DARASA LA ALHAMISI na DR. CHRIS MAUKI: CHANGAMOTO ZA KIAFYA NA KISAIKOLOJIA KWA KINAMAMA WANAOLEA WATOTO PEKE YAO “SINGLE MOTHERS”

 

 

SINGLE PARENT

 

 

CHANGAMOTO ZA KIAFYA NA KISAIKOLOJIA KWA KINAMAMA WANAOLEA WATOTO PEKE YAO

 “SINGLE MOTHERS”

Ni kweli kabisa kwamba malezi ya mzazi mmoja wakati wote ni yenye changamoto sana kwa mzazi mwenyewe na hata kwa watoto wanaolelewa na mzazi huyo, hapa namaanisha malezi ya baba peke yake au malezi ya mama pekeyake “single mothers”. Hali hizi hutokea kutokana na sababu tofauti kama vile kufiwa na mwenza, kutengana au kutalikiana kwa wanandoa, na kupata mtoto au watoto pasipo kuolewa au kuishi na mwenza. Utafiti ulioandikwa katika mojawapo ya makala za afya ya jamii umeonyesha kwamba kuna uwezekano mkubwa wa wakinamama wanaolea watoto pasipo waume zao kupata changamoto za kiafya na kisaikolojia, ingawa changamoto hizi zaweza kutofautiana kutokana na maeneo au mazingira ya maisha wanayoishi. Baadhi ya changamoto hizi ni kama vile magonjwa na matatizo ya afya ya akili “mental health issues” ambayo yanauwezekano mkubwa wa kusababisha ugonjwa wa sonona “depression”.

Wanawake waliohusishwa katika utafiti huu walifikia idadi ya 25000 kutoka nchi tofauti duniani na waliulizwa maswali tofauti yakiwemo maswali yahusuyo hali ya zilivyokuwa ndoa zao, hali za watoto wao na changamoto za malezi wanazo kumbana nazo kila siku, sababu zinazokwamisha utendaji kazi wao wa kila siku, changamoto wanazokutana nazo katika maisha binafsi kama vile katika kujipenda, kujijali, na kutafuta furaha binafsi. Wanawake hawa waliulizwa pia kutoa maoni kuhusiana na hali za afya zao.

Ingawa utafiti huu ulihusisha kinamama wa chi tofauti ulimwenguni, asilimia zaidi ya 38 ya kinamama wa nchi za Denmark na Sweden walionyesha kuanza malezi ya mzazi mmoja wakiwa chini ya miaka 50. Asilimia zaidi ya 33 ya wanawake waishio nchini Marekani pia walielezea kuanza kuishi maisha ya malezi ya mzazi mmoja wakiwa chini ya miaka 50. Hali kama hii iliendelea kuonekana kwa akinamama wan chi za uingereza kwa asilimia 22, na nchi nyingine nyingi zilizohusishwa katika utafiti huu.

 

Kwa ujumla, kumeonekana kuwepo kwa uhusiano mkubwa baina ya malezi ya mzazi mmoja wa kike “single mother” na kuongezeka kwa matatizo ya kiafya na kisaikolojia katika miaka ya utu uzima na hata maisha ya uzeeni ukilinganisha na kinamama wanaowalea watoto wao wakisaidiana na waume zao. Wanawake walioonyesha kuwa kwenye hatari kubwa ni wale walioanza malezi ya mzazi mmoja mapema zaidi, hususani wakiwa katika umri ya 20 au chini ya miaka 20. Wengine ni wale walioendelea kulea watoto pekeyao kwa zaidi ya miaka minane na wale wanaolea watoto wawili au zaidi ya wawili wakiwa peke yao, hapa namaanisha pasipo uwepo wa mzazi wa kiume.

Ukubwa wa matatizo haya umeonekana kutofautiana kutoka sehemu moja hadi nyingine. Kwamfano, uhusiano baina ya malezi ya mzazi mmoja na matatizo ya kiafya na kisaikolojia yameonekana kuleta athari hasi “negative effect” chache zaidi kwa wanawake wa nchi za Ulaya tofauti na wanawake wa nchi nyingine. Hali ilionekana kuwa mbaya zaidi kwa wanawake wa nchi za kusini mwa jangwa la Sahara, nchi zinazoendelea au nyingi zilizo masikini, ikiwemo Tanzania. Baadhi ya sababu za kuongezeka au kupungua kwa athari hizi hasi ni kuwepo kwa msaada mkubwa wa ndugu au “social support”. Hali hii inaonekana kukosekana kwa familia nyingi za nchi za kimasikini ambapo kila mtu anayemzunguka mama huyu anaye lea watoto peke yake ni masikini au asiyejiweza, mwisho wa siku hali ya watoto wake ya elimu, chakula, malazi inazidi kuwa ngumu. Ikumbukwe kwamba hii haimaanishi kuwa wanawake wanaojiweza kimaisha hawaathiriki kabisa, la hasha, wao pia wanaweza kuonyesha athari tofauti hususani za kisaikolojia, na hata watoto wao pia. Hali ngumu ya kifedha, ukosefu wa elimu au elimu ndogo pamoja na ukosefu wa fursa za ajira zilionekana pia kuwa sababu kubwa katika kuongeza athari kwa kinamama hawa.

Mtaalam Bella DePaulo, Daktari wa falsafa, na yeye pia ameonyesha kuwa baadhi ya kinamama wanaolea watoto peke yao wanaumizwa au kusumbuliwa na ule unyanyapaa “stigmatization” ya kwamba, ameachika, ameshindwa kuishi na mume, hajaolewa, aliza kabla ya ndoa, watoto wake wameharibika, atawezaje kulea mwenyewe, na maswali yanayofanana na hayo. Pamoja na tatizo hili ambalo limewaathiri wakina mama wengi kisaikolojia, bado wapo wamama wachache ambao wameweza kustahimili na kuishi wakiwa na furaha na kuwapa furaha watoto wao pia.

Pamoja na kwamba athari za kisaikolojia zinaweza kuwakumba akinamama wengi, tena waishio katika maeneo tofauti ulimwenguni, tafiti zimeonyesha kuwa athari za kiafya zinasababishwa zaidi na tofauti za kipato. Kama wanawake wote wangeweza kuwa na kipato sawa, wale wanaoishi na watoto wao peke yao na wale wanaolea pamoja na waume zao basi athari za kiafya zingepungua kwa kiwango sawa au kutoonekana kabisa. Tofauti na suala la athari za kiafya, suala ya unyanyapaa “stigma” na athari zake zinaweza kumuathiri mama yeyote anayewalea watoto wake peke yake bila kujali anauwezo au hana uwezo kifedha. Sasa hapa izingatiwe kwamba yawezekana mama huyu ananyanyapaliwa kweli au yeye binafsi anahisi tu kwamba ananyanyapaliwa. Hali hizi zote zaweza kuleta athari.

Ni kweli kabisa kwamba msaada na ushirikiano wa ndugu unaweza kwa kiasi kikubwa sana kuwasaidia akinamama wa namna hii katika kupunguza athari hasi kwao wenyewe na kwa watoto wao, lakini tafiti zimeonyesha kwamba serikali na mamlaka husika zinaweza kuongeza wigo wa msaada kwa akinamama hawa, hususani katika sera za afya za akinamama na familia, sera za afya na hifadhi ya jamii na maeneo mengine ya maendeleo ya jamii. Kuwepo kwa ushauri nasihi au ushauri wa kisaikolojia katika jamii pia kutasaidia pale ambapo wahusika watahitaji msaada binafsi.

Imeandaliwa na kuandikwa na;

Dr. Chris Mauki

Mtaalamu wa saikolojia, mahusiano na stadi za familia

UDSM/UP

chrismauki57@gmail.com

www.chrismauki.co.tz

 Dr. Chris Mauki. An expert in Relationships, Social and Counseling Psychology. Lecturer in Psychology: UDSM. Inspirational & Motivational speaker. Family man


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *