DARASA LA ALHAMISI NA DR. CHRIS MAUKI: AINA 10 ZA WAKE (10 TYPES OF WIVES)

 

AINA 10 ZA WAKE

(10 TYPES OF WIVES)

1. Mke sherehe (Party wife)

Wake wa aina hii wako mguu na njia kila siku na wanajuana na kila mtu. Wao kila siku wana sherehe, leo sendoff, kesho kichen party, keshokutwa bag party mtondogoo wedding nk. Mara chache wanakaa nyumbani siku za wikiendi, yani zile siku za mume na watoto kuwepo nyumbani yeye ndio party mood  activated. Wanaweza kutumia hela ya chakula cha familia kuchangia sherehe au kununulia zawadi.

2. Mke kamusi (Dictionary wife

Hahitaji kuomba ushauri hata siku moja yeye anachojua ndio mpango mzima. Kila wakati analazimisha mawazo yake yawe sawia na yaaminike. Hataki kupingwa au kurekebishwa kwa chochote. Anatoa oda tu, neno naomba au tafadhali hutolisikia kwake, na ni mkali sana vitu vinavyopotea au kuwekwa vibaya nyumbani tofauti na alivyovipanga yeye.

3. Mke pampas (Pampas wife)

Huyu ni mke aliyeharibiwa kabisa na wazazi wake hususani wazazi matajiri, wazazi wanaojiweza, au labda ndio binti pekee kwao. Wavivu sana kufanya kazi za nyumbani. Wao wanapenda tu shopping na vitu vya fasheni. Maranyingi mke huyu anamwona mume wake kama house boy, utaskia baby nisaidie hiki, baby niletee kile, hubby njoo nitolee hiki, hubby utanipeleka pale. Mume utadhani dereva au shamba boy. Unakuta mume anahasira moyoni lakini ndio hivyo tena kamba ilishaungulia kiwandani.

4 Mke ofisi (The Office wife)

Mke wa aina hii anajali sana majukumu ya kazini kuliko familia yake, anaweza kuwa na muda mrefu sana wa kazi akakosa muda na watoto au mume wake na anatumia majukumu ya kazi kama kisingizio cha kutokuwepo nyumbani au kutotimiza majukumu yake ya mke au mama nyumbani.  Ningumu sana kwa mke wahivi kumheshimu mume wake, na hawa ndio wanaowafanya wanawake wengine waliosoma kuonekana wabaya kwenye ndoa. Mawazo yao nikwamba mume hana umuhimu sana maana hata wao wanaweza kuendesha familia bila shida. Waume wanaoishi na wake wa aina hii wanastahili pole na uvumilivu mkubwa.

5. Mke mgonjwa

Wakati wote anaonekana kama anaumwa, mpole sana na aliyenyong’onyea.  Anapenda kulaumu kila kitu, atalaumu kuhusu mume, watoto, ndugu hata hali ya hewa. Kila wakati wao ni wenye hofu kwa kila kitu, ukimshauri afanye bishara hii anaogopa mwambie nyingine ataogopa, anaweza kulalamika uchovu au kuumwa hata katika nyakati mume anaomba tendo la ndoa. Pamoja na lawama za udhaifu na kuumwa au kuchoka mara kwa mara wala hauoni akisema anaenda hospitali.

6. Mke mwalimu mkuu (Headmistress wife)

Hawa hujiweka kuwa viranja wa familia hatakama mume ndio anayeleta kila kitu. Kila wakati anatamani aonekane yeye ndio kiongozi wa familia. Maranyingi huwafanya wengine wote ni watoto au wanafunzi bila kujali huyu ni mume wake au yule ni mgeni kaja kutembelea familia. Wanauliza maswali kwenye kila kitu, utaskia, kwanini umefanya hivi, kwanini hiki kiko pale, kwanini hivi kwanini vile na pia wanaweza kutoa adhabu hata kwa waume zao kwa vitu visivyo vya maana kabisa. Utaskia “umeamua kufanya hivyo ee!! Basi utaona.

 7. Mke ngumi (fighting wife)

Wake wa namna hii ni wenye kuudhi kila mara na pia mara kwa mara ni wapenda fujo. Anawezakuweka mazingira ya valangati hatakama haukuwa na mpango wa kurusha ngumi ukajikuta mmekunjana, akianza fujo hajali umelala, umepumzika, unaongea na simu, unakula, uko na marafiki, hilo hajali we fahamu tu inakula kwako hadi hasira zake ziishe. Wanapenda kupayuka sana, atarusha maneno kwa sauti ya juu tena maneno yaliyounganika kama vile taarabu na kama ndio mnaishi uswahilini kila jirani atajua kimenuka kwenu. Akianza kuongea hanyamazi, bora nyuki au mbu masikioni kuliko mke wa aina hii. Wake wahivi wanaamini sana kwenye nadharia ya moto kwa moto, ukimwaga ugali anamwaga mboga.

8. Mke ndoo ya taka (Dustbin wife)

Hawa ni wachafu wakati wote na wala hawajipendi kimuonekano, anaweza kuvaa kitu cha gharama lakini bado hauoni kama kavaa kitu. Unawezakumkuta sehemu ya utanashati sanaaa labda ni sherehe ya watu wazito lakini yeye katokelezea kikawaida sanaaaa na wala hajishangai. Wako very unorganised na wako kama wamechanganyikiwa. Ni wavivu wa kila kitu isipokuwa umbea a.k.a ubuyu. Hawa hawafanyi kitu, wao kila kitu dada fanya hivi, dada fanya vile. Yani dada au kaka wa kazi kwao ni zaidi ya punda.

9. Mke mlinzi (Protective wife)

Wake wa aina hii wanawabana sana waume zao. Wana wivu sana na waume zao. Kwake kila mwanamke ni tishio dhidi ya mme wake, hawamuamini mwanamke yoyote kukaribiana na mume wake, hata mume anapokutana na mwanamke ambaye ni rafiki wa mke wake anahofia kumwambia mkewe kuwa nimekutana na rafiki yako kwasababu mke atakosa imani kabisa. Mke wa hivi huwaona marafiki wote wa mume wake kuwa ni maadui na wapotoshaji. Ni wabishi sana kumruhusu mtu mwingine amuadabishe au kumuadhibu mtoto au watoto wake, hawa ndio wale wanaenda shule haraka sana akiskia mwalimu kamchapa mtoto wake au kampigisha magoti mtoto wake na wala hataki kusikia maelezo toyote. Ndugu za mume, marafiki wamume na hata wafanyakazi wa mume wanamuogopa mke wako kama akiwa kundi hili.

10. Mke mzuri (A good wife)

Huyu ndio yule mke ambaye amezungumzwa kwenye zaburi na vitabu vingine vitakatifu. Anajali, anajua kupenda, anapendeza na anawapenda wa kwake. Ni wa msaada. Anaweza kusimamia shuhuli za mumewe asipokuwepo pasipo shida yoyote. Mara zote yeye ni mlinzi na kiongozi wa kiroho kwa watoto na hata familia yote. Ni muelewa sana, mwenye ujasiri na anayejiamini.

Na: Dr. Chris Mauki

Mtaalamu wa saikolojia na mahusiano

University of Dar es salaam

0713 407182

chrismauki57@gmail.com

www.chrismauki.co.tz

 Dr. Chris Mauki. An expert in Relationships, Social and Counseling Psychology. Lecturer in Psychology: UDSM. Inspirational & Motivational speaker. Family man


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *