DARASA LA ALHAMIS na CHRIS MAUKI: MIGOGORO NA UTATUZI WAKE KATIKA MAHUSIANO

Mahusiano ya wengi sanayamefikia katika hali mbaya na mengine kufa kabisa huku wapenzi wakiachana katika maumivu na majeraha makali ya moyo kisa kikubwa kikiwa kutojua kwao kuishughulikia migogoro inayojitokeza katika mahusiano yao.  Mara nyingi katika ushauri tunasema shida sio kujikuta ndani ya migogoro bali shida ni namna mnavyoishughulikia migogoro hiyo.  Unapoona mahusiano ya wengine ni mazuri na ya kutamanisha, haimaanishi nao hawana migogoro, bali wanayo lakini tofauti ni ujuzi wao wa kushughulika na migogoro hiyo.
Kiu yangu ni kwamba, mwisho wa kusoma andiko hili ufahamu namna ya kuboresha mahusiano yako kupitia kujua jinsi bora za kushughulikia migogoro baina yako na mpenzi wako pamoja na wote wanaokuzunguka.
Tunaziona ndoa na mahusiano mengine mengi yakiwa na maumivu, machungu na mapigano kuliko nyakati za amani na maelewano.  wale walioweza kuimarisha amani na maelewano katika mahusiano yao sio kwamba ni mapacha na wanafanana katika kufikiri na kutenda kwao, sio kwamba wameumbwa wenye tabia za kufanana na mtazamo sawa bali ni wale waliojifunza kuchukuliana na tofauti zao, wakizikubali na kuzielewa vema na kila mmoja akijaribu kuujazia udhaifu wa mwenzake, wamejifunza kuzungumza kila mmoja kwa lugha ya mwenzake wakizielewa haiba zao na kubadilika kutokana na hali halisi.
Kwakuwa wote hatufanani, na tofauti hizi tunaingia nazo katika mahusiano yetu, daima lazima tofauti ziibuke baina yetu, na sio kwamba mgogoro huwa mmoja bali huwa mingi, midogo na mikubwa, na wala hili sio jambo baya na lakushangaza bali ni kitu cha kawaida.
Nini maana ya “mgogoro” Ni kutofautiana, baina ya watu, kupingana, kutoafikiana katika jambo fulani au mawazo fulani.
Kati ya njia za kizamani ambazo zinatumika na wapenzi wengine katika kushughulikia migogoro ni kuinyamazisha, kuifukia na kujitahidi kuisahau migogoro hiyo, njia hii imetumika sana hasa kwa wale wanaoshika dini zao.  Kwa kuzika na kufunika migogoro hatutatui bali tunajenga na kukomaza maumivu ya ndani na chuki ambayo taratibu inabadilisha mitazamo yetu kuwa mibaya kwa wale tunaowapenda.  Kumbuka, tofauti hizi zinapozikwa, huzikwa zikiwa hai, na hivyo lazima zitafufuka na kuleta shida.
Wapendanao wengine hushughulikia migogoro yao kwa kuamua kupakua kila kilichopo moyoni na kukimwaga kwa aliyewaudhi, tumesikia wengi wakisema “mpe vidonge vyake”, “mpakulie” kwa wengine njia hii imezaa vita na magomvi tele.  Neno baada ya neno, jibizano baada ya jibizano na hatimaye kofi na ngumi navyo vikaingia kazini.
Kutokana na tafiti tulizozifanya kwa wanandoa wengi na wale wengine walio katika mahusiano, wengi wameelezea kuumizwa sana na viugomvi vya mara kwa mara vinavyosababishwa na mgogoro fulani baina yao, kumbuka kuwa migogoro inaweza kushughulikiwa pasipo magomvi.
Ugomvi maana yake ni vita ya maneno ambayo inaruhusu hisia za hasira kuchukua nafasi, na hapa wapenzi hawaangalii tena sababu za mgogoro wao bali wanaanza kulengana wenyewe binafsi na kushushiana maneno, matusi na lawama,  kwa wale wanoamini vitabu vitakatifu vinasema “wapumbavu hugombana wakati wote bali wanaoepusha magomvi huleta heshima”.
Katika kushughulikia migogoro inakupasa uyafahamu haya.
1.       Migogoro ni jambo asilia na kwahiyo haliepukiki
Kama nilivyokwisha kusema awali kwamba wote sisi tumetokea katika tofauti, mitazamo yetu na matakwa yetu ni tofauti na kwahiyo tutegemee kabisa kutofautiana katika chaguzi zetu, mapendeleo yetu, mitazamo yetu nk.  Migogoro pia haiepukiki hususani kwa watu wanaopendana na wenye kiu ya kudumisha pendo lao zaidi. Migogoro ya mara kwa mara baina ya wanandoa ni ile ya maneno, hii kwa jinsi ilivyo peke yake haidhuru kitu, kwa kugemea na kupevuka kwa wale waliotofautiana. Wako wanaoweza kutofautiana, wakalumbana kwa maneno na wakaishia mwisho mwema, wako wanaolumbana na kushia katika kutwangana.
2.       Migogoro huonyesha kunyimwa au kudhulumiwa kwa hadhi au hitaji la mmoja baina ya wapendanao
Kila mtu ana mahitaji binafsi na ya msingi katika mahusiano, mtafiti William Glaser anasema kati ya mahitaji ya msingi ya mwanadamu ni hitaji la kupenda na kupendwa na hitaji la kujiona au kuonwa wathamani na unayefaa na unayestahili.  Mara unapoingia katika mgogoro na mpenzi wako, hembu jiulize, ni hitaji gani ambalo halijatimizwa? Maana kwa kutokutimizwa kwa hitaji lolote lako lazima itapelekea mgogoro kunyanyuka.
3.       Migogoro wakati wowote ni dalili ya hitaji lililofichika au lililojificha
 Wakati wowote unapojikuta katika mgogoro kunakuwa na hitaji ambalo halijatatuliwa au kupatiwa ufumbuzi.  Kwa kutatua mgogoro yamkini isiwe njia ya kulisuluhisha tatizo, ni bora waangalie kwa undani dalili hizo ili ugundue hitaji ambalo mwenzako amekazana kulitimiza na baada ya kuligundua basi litatue tatizo hilo na sio kutatua dalili zake tu.
4.       Migogoro mingi haishughulikiwi kwa uwazi kwasababu wengi wetu hatujajifunza njia bora za kutatua migogoro hiyo.
Wapendanao wengi hudharau vimigogoro vidogo vidogo, wakiviepusha visisumbue mahusiano yao, na mara migogoro mikubwa ijapo, watu hawa huiepuka pia maana hawajui namna ya kukabiliana na hata ile midogo.  Kamahujui kushughulikia migogoro midogo, je hiyo mikubwa utaiwezea wapi? Hakuna vijimigogoro katika mahusiano, yote huitwa migogiro na inastahili kupatiwa uzito sawa katika kushuhulikiwa na sio kudharauliwa maana athari zake ni kubwa.
5.       Migogoro inatoa fursa ya mahusiano yetu kukua
Migogoro inafananishwa na baruti, baruti yaweza kuleta uharibifu mkubwa ikitumiwa vibaya na pia yaweza kuleta mabadiliko mazuri ikitumiwa vizuri. Ni baruti hiyohiyo iwezayo kuvunja nyumba na kuua lakini ni baruti hiyohiyo iwezayo kuondoa mlima au kichuguu ili kutengeneza barabara au nyumba nzuri.  Kupitia migogoro mtu anaweza akazishirikisha tofauti zake kwa mwingine, kukutana na migogoro kunakupa fursa pia ya kuonja nguvu ya mwenzako.  Kila mmoja akiwa katika mgogoro hujaribu kuleta njia mbadala ya kulijadili suluhisho, njia hizi zaweza kuangaliwa na wote na baadaye kufikia maamuzi mema pale mgogoro unaposuluhishwa, wote hujengwa na kukua.  Lazima  ujifunze  kujua kuwa  kutofautiana katika mahusiano  ni kitu kimoja na matokeo ya kule  hutofautiana kwetu ni kitu kingine, na wala vituhivi havioani.  Ndio maana kutofautiana kwa wapenzi fulani kwaweza kuleta matokeo mazuri wakati kutofautiana kwa wapenzi wengine kukaharibu kila kitu.
6.       Migororo isiyosuluhishwa au kutafutiwa ufumbuzi huathiri ubora wa mahusiano na kufanya wapendanao kutokujihisi kutosheka na penzi lao.

Migororo isipotafutiwa ufumbuzi vikwazo kuinuka mara kwa mara na wapendanao hujikuta wanakuwa wenye kukwepa na kujihami katika kila kitu kwasababu ya kuogopa kuumizwa, tabia hii ni kitanzi katika mahsuiano, kamwe msitegemee penzi lenu kukua kwa staili hii.

(Je wewe unafanya nini unapojikuta katika migogoro kwenye mahusiano yako??? Usikose sehemu ya 2 Alhamis ijayo)Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *