DARASA LA ALHAMIS na DR. CHRIS MAUKI: NINI CHANZO NA ATHARI ZA HASIRA??

 

Angry Black Man

IELEWE HASIRA NA CHIMBUKO LAKE
(Msaada katika kuyaboresha mahusiano yetu)
Hasira ni hisia nzito zinazoambatana na maumivu ya moyo. Ingawa ni mojawapo yahisia tulizopewa zawadi na Mwenyezi Mungu lakini kila mtu anapokuwa na hasira maranyingi matokeo yake huwa sio mazuri. Takwimu zinaonyesha kuwa hasira ni sababu ya pili kwa ukubwa inayosababisha ajali nyingi katika nchi zilizoendelea hususani Marekani. Hasira imewapa majeraha, vidonda, michubuko na maumivu watu wengi hususani watoto walioumizwa na wazazi wao, wake walioumizwa na waume zao, wafanyakazi walioumizwa na mabosi wao, nk.

Hasira pia imekuwa chanzo cha kuvunjika kwa ndoa nafamilia nyingi, hasa pale ambapo wanandoa wote au mwanandoa mmoja anaposhindwa kuzitumia hasira hizo vema.

Wakati wowote hasira au hali ya kutofautiana inapojipenyeza katika mjadala au mazungumzo yoyote hufanya hali kuwa ngumu katika kufikia suluhisho.

Hasira ni nini?
kama ningekuuliza, hasira ni nini, ungenijibu nini? Je unamaelezo sahihi ya kuelezea hasira au unajua tu kuipata na kuitumia? Ingawa tumeona awali kuwa hasira ni hisia nzito na zenye maumivu ya ndani, lakini nivema kujua kuwa zinaweza kuambatana na hisia nyingine mbaya kama vile machungu, visasi, ukali, vinyongo nk. Hapa ndipo pale mtu anapoweza kulipuka kama bomu, kisa tu alikuwa ameficha hasira tele moyoni.

Hasira yaweza kumpeleka mtu kufanya uharibifu, kuvunja au kulipiza kisasi, hasira huzalisha vita, chuki na maumivu ya moyo pia. Hasira huzalisha vita baridi (cold war), huzalisha kuziriana, hisia kama hizi zaweza kukujia hasa pale unapohisi kudharauliwa, kutukanwa, kudhalilishwa au kukosewa heshima.

Aina hii ya hasira hujitokeza pia katika mahusiano hata ya ndoa na hali huwa ngumu sana, taratibu kunakuwa na mlima mkubwa baina ya wawili wanaopendana na mawasiliano yao yaweza kufa kabisa.

Hatari ya hasira hasa katika mahusiano hujionyesha pia katika jitihada za wapendanao hao kujaribu kuishughulikia au kuipooza hasira hiyo. Mfano wako wanaojifanyisha kama vile hawajakasirika, wanajaribu kuiweza au kuizika hasira yao, lakini kile wanachokizika bado ni hai na kwa kitambo kidogo kitawalipukia na kuwaharibu kupitia magonjwa kama vidonda vya tumbo, magonjwa ya kupooza, mshutuko wa moyo, shinikizo la damu nk.

Hasira inayozikwa, kwa kawaida inabaki ikiwa hai katika nafsi. Wengine wanajaribu kushughulika nayo kwa kujiachia, kuji “express” wanavyotaka na wanavyojihisi, wanafikiri kuwa hii itawasaidia zaidi, lakini tabia hii inakutenga na marafiki zako, wapendwa wako na hata ndugu zako, kila mmoja anakaa mbali na wewe kwa jinsi wanavyo kujua unavyokuwa ukikasirika.
Wengi wetu hujisikia vibaya sana mara baada ya kuzicheuwa harisa zetu, mara baada ya kujiachilia unabaki ukijihisi aibu moyoni, unajihisi kukosa furaha, wengine huirudisha hasira juu yao wenyewe na kuanza kujichukia, kujidharau na kujiona wasiofaa na wasiokitu kabisa.

Hasira huwa tatizo kubwa hasa inapochukua mikondo miwili ifuatayo, Mkondo wa kwanza ni pale mtu anapoionyesha hasira kwa kupitiliza (over reaction) na mkondo wa pili ni pale mtu anapoimeza, kuifukia, au kuificha hasira yake (under reaction).
Mara nyingine mkondo huu wa pili (under reaction) hufanywa pasipo hata anayefanya kujua anafanya nini na kwa athari gani, na kwa hivyo wengine hujikuta wanajiumiza na kutojitendea haki wao wenyewe. Tunapokasirika kupitiliza (ove-react) hasira zetu zina hama mikononi mwetu, zinaanza kutuendesha sisi, sio sisi kuziendesha hasira hizo, hapafujo hujitokeza, majeraha na maumivu pia hudhihirika. Maumivu haya ya nje ya mwili sikitu, ukilinganisha na maumivu ya ndani yanayosababishwa na kuimeza hasira au jujihukumu kutokana na hasira zetu.

Ukweli husu Hasira
Yawezekana umeijua na kuizungumzia hasira kwa muda mrefu lakini hujajua kweli inayohusu hasira na yamkini kweli hii ikawa tofauti na kile ulichokifahamu kuhusu hasira. Hasira sio tatizo na wala sio hisia kuu bali ni dalili tu ya kitu kinachoendelea ndani ya mtu. Kuionyesha au kuiachilia hasira yako kwa umpendae au mhusika yeyote hakuipunguzi hasira ile bali kuipalia makaa ili iwake vizuri.
Jinsi tunavyoitumia hasira yetu ni kitu kinachotakiwa kujifunza, hii inamaanisha unaweza ukajifunza njia au namna mpya zakukabiliana na hasira yako na hivyo kuiweza na sio yenyewe ikuweze wewe. Mwenzako au mpenzi wako hawajibiki kwa chochote katika kukukasirisha, bali wewe unawajibika.

Unajisikia vipi baada ya kuufahamu ukweli huu? Kumbuka kuwa, utendaji kazi wa haya unayoyopata hapa utakusaidia sana katika kuongeza kiwango cha amani na utoshelevu katika mahusiano na maisha yako kwa ujumla.

Nini mizizi ya hasira?
Hasira ni kile kitu tunachokiita hisia ya upili (Secondary emotion) sio hisia ambazo ndio msingi au za kwanza. Ni mchakato mzima wakutuma ujumbe kukuambia kwamba, kuna kitu kinaendelea ndani yako. Hasira husababishwa na hofu, maumivu au kuchanganyikiwa.

Hofu:
Unaweza kuwa na hofu kuwa mpenzi wako atakuzidi nguvu, uwezo au sauti, unaogopa kupeleleshwa au kutawaliwa, unaogopa kudharauliwa au kutoheshimika, basi kwakujilinda na hofu hii unajikuta unawaka hasira.

Wakati wowote unapojihisi kuwa na hasira jiulize, je kuna kitu ninachokiogopa? Hofu yangu ni nini? Hisia zangu zikoje? Usihofu kumwambia mpenzi wako unavyohisi hofu fulani, na kujua kama je yuko tayari mliongelee? Mwambie ni bora mliongelee kuliko ujikute unakarisika.

Maumivu:
Maumivu haya hutoka kona nyingi sana, kwa mfano, mpenzi wako anakwambia neno kali usilolitarajia kutoka kinywani mwake, au unapika chakula kizuri kilichokugharimu muda halafu uliyemwandalia asije, au asile au wala asiseme kitu baada ya kula chakula hicho, unafanya kazi muhimu kubwa na nzito na hata hupokei pongezi toka kwa yeyote, unaweza kuwa umepigwa na unayempenda, au unaweza kugundua kuwa mpenzi wako sio mwaminifu, na mengine mengi yanayo weza kuleta maumivu.

Ili kuyapenyeza nje maumivu yetu, tunaamua kuwa na hasira, tunataka mtu mwingine alipe kwa maumivu yanayotupata, tunatamani kuweka ushindi sawa, umeniumiza! na mimi lazima niziumize hasia zako, lakini tunasahau kuwa kwa kumuumiza mtu mwingine hatuleti usawa tunaoutafuta. Tunapoumizwa hatutaki kukubali uzito wa maumivu yale kinyume chake tunaufunika kwa hasira.

Ukijiona umekasirika, jiulize je ninamaumivu yoyote ndani yangu? Je maumivu haya yanatoka wapi? Kinyume na hasira zako, jaribu kumweleza mpenzi wako kuwa unajisikia kuumizwa, umwelezee ili maumivu yako yasiingie ndani ya moyo na kujeuka hasira.

Kuchanganyikiwa:
Kuchanganyikiwa ndio kuko katika moyo au kiini cha hasira zetu nyingi. Kuchanganyikiwa huku ni kule kunakoitwa kwa kiingereza “frustration”. Neno hili frustration limetokana na neno la kilatini “frustra” maana yake “patupu” au “hakuna kitu”. Mara nyingi tunachanganyikiwa wakati ambapo tunajikuta tuko kwenye tatizo lakini kila tukitafuta suluhisho tunakuta “patupu” hakuna suluhisho la tatizo lile.

Mambo haya magumu yanapotokea katika mahusiano, yakubali kwanza na yaruhusu yawepo pale kwa muda ule huku ukiyatafutia jawabu taratibu, hii itakusaidia kupunguza nguvu ya kuchanganyikiwa. Mruhusu mpenzi wako aongee vile anavyoongea, afanye anavyofanya, awe tofauti na wewe ulivyo, achelewe pale inapobidi na awe kimya inapobidi hii itakusaidia kupunguza kuchanganyikiwa.

Mfano: Umejichosha kufanya usafi nyumba nzima, ukitarajia mpenzi wako atashangazwa na usafi uliopo na kukupongeza sana kwa kazi kubwa uliyoifanya, mara anapoingia ndani hakuna tofauti hata moja anayoiona, wala hasemi neno lolote hali hii yaweza kukupa kuchanganyikiwa na kuchochea hasira kali. Kabla ya kufikia kote huko jiulize kwanza, je ulisafisha nyumba ili uonekane? Je kama asipokuwepo yeye usingefanya usafi? Na je cha muhimu zaidi kwako ni nini? Ni usafi wa nyumba yako au ni macho yake yaone ulichofanya? Je kinachokufurahisha zaidi ni juhudi yako katika nyumba yako au ni jitihada za kumpendezesha yeye? Maswali haya yatakusaidia kupooza moto unaowaka ndani yako ambao ulikuwa unakupeleka kuchanganyikiwa na kukasirika.

Na: Dr. Chris Mauki
Social, Relationship and Counselling Psychologist
UDSM & CHRISTOM SOLUTION
chrismauki57@gmail.com
www.chrismauki.co.tz

 Dr. Chris Mauki. An expert in Relationships, Social and Counseling Psychology. Lecturer in Psychology: UDSM. Inspirational & Motivational speaker. Family man


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *