utakayekutana naye mwenye uwezo wa kupenda kwa moyo wake wote na kwa akili yake yote. Huyu sio mtu wa kujihisi kuhukumiwa mara kwa mara na anathamini sana mapenzi. Ni mtu mwenye moyo wa mapenzi na anayeweza kuzifahamu hisia zako na kuchukuliana nazo, anaweza kuhisi unavyohisi na kuweza kuvivaa viatu vyako kihisia pia. Mpenzi wa namna hii anaweza kuangalia mambo kwa mtazamo wa mpenzi wake na wala sio kuyachukulia mambo kibinafsi. Uwezo wa kuyaona mambo kwa mtazamo wa mpenzi wake, kuyachukulia kama ambavyo mpenzi wake angeyachukulia, kuyahisi kama ambavyo mpenzi wake angeyahisi, ndiyo zawadi kubwa zaidi kwenye mapenzi. Watu hawazaliwi tu wakiwa na uwezo huu bali unaweza kujifunza na kubadilika kuwa mtu wa namna hii ili kuyaboresha na kuyaendeleza mahusiano au mapenzi yenu.

Na: Dr. Chris Mauki

Mtaalamu wa saikolojia na mahusiano

University of Dar es salaam

0713 407182

chrismauki57@gmail.com

www.chrismauki.co.tz

 Dr. Chris Mauki. An expert in Relationships, Social and Counseling Psychology. Lecturer in Psychology: UDSM. Inspirational & Motivational speaker. Family man


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *