DARASA LA ALHAMISI NA DR. CHRIS MAUKI: AINA ZA WAUME (TYPES OF HUSBANDS)

AINA ZA WAUME

(TYPES OF HUSBANDS)

Mara nyingi kwenye ndoa kumekuwa na malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa wanawake walioolewa “wake”, na malalamiko haya yanaelekezwa kwenye namna waume zao wanavyoishi au wanavyofanya. Huyu analalamika mume wangu yuko hivi, na yule naye anasema mume wangu yuko vile. Mmoja anasema mume wangu anafanya hivi na mwingine analia mume wangu hafanyi vile. Huu mkanganyiko umekuwa mkubwa sana na unasababaisha maumivu kwa wake zetu. Hii ndio maana nimeamua kuna na makala hii itakayokusaidia kufahamu kuwa wanaume pamoja na kwamba wanafanana kijinsia lakini kwenye tabia zao katika ndoa wanatofautiana sana. Labda kwa kuisoma makala hii utajigundua kuwa wewe ni mume wa aina gani (kama wewe ni mume) na labda pia utamgundua mume wako yuko kundi gani kwa kuangalia namna tabia yake ilivyowakilishwa, Nakutakia usomaji mwena na wa kuelewa.

1. Mume bachelor (Bachelor husband)

Mume wa aina hii anapenda sana kufanya mambo kivyake pasipo kumshirikisha mke wake. Anapenda sana kuvinjari na kuwa na marafiki zake sana na sio mke wake, anaweza akashinda baa akajisahau kabisa kama ana mke na watoto, akiwa na rafiki zake anajisikia furaha zaidi kuliko anapokuwa na mkewe au watoto wake. Hata wakipanga kwenda mtoko na mkewe basi lazima atawaita na rafiki zake kadhaa wajumuike naye, wanaume wa hivi ningumu sana kuwapa quality time wakezao. Mkikaa pamoja na yeye na marafiki zake basi mke fahamu ndio umetengwa kabisaaa, wataanza kuongea mambo ya ligi ya uingereza, warudi ligi ya Tanzania halafu wakichoka mpira wahamie siasa, mpaka hapo kichwa kimeshakuuma unatamani kwenda ukajikunyate na watoto wako nyumbani. Wanaume wa hivi kwakweli hawamaanishi sana kwenye masuala ya ndoa. Wao ndoa huichukulia kirahisirahisi tu. Mara zore ni watu wasiionyesha kupevuka au kukua kwenye mambo yanayohusiana na ndoa au familia “They are always pre-mature on things related to marriage and family”.

2. Mume tindikali (Acidic husband)

Yeye anachemka kama tindikali kila wakati. Mkali hatari. Anafujo hatari. Ngumi mkononi. Ukimjibu tu kidogo umeisha. Ukinyamaza anasema kwanini hutaki kujibu anachoongea, kwahiyo anaweza kukuadhibu kwa kumdharau. Kila mara anamudi na ni mbabe kwenye kila jambo. Kiufupi ni mume hatari sana na wakumwogopa wakati wowote ule maana hujui ataamka na kipi

3. Mume mtumwa (Slave husband)

Waume wa namna hii kila mara kiu yao nikutaka wafanyiwe na kuheshimiwa kama wafalme ila wao wanawafanya wakezao kama watumwa. Kila mara huwahimiza sana wakezao kufanya mambo ya mila na tamaduni zazamani katika kuonyesha heshima kwao, hata kitu ambacho anaweza kufanya yeye atataka mke afanye maana nikazi ya mwanamke. Akiangusha kitu mke ndio aje aokote. Hawa ndio wale maranyinyine wanataka mke amsalimie shkamoo baba nanihii, au shkamoo mume wangu. Huwezi kusalimia mumewako haujapiga goti, au kuinama maana ni dhambi. Maranyingine waume wa aina hii hawapendi kabisa kuitwa kwa majina yao ya kwanza, wanapenda kuitwa kwa majina ya ukoo au ya watoto wao, ukimwita jina lake anaona ni dharau kubwa sana.

4. Mume wa jumla (General husband)

Mwanaume wa hivi ni mume wa kila mwanamke. Utaona anawajali wanawake wengine kuliko anavyomjali mke wake. Atawasifia wanawake wengine walivyopendeza na walivyo wazuri wakati mke wake wala hajawahi kuskia sentensi kama hizo kwenye kinywa cha mumewe.  Hata kama hana mahusiano na hao wanawake lakini utaona anapenda sana kuwasaidia hususani kuwapa pesa wakati hata sikumoja hawezi mpa pesa mkewe. Ukiwachunguza marafiki zao wengi ni wanawake kuliko wanaume. Ni mkarimu sana kwa wanawake wengine lakini sio kwa mkewe. Anaweza kuwa rafiki sana kwa marafiki za mkewake kuliko alivyo rafiki kwa mke wake.

5. Mume mkavu (Dry husband)

Mume wahivi ana mudi kila wakati, hujui sangapi anafuraha na sangapi kabadilika. Ningumu sana kuzielewa hisia zake. Unaweza kufikiri anafuraha maana alikuwa anacheka ghafla ukimjeukia unaona kashanuna. Wabahili sana wanaume wahivi. Hawajali kabisa hisia za wake zao. Anaweza kusema neno kavu na chungu mkewe akaumia hata kutoa chozi lakini yeye bado tu anaendelea kubwabwaja maneno bila kujali kuwa amemuumiza mwenzake kihisia. Wanaume wa hivi hawanamuda wowote kwenye kuweka jitihada katika mahusiano yao ili penzi linoge. Wao wanadhani mahusiano mazuri yanakuja tu yenyewe, mkikosana, wewe ndio utahangaika sana kwenye kutafuta suluhu yeye yupo tu wala hana habari. Kiufupi nikwamba waume wa aina hii hawana utu.

6. Mume panadol

Waume wa namna hii marazote huwatumia wakezao kama mashine za kutatua matatizo yao. Wanawapenda wake zao pale ambapo mume anauhitaji fulani na akishafanikiwa kupata ufumbuzi wa hitaji lake basi mke yule hafai tena. Waume wajinsi hii ni wenye akili sana na wajanja, wanajua kila udhaifu wa wake zao na wanatumia madhaifu hayo kupata wanachokitaka kutoka kwa wakezao.

7. Mume mnyonyadamu (Parasite husband)

Mume wa hivi mara nyingi ni mvivu. Hapendi sana kufanya kazi au kujituma. Atajifanya kugandana na mke wake kama vile anamapenzi lakini kumbe ni kutaka kutumia hela au status ya mke wake. Huonekana kama anayejua mapenzi sana lakini hutumia hela za mkewake kuhonga wanawake wengine. Hawa sio watu wagunduzi na wavumbuzi wa vitu, hawezi kuwaza kitu kipya cha kifamilia na ni wagumu sana kusaidia majukumu na kazi za nyumbani.

8. Mume mtoto (Baby husband)

Hawa ni waume wasioweza kabisa kubeba majukumu yao, mara zote wako kama watoto tu. Hawawezi kufanya maamuzi wenyewe pasipo kuuliza mama zao, baba au ndugu wengine. Anapokutana na magumu au changamoto ghafla hukimbilia kwa wazazi wake badala ya kuzungumza na mkewe ili kutafuta sukuhisho. Maranyingi huwataka wakezao wawapende na kuwajali kama vile mama zao walivyofanya na chakushangaza anaweza kabisa kumwambia mkewe “mama yangu alikuwa ananipikia hivi”, mama yangu alikuwa hivi, mama yangu alifanya vile, wewe hufanyi hivi…!! Ni watu wenye kuwalinganisha sana wake zao na mama zao kwenye mambo mengi na hili huwakera sana wake zao na maranyingine kusababisha uadui kati ya wazazi wa mume na mwali wao.

9. Mume mgeni (A visiting husband)

Maranyingi waume wa hivi sio watu wakuwepo nyumbani wao zaidi huwa kazini. Wao wanakuja nyumbani kama vile wageni na nyumbani kunakuwa kama nyumba ya kufikia wageni. Wanajitahidi sana kuhakikisha kila kitu mke anachohitaji na watoto wanachohitaji kinapatikana. Atalipa ada kwa wakati. Atahakikisha mke wake anausafiri au anahela ya matumizi na hata mahitaji mengine yatakuwepo. Watoto wakitaka starehe nyingine atahakikisha wanazipata, nyumbani kutakuwa na wasaidizi na labda dereva wa watoto pia, lakini yeye ningumu sana kuwa na muda na mkewe au watoto wake. Kwakufanya haya yote yeye hudhania amemaliza kazi yote na maranyingine hujipongeza au hata kujisifia kwa wenzake bila kujua kwamba bado kuna kitu chamuhimu sana hajakifanya. Hawa wako bize kila dakika. Hali hii kumweka mke kwenye njia panda kubwa ya mawazo maana akijiangalia kila kitu anachohitaji kipo lakini bado anapungukiwa na penzi na muda wa mumewe, watoto nao wanaona wanakila hitaji lakini kiu ya kuwa na baba kila siku haiishi. Hili sio jambo rahisi kwa mke na watoto. Kama wewe ni wa tabia hii, hongera kwa kazi nzuri unayoifanya katika kusimamia familia yako lakini nakushauri badilika kidogo kwenye eneo la kuwapa familia yako muda wako. Waweke kwenye ratiba zako na utaona mabadikiko makubwa kwao na kwako pia.

10. Mume mzuri

Hawa wanawapenda na kuwajali wake zao. Wakotayari na hawasukumwi katika kuhakikisha wakezao na  watoto wao wanafuraha, wanamahitaji yao na anajali hisia zao. Hujitahidi sana kuhakikisha wanapata muda na wake zao na watoto wao pia. Hujitahidi pia kuwa viongozi wa masuala ya imani kwa wanafamilia wao. Ni watu wasiokwepa majukumu, wanaojibidisha, na wanaowachukulia wake zao kama marafiki, kama wadau katika ujenzi na maendeleo ya familia na pia huwachukulia wake zao kama wasaidizi. Najua ndani yako unaweza kudhani kuwa waume wajinsi hii hawapo, labda walishakufa wote au wako mbinguni tu lakini nikuhakikishie kuwa wapo, hata kama ni wachache, wapo, na nichukue nafasi hii kuwatia moyo waendeleze wema huohuo maana matokeo yake ni matamu sana.

Na: Dr. Chris Mauki

Mtaalamu wa saikolojia na mahusiano

University of Dar es salaam

www.chrismauki.co.tz

 Dr. Chris Mauki. An expert in Relationships, Social and Counseling Psychology. Lecturer in Psychology: UDSM. Inspirational & Motivational speaker. Family man


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *