DARASA LA ALHAMIS na DR. CHRIS MAUKI: ITAMBUE HAIBA YAKO (Know your Personality) PART II

my miriam 2

ITAMBUE HAIBA YAKO
(Know your Personality)
Baada ya kufahamu utofauti mkubwa tulionao kwenye haiba “personalities” zetu, sasa nina jibu swali “Tufanye nini??”

Kitu cha kwanza ni kukubaliana na ukweli kwamba mtazamo wako (jinsi unavyojitazama) hubadilika badilika. Tena hubadilika kiasi ambacho mara nyingine huwezi kutambua. Unaweza kuchagua mwenyewe jinsi unavyotaka mtazamo wako uwe. Kwa mfano;
1. Kufanikiwa au kushindwa
Jaribu kutoangalia nyuma kule ulikowahi kushindwa zaidi, kila mtu anahistoria ya kushindwa sio wewe tu. Wacheza mpira maarufu duniani, mara nyingine hukosa magoli rahisi kabisa lakini hakuna hata mmoja aliye acha kucheza au kuharibu fani yake kwa sababu ya kukosa goli. Wala hakuna aliyekiri kuwa yeye sio bora kwa sababu tu ya kukosa goli moja. Ni vema kukumbuka kule tulikowahi kushindwa kama tu tunataka kujifunza katika makosa yetu, na sio kwa kutaka kujisononesha na kujilaumu kwa namna tulivyokosea. Jifunze kuziacha historia za kufeli na kushindwa zifukiwe katika yaliyopita.

Tengeneza mafanikio yako wewe mwenyewe anza katika hali ya chini kabisa, chagua vile vitu usivyo viweza kabisa kuvifanya mfano; Kuzungumza mbele ya watu, kuimba, kuogelea, kuwa kwenye usaili, kusimama mbele ya kamera n.k anza kuvifanya kwanza kupitia ufahamu wako (viwaze akilini) hali hii inaitwa (creative visualization) ni njia majawapo bora ya kufanya mazoezi ya vile tunavyoshindwa katika fikra zetu, kwanza jitahidi kujitazama fikrani ukiwa au ukifanya vitu hivyo kwa ushindi hadi ufahamu wako utakapoizoea hali hiyo na kuacha kutuma jumbe za kushtuka (kupanick) au uwoga wakati utakapokuwa unafanya vitu vile kihalisi.

Katika kufanya mazoezi ya kufikiria kimtazamo, chagua kufanya katika utulivu mchana au jioni. Muda kabla hujaenda kulala ni mzuri zaidi. Rudia zoezi hili mara kwa mara mpaka uzoee na fikra zizoee.

2. Andika vile vitu uvipendavyo juu yako wewe mwenyewe
Kama kuna mtu anayesema kuwa hana kitu cha kuandika basi mtuhuyo hajafikiri kwa undani au ni mwongo, kila mtu anakitu chema ndani yake.
Kama ukishaandika vitu hivi, angalia tabia ya vile vitu ulivyoviandika pale, kama vitu hivyo vikifanywa na mtu baki usiyemjua je utasema yeye ni mtu mbaya? Kama sio, kwa nini wewe unajiona usiyefaa na uliyejaa mabaya tu?
Badala ya kutazama yale yaliyo mabaya na yakushindwa katika historia yako tazama mafanikio yako. Kila mmoja ana mafanikio ya aina fulani, hata kama ni madodo kiasi gani. Hata kama unatazama yale yaliyowahi kufanyika huko awali basi yatazame katika mtazamo chanya.

Wengi wetu hatuchukui muda kujiuliza vyanzo vya mitazamo yetu hasi, tunaamua kuikubali tu na kuikumbatia na kuifanya asili yetu. Ila mara tu utakapo gundua kuwa tatizo sio lako wewe bali ni mazingira uliyokuziwa au aina ya wazazi uliokuwa nao basi utaacha kujidharau.
Wako watoto wanaofurahia kupelekwa shule za bweni mbali na nyumbani, ila wako ambao hawapendi kabisa lakini wanalazimishwa, hali hii hupandikiza ndani ya watoto hawa upweke, hofu, msongo wa mawazo na kutokutulia (nazungumzia utulivu wa ndani) jambo ambalo huendelea hata katika utu uzima wao. Wako wengi ambao tabia zao za leo zilianza kuharibikia katika shule za bweni mbali na wazazi kwa mfano tabia za kusagana au kuingiliana kinyume na maumbile.

Sisi tumeumbwa katika mifumo na vipindi mbalimbali, mara nyingine tuko chanya (watu wema, wazuri) na mara nyingine tunakuwa hasi (watu wabaya). Kama mtoto atakuwa akiambiwa kila wakati kuwa “kamwe huwezi kuwa na akili kama dada yako” maneno haya hufanyika halisi kwake. Je hujawahi kusikia mtu akisema “mimi sijui kuogelea”, “mimi sijui kama nitaolewa” “Kamwe sitokaa niendeshe gari” , “Mimi sintokaa nijue kiingereza”, “Mimi na kuimba ni tofauti” Haimaanishi kama watu hawa wangeanza kujifunza au kuzaliwa katika mazingira ya vitu hivi, wangevishindwa. Labda kuna sehemu mtu au watu fulani waliwasemea kutoweza au kushindwa na huo ukawa mwanzo wa kuwekewa kizingiti cha ujuzi ndani yao.

Wakati wowote mtu anapojisemea jambo, au neno lililo baya, lisilojenga, lakushindwa, kama utalisema kwa sauti au utalifikiria akilini, katika hali yoyote ile jambo hili hulazimisha uhalisi wa maneno yale kuingia katika mfumo wa maisha yako na kutenda kazi kwa hiyo jifunze kukataa, kukanusha na jitahidi kutenda kinyume na zile sentensi mbaya juu yako. Kama tunaamini utendaji wa kazi wa yale tunayojisemea au kusemewa vibaya basi hata yale tunavyojisemea au kusemewa vema hutenda kazi pia. “If negative proclamation works, surely positive proclamation must work too” Amua kubadilisha yale unayojisema au yale unayosemewa. Badili yale yaliyo negative (yakufeli) yawe positive (yakuweza). Kama hujiamini wewe mwenyewe wala hujithamini, basi utakubali kirahisi kila neno gumu na baya utakaloambiwa na kila mwenye tabia ngumu na kama utayakubali unayoambiwa au unayorushiwa hutaweza kamwe kukabiliana na ushindani kutoka kwa mtu au watu wenye tabia ngumu. Kumbuka daima udhaifu huanzia kwako mwenyewe.

Ukishajifunza kupunguza kujilaumu na kujipinga mwenyewe na kuboresha jinsi unavyojitazama basi utakuwa salama katika kukabiliana na maneno na matendo magumu toka kwa yeyote mwenye tabia ngumu. Na kwa kuwa umejifunza vizuri kujielewa basi sasa waweza kuwaelewa vizuri zaidi wale wenye tabia ngumu. Sasa utaweza kuelewa kuwa kuna kitu kimemfanya au kimewafanya wawe vile walivyo. Mara utakapoweza kumwonea huruma yeyote, haijalishi anatisha kiasi gani basi hawezi tena kukuathiri kwa vyovyote vile.

Kwa jinsi ujasiri wako unavyoongezeka, unaweza pia kuziweka katika matendo mbinu nyingine nyingi za kushuhulika na watu wenye tabia ngumu. Utajikuta unaweza kukabiliana nao na pia kuchukuliana nao katika mazingira tofauti na pia hata katika nyakati ambazo hutakuwa unafanya vizuri katika jambo fulani, hautajilaumu na kujishusha, bali utajisifu kwa kukazana na kujitahidi hata kama haukubahatika.

Dr. Chris Mauki
Social and counselling psychologist
University of Dar es salaam
University of Pretoria
chrismauki57@gmail.com
www.chrismauki.co.tzDr. Chris Mauki. An expert in Relationships, Social and Counseling Psychology. Lecturer in Psychology: UDSM. Inspirational & Motivational speaker. Family man


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *